yanayoikabili nchi, hasa ukosefu wa ajira na ufisadi hayatapatiwa ufumbuzi,
unaoenda sambamba na kuwapatia matumaini wananchi wanyonge, kuna hatari ya
mstakabali wa amani ya nchi kuwekwa rehani.
Chama hicho kimesema kuwa matatizo hayo mawili ambayo yamechangia kwa kiasi
kikubwa kuwakosesha wananchi matumaini, kama inavyodhihirika miongoni mwa
watu wengi kwa sasa, yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka, ili kunusuru
nchi, kwani ni hatari kwa watawala kuongoza wananchi waliokata tamaa.
Ili kuziba ombwe la uongozi, kwa viongozi kutowasemea wananchi wanyonge,
hasa wale wa vijijini, chama hicho kimesema kuwa kimejitolea kuifanya kazi
hiyo katika majukwaa mbalimbali, ikiwemo mikutano ya hadhara, bungeni na
kokote kule, ambako kitaweza kupaza sauti kuonesha uongozi mbadala namna
ambavyo nchi inapaswa kuongozwa, kikijikita kutoa suluhisho ya matatizo
hayo.
Akihutubia mikutano ya hadhara katika Wilaya ya Mheza, akiwa kwenye ziara
ya kukagua uhai wa chama mkoani Tanga, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara,
Zitto Kabwe amesema kuwa hali ya wananchi kukosa matumaini kwa watawala wao
ni moja ya dalili mbaya kwa utawala wowote ule na tishio kubwa la amani ya
nchi.
“Wananchi mmepoteza matumaini, mmekata tamaa, hamuwaamini tena watawala
walioko madarakani, mmepoteza matumaini na CCM. Kwa mambo mliyofanyiwa
miaka nenda rudi na chama hicho, hamtuamini tena wanasiasa, kila anayekuja
mnamuona ni yule yule. Kila mkitusikiliza mnatusikia tunazozana kuhusu
posho, tunagombania maslahi yetu, badala ya kuwasemea ninyi wanyonge wenye
nchi.
“Kati ya mambo ambayo yataipasua nchi hii ni suala la ukosefu wa ajira kwa
vijana upande mmoja na ufisadi, rushwa na ubadhirifu upande mwingine.
Takriban miaka mitano sasa, mnasoma katika magazeti na kusiki, fulani
kapiga pale, fulani kapiga hapa, mkurugenzi yule wa halmashauri kaiba pale,
mkurugenzi huyu wa shirika la umma kaiba hapa, mwanasiasa yule kafisadi
hapa, mnazidi kukosa matumaini.
“Tunawafundisha vibaya watoto wetu hawa. Wataamini kuwa ukitaka kuishi
katika nchi hii ni lazima uwe fisadi, kitu ambacho sikweli. Watawala sasa
wanafikiria kula tu, wanafikiria maslahi yao, hawasemei tena wananchi
maskini, hasa walioko vijijini. Tangu alipofariki Mwalimu Nyerere,
aliyekuwa watetezi wa wanyonge, wananchi wa vijijini wamekosa msemaji
kabisa,” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alitolea mfano wa namna
wananchi wa vijijini walivyotelekezwa, akisema kuwa kila inapotokea umeme
umekatika maeneo ya miji mikubwa, nchi husemwa ‘iko gizani’, bila kujali
kuwa kuna wananchi tangu Tanzania ipate uhuru ‘wako gizani’ miaka yote,
lakini athari za kukosekana kwa nishati hiyo ikiendelea kuwaathiri.
“Leo nilikuwa Zirai huko vijijini ndani kabisa, wananchi wana utajiri wa
mazao yao, wanalima Irki, wanalima karafuu, wanalima mdalasini, wanalima
mazao mengi ambayo yangewafanya kuwa matajiri kama yangepata soko, kama
wangepata miundombinu ya barabara kuja huku, ili mazao hayo yasafirishwe,
lakini nani anawasemea watu hawa?” alisema Zitto.
Mbali ya kukagua uhai wa chama mkoani Tanga, Zitto pia anafanya ziara
mkoani Tanga, kwa ajili ya kuifafanua hoja yake juu ya zao la mkonge,
aliyoiwasilisha bungeni katika mkutano wa bunge uliopita, ambapo amewaambia
wananchi wa Mheza kuwa inashangaza kuona baadhi ya wabunge wa Tanga,
waliipinga hoja hiyo, kwa kujali maslahi ya CCM, badala ya kuangalia
manufaa kwa wananchi, hasa wakulima wadogo.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.