Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, February 17, 2012

MAKAMU WA RAIS DK GHARIB BILAL KUANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUKWA KESHO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohammed Gharib Billal atafanya ziara ya siku 7 Mkoani Rukwa ambapo itajumuisha Mkoa mpya wa Katavi. Ziara yake hiyo itaanza tarehe 18 na kumalizika tarehe 24 Februari 2012 ambapo atawasili tarehe 17 akitokea Mkoani Ruvuma.
Awapo Mkoani Rukwa atatembelea Wilaya zote tatu za Mpanda, Nkasi na Sumbawanga. Mpanda atakuwepo kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 20 ambapo atapokea taarifa ya Serikali pamoja na Chama cha Mapinduzi. Aidha atafanya mkutano wa ndani katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Mpanda na mikutano wa nje katika uwanja wa Kashaulili na Ofisi ya Tarafa Inyonga.
Pamoja na hayo atapata fursa ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya Tarafa ya Inyonga na Ghala la Mkutano wa Hadhara katika kijiji cha Mwamapuli. Atatembelea pia mbuga ya wanyama ya Katavi kabla ya kuondoka kuelekea Wilaya ya Nkasi.
Akiwa wilayani Nkasi kuanzia tarehe 20 Februari 2012 Makamu wa Rais atapokea taarifa ya ujenzi wa barabara za Mkoa wa Rukwa na taarifa ya Wilaya ya Nkasi. Atafungua miradi ya maendeleo ikiwepo nyumba ya watumishi wa Halmashauri, Jengo la Utawala Shule ya Sekondari Nkomolo, na Daharia Shule ya Sekondari Korongwe. Atafanya pia Mkutano wa hadhara katika kiwanja cha shule ya Sekondari Korogwe.
Akimaliza ufunguzi wa miradi hiyo, ziara yake itahamia katika Wilaya ya Sumbawanga ambapo atamalizia ziara yake na kuelekea Mbeya kwa ajili kuendelea na zoezi kama hilo ambalo linatemewa kufanyika katika nchi nzima.
Mhe. Makamu wa Rais atawasili Sumbawanga tarehe 22 Februari 2012 akitokea Nkasi ambapo atapokelewa na viongozi wa chama na serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya. Baada ya kupokelewa atapewa taarifa fupi ya Chama na Serikali.
Awapo Sumbawanga atapata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo ataweka jiwe la Msingi Jengo la ofisi ya Mkaguzi Mkazi Mkoa wa Rukwa na Jengo la benki ya CRDB. Atazindua Maghala ya kuhifadhi bidhaa bandarini yaliyopo Kasanga, Soko Jipya la Samaki Kasanga, na kampeni ya usafi katika Mji wa Sumbawanga “SUMBAWANGA NG’ARA” kwa kugawa vitendea kazi vya usafi.
Atapata pia fursa ya kusalimiana na wananchi katika maeneo yote ya miradi atakayotembelea ambapo atatembelea pia ngome ya “FORT BISMARK” iliyopo Kasanga na Kiwanda cha nyama cha SAAFI kinachomilikiwa na Mbunge Msataafu na mjasiriamali Ndugu Chrissant Mzindakaya.
Makamu wa Rais pia atafanya Mikutano wa hadhara katika viwanja vya Rukwa High School na Uwanja wa Mpira wa Laela. Atazungumza na wazee maarufu wa Wilaya ya Sumbawanga katika uwanja wa Ikulu Ndogo ya Sumbawanga.
Mhe. Makamu wa Rais atakamilisha ziara yake tarehe 24/02/2012 na kuondoka Sumbawanga kuelekea Mkoa jirani wa Mbeya ambapo atakuwa na ratiba ya ziara ya kikazi Mkoani humo.
IMETOLEWA NA
HAMZA TEMBA
AFISA HABARI OFISI YA MKUU WA MKOA
RUKWA

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.