Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 18, 2012

Dk Slaa: Sina mpango wa kuwania Ubunge ArumeruFriday, 17 February 2012 21:18

Mussa Juma, Arusha na Boniface Meena
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema hana mpango wa kugombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki.Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikaririwa akisema kama Dk Slaa ataamua kuwania ubunge katika jimbo hilo, chama kitaheshimu uamuzi wake akisema: “Katika suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la msingi... kama Dk Slaa ataamua kugombea ubunge Arumeru Mashariki, tutaheshimu uamuzi wake.”

Mbowe alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi ikiwemo Igunga na chama hakikuwahi kumlazimisha kwani jambo la kwanza ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka kuwania kiti hicho.“Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga lakini hakwenda. Hii ni kwa sababu anakubalika karibu kote nchini, hivyo kama atakuwa na utashi binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama zitatumika tu kufikia uamuzi,” alifafanua.

Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Mlimani jana, Dk Slaa alisema hafikirii kuwania ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa kuwa kazi yake ni kukijenga chama kitaifa ili kiweze kupata wabunge wengi.

Alisema hawezi kujifunga kwenye jimbo moja wakati alishasema kuwa kazi yake ni kutetea wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa kukijenga chama chake.“Siwezi kujifungia kwenye jimbo moja, nilishasema kazi yangu ni kukijenga chama ili kiweze kupata wabunge wengi,” alisema Dk Slaa.

Wakati Dk Slaa akitoa msimamo wake huo, baadhi ya makada waliokwishajitokeza na kuonyesha nia ya kugombea jimbo hilo wamesema kama ataamua wako tayari kumpisha.

Mmoja wa makada hao ni aliyepeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010 jimboni humo, Joshua Nasari ambaye alitoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, marehemu Jeremiah Sumari.

Tangu juzi kumekuwa na mjadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge Arumeru Mashariki kuziba pengo la marehemu Sumari lakini, wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga.

Joshua Nasari

Kwa upande wake, Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura alioupata katika uchaguzi wa mwaka 2010, alisema yupo tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk Slaa kuwania ubunge katika jimbo hilo kama akihitaji.

Nasari ambaye amerejea hivi karibuni mjini Arusha akitokea Marekani, leo anatarajiwa kuchukua fomu rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema.“Nimesikia maoni kupitia mitandao na wadau wakimuomba Dk Slaa kugombea, hili ni jambo jema kwetu kwani wananchi wanajua jimbo hili tunashinda Chadema na kama Dk (Slaa) akitaka kugombea demokrasia ya chama chetu itafanya kazi, kwani kikubwa tunataka ushindi,” alisema Nasari.

CCM walalamika
Baadhi ya wanachama wa CCM, wamelalamikia gharama kubwa za fomu za chama hicho zinazotolewa kwa makada wake wanaotaka kuwania ubunge katika jimbo hilo.Wanachama Julias Nangisa na Lameck Kanangira walisema jana kwamba gharama ya Sh300,000 wanayotakiwa kulipa ni kubwa mno kwa mwanachama wa masikini wa CCM.

“Gharama hizi kubwa zinaonyesha kama mtu huna kipato cha kutosha huwezi kuwa kiongozi ndani ya CCM kwani fomu tunatakiwa kulipa 100,000 na mchango wa chama 200,000 kabla ya kukabidhiwa fomu,” alisema Nangisa na kuungwa mkono na mwenzake.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.