Tanzania inaweza kuwa nchi pekee yenye viti vingi vya ubunge utokanao na vitu vyenye kila aina ya ubaguzi hata udhalilishaji chini ya dhana ya viti maalumu-wabunge wasio na kazi yoyote bungeni zaidi ya kungojea posho na sifa ndogo ndogo magazetini.
Kimsingi, hakuna mantiki ya kumpa mtu eti kuwakilisha vijana kwenye bunge, huyu mbunge wa kawaida ambaye jimbo lake lina kila aina ya binadamu atawakilisha nani? Je vijana au wanawake wana nini cha zaidi hadi kuwa na wawakilishi zaidi ya mmoja?
Kimsingi ubunge uwe wa vijana wazazi, wanawake na upuuzi mwingine ni iwizi wa pesa ya mlipa kodi unaofanywa na wanasiasa. Bahati mbaya hata vyama vya upinzani vimeuingia mtego huu na kushiriki dhambi hii. Siku hizi kila sehemu zinasikika nyimbo na ngonjera za demokrasia na usawa baina ya mwanamke na mwanaume. Hivi kweli kumpa mtu kiti kwa kigezo maalum na jina maalumu kama viti maalum si kumtukana na kumdhalilisha? Kwanini, kama tunawapenda na kuwathamini wanawake, tunawatengea viti vichache tu? Kwanini tusijenge mazingira ya ushindani wa haki na uchaguzi huru ili wanawake na wanaume na wanawake wapambane na atakayeshinda awe mbunge? Kwanini kuwadhalilisha na kuwagawana vijana na wanawake ambao kimsingi ni wengi na wakiamua kutumia wingi wao kwa busara hawana haja ya kupewa upuuzi unaoitwa viti maalum.
Umefika wakati wa kuwaambia vijana na wanawake kuwa viti maalum si suluhisho wala ukombozi kwao bali nyenzo ya kuwapumbaza na kuwagawanya ili wasitumie nguvu yao ya wingi kuamua nani awe mbunge hata rais. Hakuna asiyejua kuwa, kwa mfano, wanawake wengi walioteuliwa kwenye viti maalum wengi wanaonekana kwa jicho baya. Wapo wanaowaona kama kupe waliobebwa na watu fulani na kupewa ulaji huku wengine wakifikia hata kuvidhalilisha viti hivyo kwa kuviita viti vya chupi. Tumefikia mahali hata spika wa bunge anachaguliwa kwa jinsi yake badala ya sifa! Huku si kumkomboa mwanamke bali kumdhalilisha.
Ukiachia kudhalilishwa kwa viti hivi maalum, wengi wa wanufaika wa nafasi hizi ni watu ima ambao ni watoto wa wakubwa au wenye kuwa karibu na wakubwa chamani jambo ambalo limeleta malalamiko mengi karibu katika vyama vyote. Wengine wanasemekana kupata nafasi hizi kupitia rushwa na jinai nyingine kama kujuana, ukabila hata ujimbo. Anayebishia hili ajikumbushe majina ya akina mama wengi wabunge wa kuteuliwa ambao waume zao au baba zao wana madaraka atajua tunachomaanisha. Huku si kumkomboa mwanamke bali kumnyonya, kumtumia na kumdhalilisha.
Kwa vijana na wanawake kilichofanyika ni sawa na kuwatupia mbwa mfupa halafu mwizi aliyefanya hivyo akapata upenyo wa kuiba toka kwenye lindo la mbwa hao hao. Kuna haja ya kuwaambia wabunge wa kuteuliwa na viti maalum kuwa wanachofanya licha ya kuwa kazi ya kutumiwa, wanahujumu uchumi wetu. Hawana kazi bungeni zaidi ya kuwakilisha matumbo yao na wale waliowapigia kifua. Kimsingi, hawa si wabunge bali wala vya dezo vya umma. Kuwaambia ukweli ndiyo njia pekee ya kuwakomboa kuliko hawa wanaowatumia na kuendelea kutafuta jinsi ya kuhami jinai hii iliyohalalishwa.
Ukiangalia nchi ombaomba kama Tanzania kuwa na utitiri wa wabunge hata majimbo ya uchaguzi na mikoa unashangaa uwezo wetu wa kufikiri. Badala ya kujibana na kusogeza nchi yetu mbele, tumeruhusu kundi la watu wachache kupeana ulaji tena kwa kulipana kodi zetu! Kimsingi, hata tukiamua kutumia sheria zilizopo hasa katika inayolaani ubaguzi wa aina yoyote na kuhimiza usawa, viti maalum ni haramu na wizi unaohalalishwa kwa vile unatendwa na wanaoitwa waheshimiwa. Kwanini kwa mfano jimbo la Lushoto kuwa na wabunge maalum wakati mbunge wa jimbo anawakilisha aina zote za watu kuanzia wanawake, wanaume, wazee, vijana, watoto na kadhalika?
Kisheria kuwapa watu ubunge au kazi kwa kuangalia umri, jinsi, watokako na kadhalika ni uvunjaji wa katiba na sheria uanopaswa kuwafikisha wahusika gerezani. Je kuwapa wanawake ubunge kwa kuangalia jinsia yao siyo kuwabugua wanaume na hata kuwadhalilisha wanawake wenyewe? Au kwa vile ubunge ni ulaji basi wanawake wameridhika kuhongwa, kudhalilishwa na kubaguliwa katika taasisi za nchi? Kama wao wameridhika na dhihaka na jinai hii sisi kazi yetu kuwastua kuwa wasidhani kwa kupewa viti viwili vitatu vya udhalilishaji wamepata. Badala yake wamepunjwa na kupatikana. Hii yote huenda inatokana na kuwa na malengo madogo na mafupi kisiasa na ile hali ya wenye vyama kuwagaawana na kuwadhoofisha kimawazo.
Kimsingi viti maalumu licha ya kuwa nyenzo za kuibia kodi yetu na kutuwekea viongozi wa kupandikizwa na vikundi vya watu, ni chambo cha kuwaziba midomo mbwa wasiwapigie kelele wezi.
Je kuwapa vijana ubunge kwa kuangalia ujana siyo kuwabagua wazee? Mwanzoni mwa mwaka huu kuliamriwa kesi ya kihistoria iliyotufanya wachambuzi wa mambo tuliangalie upya suala zima la ubaguzi.
Je mnapotoa viti maalumu kwa mfano kwa jumuia ya wazazi. Hii siyo kuwabagua wasiozaa au ambao wameishaacha kuzaa? Wazazi hawahitaji hata kuwa na jumuia maana hata wabunge wa kuchaguliwa ni wazazi au wana wazazi pia na kama ni wanawake na wengine ni wanawake na kama ni vijana na wengine ni vijana.
Chimbuko la viti maalum ni mfumo wa chama kimoja uliowatumia ukiwahadaa kuwa walikuwa viognozi wa kesho. kuepuka changamoto na wingi wa wanawake na vijana ilibidi uundwe uchochoro wa kuwazuga, kuwagawanya ili wasikengeuke na kudai wao ni taifa la leo. mfumo wa chama kimoja uliona hatari ya vijana na wanawake kama wangeachwa bila kupewa kitu cha kuwahangaisha huku wakijenga chuki miongoni mwao kama ilivyo sasa ili kutotishia nafasi za wakubwa ambao mara nyingi waliwatumia vijana kwenye kila aina ya miradi na kampeni zenye faida kwao.
Sababu nyingine ya kuundwa jumuia za vijana ilikuwa ni kuwezesha kuwafuatilia na kuwadhibiti. Ukichunguza, kwa mfano, jumuia za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kuingia mfumo-zengwe wa vyama vingi vinavyoendeshwa na katiba ya chama kimoja, zilikuwa kama taasisi za ujasusi ya kuchunguzana baina ya vijana kwa vijana ndani ya chama.
Makala moja haitoshi kueleza ubovu na sababu za kuwapo ubunge wa aibu wa kudhalilishana. Tukipata muda siku nyingine tutauchambua tena. Kimsingi, kuna haja ya kubatilisha haraka ubunge huu haramu.
Chanzo: Dira Februari, 2012.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.