Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, February 22, 2012

Zitto: Umeme wa dharura ni ufisadi

ASEMA SH 1.7 TRILIONI ZINAZOTUMIKA KWA MWAKA ZINATOSHA KUTANDAZA BOMBA LA GESI NA KUMALIZA KABISA TATIZO
Boniface Meena, Muheza
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema miradi ya umeme wa dharura inayoigharimu Serikali Sh1.7 trilioni kwa mwaka ni kichaka cha ufisadi.
Akizungumza na wakazi wa Muheza katika mkutano wa hadhara juzi, Zitto alisema: “Umeme wa dharura unapendwa kwa kuwa ni eneo lililojaa ufisadi. Ni rahisi kufanya mikataba ya wizi katika eneo hilo. Si tumesikia wizi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL? Dola za Marekani 56 milioni zinadaiwa kupotea, Takukuru wanachunguza.”
Kauli hiyo ya Zitto imekuja wakati tayari Bunge limeidhinisha kiasi cha Sh1.6 trilioni kwa Serikali kwa ajili ya mpango wa dharura wa kutatua tatizo la mgawo wa umeme kuanzia Agosti mwaka jana hadi Desemba mwaka huu.
“Nilimwandikia Spika mwaka jana kumuomba aiambie kamati ya Makamba (Januari) (ya Nishati na Madini) kuchunguza ufisadi katika ununuzi wa mafuta ya IPTL lakini, mwaka unapita hakuna hatua iliyochukuliwa. Nimemkumbusha tena Spika katika mkutano uliopita lakini hajajibu. Mimi sitachoka, nitaendelea kumbughudhi Spika hadi ufisadi huo ufichuliwe.”
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alipotafutwa jana kuthibitisha kama amepata barua ya Zitto iliyomwomba achunguze wizi kwenye baadhi ya miradi hiyo hakupatikana kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila ya kupokewa.

Alisema hakuna sababu nyingine ya miradi hiyo zaidi ya mwendelezo wa ufisadi. Alisema fedha hizo zingetosha kama zingetumika kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ili kuondoa kabisa tatizo la umeme badala ya kutegemea umeme wa dharura.

“Pia sehemu ya fedha hizo zingeweza kutumika katika ujenzi wa bomba jingine la gesi kutoka Kiwira hadi Dar es Salaam ambalo kwa pamoja, umeme huo ungeingizwa kwenye gridi ya taifa na kumaliza kabisa tatizo hilo.”

Alisema Serikali imewagawa Watanzania katika matabaka kwani umeme ukikatika Dar es Salaam na watu wakapiga kelele, inatikisika na kushughulikia matatizo yao haraka, lakini vijijini hata watu wakipiga kelele vipi, hawasikilizwi.

Serikali imeamua kukalia ripoti inayothibitisha namna ufisadi unavyoliangamiza taifa: “Serikali inatakiwa kutoa ripoti hiyo ili wananchi wajue nchi yao inakoelekea na waweze kuchukua hatua haraka kuinusuru.”
Zitto alisema ni lazima wananchi wasimame kidete ili kulinda maslahi yao dhidi ya mafisadi kwa kuwa Serikali imeshindwa kufanya hivyo na kuwasababishia wananchi umasikini wa kutupwa.
Katika mkutano huo, Zitto alisema maisha ya wananchi wa Tanzania yako hatarini kwa kuwa wale ambao ni masikini wanaotegemea kilimo wamekata tamaa kwa kukosa msaada katika sekta hiyo.

“Kila siku mnaambiwa kilimo kimekua kwa asilimia nne, mbona haibadiliki na nyie hamshangai? Ni lazima muwe mnahoji hao wanaofaidika na kilimo ni kina nani hasa kama siyo mafisadi? Umaskini tulio nao nasisitiza wao ndiyo chanzo,” alisema Zitto.

Januari Makamba
Makamba alipoulizwa kuhusu madai ya Zitto kumwandikia barua Spika alisema amepata nakala lakini kamati yake haijapewa maelekezo rasmi kuchunguza suala hilo.
Alisema suala la ununuzi wa mafuta ya umeme linatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kibunge kwa kuwa haliko wazi katika mchakato wake.
“Tatizo ni kwamba zoezi zima haliko wazi, mimi naunga mkono kuwa uchunguzi wa kibunge ufanyike na ieleweke wazi masuala ya ugavi na nani amepataje zabuni,” alisema Makamba.
Kwa upande wa gharama za kukodi mitambo ya dharura, alisema hawezi kushangazwa na matumizi ya kiasi hicho lakini akasema hana uhakika na kiasi cha fedha kwani mchakato umekuwa kwa zaidi ya miezi sita tokea Agosti 8, mwaka jana.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.