Musa Juma na Moses Mashalla, Arusha WAKATI Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akianza kugusa hisia za watu wanaomtaka agombee ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema iwapo mtendaji mkuu huyo wa chama ataamua kuwania kiti hicho, wataheshimu uamuzi wake. Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, aliyepeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010, Joshua Nasari na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, marehemu Jeremiah Sumari, naye amesema kama katibu mkuu wake ataamua kuwania kiti hicho, hatakuwa na pingamizi ikiwa chama kitaamua kwani lengo ni kutwaa jimbo hilo. Akizungumza na Mwananchi jana baada ya kuibuka mjadala kuhusu uwezekano wa Dk Slaa kuwania jimbo hilo, Mbowe alisema, "Katika suala la kugombea, utashi binafsi ni jambo la msingi...,kama Dk Slaa ataamua kugombea ubunge Arumeru Mashariki, tutaheshimu uamuzi wake." Mbowe alisema katika uteuzi wa chama, kuna vigezo vinavyoangaliwa ikiwa ni pamoja na jinsi mtu anavyokubalika kwa wananchi anakogombea, sifa zake na utashi wake binafsi na kuongeza, "Hatuna uteule katika chama." Hata hivyo, Mbowe alisema Chadema hakiwezi kumlazimisha Dk Slaa akagombee jimbo hilo kama mwenyewe utashi haumtumi kufanya hivyo, na kwamba hana shaka na kukubalika kwa katibu mkuu huyo kutokana na imani aliyojijengea kwa umma wa Watanzania. Mbowe alisema Dk Slaa amekuwa akiombwa kugombea ubunge katika maeneo mengi likiwamo Jimbo la Igunga, lakini chama kisingeweza kumlazimisha kwani jambo la kwanza ilibidi mwenyewe aonyeshe utashi binafsi wa kutaka kuwania kiti hicho. "Dk Slaa aliwahi kuombwa akagombee Igunga, lakini hakwenda. Hii ni kwasababu anakubalika nchini karibu kote, hivyo kama atakuwa na utashi binafsi kwanza, nadhani taratibu za chama zitatumika tu kufikia uamuzi," alifafanua. Mwenyekiti huyo wa Chadema pia alitoa angalizo kwamba, wakati mwingine uamuzi wa chama kupata mgombea unaangalia jinsi mgombea alivyo na mtandao katika jimbo analotaka kugombea ili hata kama akichaguliwa aonekane ni mbunge wa eneo hilo. "Ndiyo maana nasema kuna vigezo vingi tu, kwa mfano mtu anaweza kuwa mbunge mzuri bungeni, lakini je, ana connectivity (kinachomuunganisha) jimboni, kuangalia kama ana makazi na mtandao mwingine kwani asije akawa mbunge mzuri bungeni, lakini jimboni akiwa kama mgeni hivyo watu wakaona kama kimewapelekea pandikizi tu,"alifafanua Mbowe. Tangu juzi kumekuwa na mjadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi wakimtaka Dk Slaa akagombee ubunge Arumeru Mashariki kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehebu Sumari, lakini wengine wanapinga na kumtaka aendelee kubaki na nafasi yake ya katibu mkuu wa chama kwa lengo la kukijenga. Hata hivyo, Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alishika nafasi ya pili akiwa nyuma ya Rais ya Jakaya Kikwete, juzi alinukuliwa na gazeti moja la kila siku (siyo Mwananchi) akisema, "Siwezi kulizungumzia jambo hilo, maana nilikwisha kusema muda mrefu kuwa sitaki tena ubunge na isitoshe mimi si mwenyeji wa Arumeru," Joshua Nasari Kwa upande wake Nasari (26) ambaye ana mtaji mkubwa wa kura kufuatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 alitoa msimamo wake akisema yupo tayari kufanya mazungumzo na viongozi wa juu ya chama chake juu ya kumpisha Dk Slaa kuwania ubunge katika jimbo hilo kama akihitaji. Nasari ambaye amerejea hivi karibuni mjini Arusha akitokea nchini Marekani, leo anatarajiwa kuchukua fomu rasmi ili kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema. "Nimesikia maoni kupitia mitandao na wadau wakimuomba Dk Slaa kugombea, hili ni jambo jema kwetu kwani wananchi wanajua jimbo hili tunashinda Chadema na kama Dk (Slaa) akitaka kugombea dekomrasia ya chama chetu itafanya kazi, kwani kikubwa tunataka ushindi,"alisema Nasari. Nasari aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kati ya 2008 na 2009 alipohitimu shahada ya Sayansi ya Jamii katika masuala ya utengenezaji Sera na Utawala, alisema ana imani Chadema kitashinda Arumeru. "Nilikuwa Marekani kikazi na sasa nimerejea kama ulivyoshuhudia watu wengi wananiunga mkono na tayari wamenichangia Sh 11milioni za kampeni na magari manane," alisema Nasari. Mgombea huyo ambaye tayari ametangaza kuacha kazi katika shirika la Kimarekani la Foundation For Tomorrow ili kujikita kwenye uchaguzi huo, alisema wakazi wa Arumeru Mashariki wanahitaji mwakilishi sahihi ambaye anaweza kuwatetea katika kuinua uchumi wao. Hata hivyo, alisema tayari amepata taarifa za Dk Slaa kutoa tamko kuwa hawezi kushiriki katika uchaguzi huo, kwa kuzingatia kuwa sio mkazi wa Meru na pia hana nia ya kugombea kiti hicho. "Nategemea Dk Slaa na viongozi wengine wa kitaifa, wakiwapo wabunge, marafiki zangu wa vyuo vikuu na wengine wengi tutakuwa nao Arumeru kuhakikisha Chadema inashinda,"alisema Nasari. Hadi kufikia jana, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Mkoa wa Arusha (Bavicha), Ephata Nanyaro, wanachama waliokuwa wamechukua fomu ni Yohane Kimuto, Samweli Chami na Rebecca Mwingisha na leo Nasari atakuwa mwanachama wa tatu. "Tunatarajia wanachadema wengi zaidi watajitokeza katika siku hizi zilizobaki ili kuchukuwa fomu na kurejesha mapema,"alisema Nanyaro. Mgombea CCM alalamikia rushwa Katika hatua nyingine, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM katika Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Elirehema Kaaya ambaye pia ni afisa wa mifugo mkoani Mwanza, amekitaka chama hicho kukemea kampeni za fedha ndani ya chama katika uchaguzi huo. Kaaya ambaye pia aligombea jimbo hilo katika uchaguzi uliopita na kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM, alisema wakazi wa Arumeru hawahitaji mgombea wa CCM ambaye anapata nafasi hiyo kwa kutumia fedha. "Arumeru wanataka mtu wa kuwasemea matatizo yao mjengoni (bungeni) na sio mtu anayetumia fedha kupata ubunge na mimi naomba chama kikemee na kukomesha matumizi ya fedha,"alisema Kaaya. Akizungumzia maombi hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru Edson Lihweuli alionya mgombea yoyote ambaye atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au kukiuka taratibu atachukuliwa hatua. Lihweuli alisema wagombea wote ambao wamechukua fomu, wamekuwa wakipewa taratibu hizo ili kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama hicho unakwenda vizuri. Wakati huohuo, Mkuu wa shule ya Sekondari ya Leguruki inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Mwalimu Athony Msami jana alijitokeza kuchukua fomu na kufanya wagombea wa chama hicho wanaomba ridhaa ya chama kufikia sita.Wengine waliokuwa wamechukuwa fomu ni Sioi Sumari, mtoto wa aliyekuwa mbunge Jeremiah Sumari, William Ndeoya Sarakikya, Elipokea Urio, Elishiria Kaaya na Elirehema Kaaya. Wakati kada huyo wa CCM akichukua fomu, juzi jioni Mkurugenzi wa kituo cha Mikutano cha Arusha(AICC), Elishiria Kaaya alirejesha fomu na kueleza kuwa anagombea ili kutekeleza ilani kwa kushughulikia matatizo ya wananchi wa Meru. Kaaya ambaye pia aligombea uchaguzi uliopita na kuangushwa katika kura za maoni na Marehemu Sumari, alisema miongoni mwa mambo ambayo atayasimamia ni kuhakikisha anashirikiana na wananchi kukabiliana na matatizo ya upatikanaji maji, barabara, huduma za afya na masuala ya elimu. Takukuru yaanza kazi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha imekutana na wagombea waliojitokeza kuchukua fomu katika uchaguzi huo na kuwaonya kutojihusisha na rushwa pia kuwataka waheshimu sheria za gharama za uchaguzi. Takukuru pia imetamka kwamba tayari imeshashaanza kupokea malalamiko mbalimbali ya makada wa vyama tofauti vya siasa wilayani humo, kujihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na kwamba madai hayo yameanza kufanyiwa kazi. Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto imesema katika kujipanga kukabiliana na rushwa katika uchaguzi huo taasisi hiyo imekutana na wagombea wote wa vyama hivyo kwa lengo la kuwatahadharisha. “Katika kujipanga na uchaguzi wa Arumeru kwanza tumewaita wagombea ambao wameshajitokeza hadi sasa pamoja na viongozi wa vyama vyao, lengo ni kuwatahadharisha na kuwataka waheshimu sheria ya uchaguzi,”alisema Kasumambuto | ALIYEPEPERUSHA BENDERA CHADEMA 2010 AREJEA KUTOKA MAREKANI, AUNGA MKONO. |
Jisikie huru kabisa kuchangia lolote linalohusiana na jamii, uchumi, siasa, imani na elimu katika Blog yetu. Tunakaribisha habari, taarifa, picha za matukio, maoni na ushauri ili kuwekana sawa katika dunia yetu hii ndogo. Wote mnakaribishwa katika kuimarisha mshikamano wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini mwetu!!
Pages
Forums
- Critical Analysis (11)
- Education Issues (15)
- Geology and Mining (21)
- International News (37)
- National News (147)
- Political Issues (67)
- Religious Issues (28)
- Social Issues (79)
- Sports (19)
Friday, February 17, 2012
Mbowe: Dk Slaa ruksa kugombea Arumeru
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.