Hakuna shaka kuwa Edward Lowassa waziri mkuu aliyetimka madarakani kutokana na kuingiza kampuni feki ya Richmond iliyoishia kuleta maafa kwa taifa, ni mtu ambaye amegeuka kuwa mkarimu hata kupita kiasi.
Hivi karibuni akiwa Kigoma akichangia shule ya Sekondari ya FPCT Bigabiro, Kigoma, alitoa mchango wa shilingi 60, 500,000 cash ukiwa ni mchango wake na marafiki zake ambao hawatajwi kwa majina. Huu si mchango mnono wa kwanza wa Lowassa hasa baada ya kuondoka madarakani. Wengi wanajiuliza: Kama ana uchungu na taifa hili kiasi cha kulitakia maendeleo na mengine mema, mbona alitumia nafasi yake kujinufaisha kwa kuingiza kampuni feki iliyoliingiza taifa kwenye zahama? Mwaka 2006 alichanga jumla ya shilingi shilingi 60, 000,000 kati ya sh 88,340,000 kwa ajili ya shule ya sekondari ya michezo ya Kigamboni. Hapa bado hatujaorodhesha michango mingine ya kuanzia shilingi 10,000,000 kwenda juu ambazo Lowassa ameishachangia kwa vituo vya yatima, kuzindua album, makanisa na mingine mingi.
Je hii pesa inayochangwa imepatikana kihalali au ni matunda ya tuhuma zake za Richmond na nyingine za zamani za marehemu baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyedai mwaka 1995 kuwa Lowassa amejilimbikizia utajiri mwingi ambao hautokani na kipato halali-asioweza kuutolea maelezo ulivyopatikana. Na kweli, tangu mwalimu alirushe kimondo hicho, si Lowassa wala familia yake walikuwa tayari kuelezea walivyochuma huo utajiri!
Baada ya Lowassa kulazimishwa kuutema uwaziri mkuu, alijikuta akikabiliwa na pigo jingine takatifu. Pigo hili ni pale chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipomtuhumu kuwa gamba au mtuhumiwa mkuu wa ufisadi kiasi cha kumtaka aachie hata nyadhifa chache alizokuwa amebakia nazo. Lowassa hakukubali kutupwa nje ya uringo wa siasa hasa ikichukuliwa kuwa anatajwa tajwa kutaka eti kumrithi rais Jakaya Kikwete hapo 2015 jambo ambalo wanaojua alivyochafuka sana wanaona ni kama tusi na kejeli kwa taasisi ya urais na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Ili kufanikisha azma yake hii, Lowassa, bila kujali kuwa watu wana akili za kuhoji na kuchambua, amekuwa akimwaga pesa kwa njia ya michango ili kujiweka karibu na wapiga kura akiwaaminisha kuwa anaweza kuwafaa wakati nafasi ya kufanya hivyo aliishaipoteza kwa kuitumia vibaya na kuliacha taifa kwenye zahama ya kiza na kulanguliwa umeme.
Je haya mamilioni anayotoa Lowassa yanatokana na malipo ya marupurupu ya ustaafu anayopewa kinyume cha sheria? Maana, Lowassa hakuwahi kustaafu zaidi ya kulazimishwa kuachia ngazi. Wengi wanashangaa ni kwanini Lowassa anaendelea kutanua bila kufikishwa mahakamani. Pia wengi wanashangaa jinsi CCM inavyomgwaya kiasi cha kumtishiatishia bila kumchukulia hatua. Kuko wapi kutekeleza dhana ya kujivua gamba ambako kumekuwa kukiahirishwa baada ya Lowassa kutishia kumwaga mtama? Je Lowassa kwa kukikamata mateka chama chake na serikali yake anaweza vile vile kuwakamata mateka watanzania akaishia kuwa rais wao hata kama ataingia kwenye vitabu vya historia kuwa anaweza kuwa rais mwenye kuchafuka kuliko waliowahi kumtangulia? Je watanzania ni wa hovyo kiasi hiki? Je wanapopokea mamilioni yake wanategemea kumpa kura wakati ukifika au kuyatumia kama ushahidi kutaka aeleze aliko na alivyoyapata huku pia wakimlazimisha atoe maelezo kuhusu shutuma zake?
Wengi pia wangetaka kuwajua hao marafiki wa Lowassa wenye uchungu na taifa letu kiasi cha kumwaga mamilioni kama wameyapata kihalali au ni watu wa kuaminika au kutisha shaka. Lazima kujiridhisha isijekuwa wananchi na michango ya maendeleo vinatumika kusafishia pesa chafu itokayo kwa magenge ya watu wachafu. Hata hivyo, kwa wanaokumbuka adha alizowasababishia Lowassa kwa kubariki na kuingiza kampuni ya Richmond na hatimaye Dowans, hata awape nini hawawezi kumsamehe. Kwa wanaokumbuka ni mabilioni mangapi ya shilingi yaliteketezwa na mradi huu ambao waziri wa zamani wa Nishati na Madini Ibrahim Msabaha aliwahi kusema ni waziri mkuu yaani Lowassa na mhindi wake yaani Rostam Aziz, hawezi kupumbazwa na misaada ya mamilioni wakati wao walichuma mabilioni ukiachia mbali kuendelea kuchuma ya ustaafu wakati Lowassa hakustaafu.
Kama michango yote ambayo Lowassa ameishaitoa ingefanyiwa mahesabu, ni pesa nyingi kuliko hata mishahara yake yote ya utumishi wake serikalini. Kwa mfano mifano miwili hapo juu ya michango ya Lowassa ya shilingi 120,000,000 ni zaidi ya mshahara wa mbunge wa mwaka mzima. Hapa hajala wala kulisha familia yake kuvaa na kufanya mambo mengine. Kama Lowassa akifanyiwa ukaguzi wa kimahasibu tangu aanze kazi na marupurupu yake yote vikalinganishwa na misaada aliyowahi kutoa na mali anazomiliki itagundulika kuwa maneno ya baba wa taifa yalikuwa ya kweli. Na hivyo, yasipuuzwe wala kusahauliwa hasa wakati huu ambapo nchi inahitaji uongozi adilifu na mpya.
Tumalizie kwa kumtaka Lowassa awataje hao marafiki zake na jinsi walivyopata hayo mamilioni. Lazima tujue kama wanafanya biashara au kazi halali, wakilipa kodi na kama ni watumishi wa umma akiwamo naye na Lowassa, je wametaja mali zao kama wanavyotakiwa na sheria? Kujua ukweli kuhusu jinsi wanavyopata pesa hii wanayotoa kwa jina jema la kusaidia jamii ni jambo jema. Lazima kila kitu kieleweke ili kuepuka jamii kugeuzwa kama fisi kulishwa nyama yake nayo ikaifakamia kwa uchoyo. Ni wakati muafaka kuangalia nani anatoa kuliko kuangalia nini kimetolewa. Hapa tuepuke cha baniani mbaya kiatu chake dawa.
Chanzo: Dira Februari, 2012.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.