Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, February 18, 2012

Samuel Sitta Matatani

Festo Polea
WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ameingia matatani baada ya Jeshi la Polisi nchini kutolea tamko ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe na kueleza kuwa hautokani na kulishwa sumu, huku likisema limefungua jalada kwa ajili ya uchunguzi wa kauli yake hiyo.

Tamko hilo la polisi lililotolewa jana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. DCI Manumba aliwataka watu kuupuza madai hayo akieleza kuwa ushahidi uliopatikana kutoka nchini India alikolazwa Dk Mwakyembe hauonyeshi kuwa alilishwa sumu. Manumba alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake kuhusu hali na mwenendo wa uhalifu nchini katika kipindi cha mwaka jana.

Akifafanua kuhusu kauli hiyo ya Waziri Sitta, DCI Manumba alisema, "Jeshi la Polisi limekaa kimya muda mrefu likifanyia uchunguzi kauli hiyo kwa kuwa maneno hayo ndani yake yanaonyesha jinai." Aliendelea “Kazi ya Jeshi la Polisi ni kuchunguza makosa na si kufuatilia nani anaumwa ugonjwa gani. Nani anaumwa nini ni jukumu la madaktari. Lakini tumekuwa kimya muda mrefu tukichunguza tuhuma hizo nzito.’’ DCI Manumba aliendelea kufafanua “Ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India.

Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu katika maradhi yanayomsibu Mwakyembe.’’ Manumba aliongeza kuwa kwa kuwa suala hilo ni la kisheria na kiupelelezi, Jeshi la Polisi linaandaa jalada la upelelezi kuhusu kauli hiyo ya Waziri Sitta na likikamilika, litapelekwa kwa DPP kwa ajili ya uamuzi.

“Hata hivyo, Sitta mwenyewe nilimsikia katika kauli yake akisema kuwa naye ameisikia katika vyombo vya dola, hivyo tunaandaa jalada la upelelezi na likikamilika litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa uamuazi wa kisheria wa nani ashtakiwe au nani ana makosa. Lakini sasa ni hayo kuhusu kauli hiyo Waziri Sitta ninayoweza kusema,’’ alisema Manumba.

Awali Manumba alisema kabla Dk Mwakyembe hajaanza kuumwa na kukimbizwa India kwa matibabu, Jeshi la Polisi lilipokea maandishi kutoka kwa waziri huyo yaliyodai kuwa alikuwa akitishiwa uhai wake, lakini likiwa katika hatua za mwisho kukamilisha upelelezi wake, akaanza kuugua na kukimbizwa India kwa matibabu.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.