Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, February 10, 2012

Hotuba ya upinzani ya muswada wa Marekebisho ya sheria ya mabadiliko katiba Chadema yamkubali JK

MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SHERIA NA KATIBA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA
YA MABADILIKO YA KATIBA, SHERIA NA. 8 YA 2011

(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge lako tukufu lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Siku kumi na moja baadaye, yaani tarehe 29 Novemba, 2011, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha Muswada huo kuwa Sheria kwa mujibu wa ibara ya 97(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na kanuni ya 92(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007. Kwa mujibu wa kifungu chake cha 1(2), Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Na. 8 ya 2011, ilianza kutumika tarehe 1 Desemba, 2011, yaani siku mbili tu baada ya kupata kibali cha Rais.

Mheshimiwa Spika,

Leo ni siku arobaini na moja tangu Sheria hii ipate kibali cha Mheshimiwa Rais, na siku thelathini na tisa tangu ipate nguvu za kisheria ili ianze kutumika. Tumekutana hapa leo hii ili Bunge lako tukufu lipate fursa nyingine tena ya kuitafakari Sheria hii. Kila mmoja wetu humu ndani, na kila Mtanzania anayefuatilia mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya, anafahamu kwamba tendo la kwanza lililoidhinishwa na Sheria hii, yaani kuteuliwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, halijafanyika hadi sasa. Tumekutana hapa leo hii ili kujadili, na kama Bunge lako tukufu litaridhika, kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 unaopendekezwa na Serikali, na hivyo kumwezesha Mheshimiwa Rais kutenda tendo hilo la kwanza kwa mujibu wa Sheria hii.

MAJADILIANO YA CHADEMA NA RAIS

Mheshimiwa Spika,

Tarehe 20 Novemba, 2011 Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliunda Kamati Maalum ya wajumbe saba iliyopewa jukumu la kuonana na Mheshimiwa Rais kuhusu Sheria hii na mustakbali wa taifa letu. Siku mbili baadae, yaani tarehe 22 Novemba, 2011, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe alimwandikia Mheshimiwa Rais barua ya kumwomba kuonana na Kamati Maalum ya CHADEMA kwa siku na muda atakaoona yeye Mheshimiwa Rais unafaa.

Siku iliyofuata, yaani tarehe 23 Novemba, Mheshimiwa Rais alijibu maombi ya Mheshimiwa Mbowe kwamba alikuwa tayari kukutana na Kamati Maalum tarehe 27 Novemba, 2011. Kamati Maalum ilikutana na Mheshimiwa Rais na washauri wake Ikulu, Dar es Salaam kwa zaidi ya masaa matatu siku hiyo, na kwa karibu masaa nane siku iliyofuata, yaani tarehe 28 Novemba, 2011. Mheshimiwa Rais na washauri wake walikutana kwa mara nyingine tena na Kamati Maalum siku ya tarehe 20 Januari, 2012 wakati taifa linaomboleza kifo cha Mbunge mwenzetu Marehemu Jeremiah Solomon Sumari. Mara hii majadiliano hayo yalichukua zaidi ya masaa sita na yalikwisha majira ya saa sita usiku!

MUAFAKA NA WADAU WENGINE

Mheshimiwa Spika,

Mheshimiwa Rais hakukutana na uongozi wa CHADEMA peke yake. Baada ya mkutano wake na Kamati Maalum ya CHADEMA, na kwa nyakati tofauti, Mheshimiwa Rais alikutana pia na wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi, viongozi wa taasisi kuu za kidini nchini na wawakilishi wa mashirika na asasi zisizokuwa za kiserikali. Aidha, kama alivyoeleza yeye mwenyewe wakati akihutubia wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kilele cha kuadhimisha miaka thelathini na tano ya kuzaliwa kwa CCM, Mheshimiwa Rais alikutana pia na uongozi wa CCM ambapo alipokea mapendekezo nane ya marekebisho ya Sheria. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba Muswada huu, na Jedwali la Marekebisho lililoambatanishwa nao, umefaidika kwa busara za Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe pamoja na mawazo na mapendekezo ya wadau wengine wote ambao nimewataja hapa. Kwa maana nyingine, Mheshimiwa Spika, Muswada huu hautokanani na njama za vikao vya siri kati ya Mheshimiwa Rais na CHADEMA! Ni Muswada unaotokana na muafaka katika ya Mheshimiwa Rais na Serikali yake na makundi mbali mbali katika nchi yetu yanayowakilisha maslahi ya kisiasa, ya kijamii na hata ya kidini. Ni Muswada unaoonyesha uso halisi wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika,

Nimeelezea historia hii kwa kirefu ili Bunge lako tukufu lipate ufahamu wa background ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulioko mbele ya Bunge hili tukufu. Hii sio tu itawasaidia Waheshimiwa Wabunge kupata ufahamu wa mambo yaliyojiri tangu Sheria hii ilipopitishwa mwaka jana, bali pia inaonyesha umuhimu wa Sheria hii na mapendekezo ya marekebisho yaliyoletwa Bungeni na Serikali. Wote tunajua jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais – kama Rais Mtendaji mwingine yeyote - ni mtu mwenye kazi na majukumu mengi kama Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu.

Kwa sababu ya kazi na majukumu mengi aliyo nayo, Mheshimiwa Rais hana muda wa kupoteza wala wa kustarehe. Kwa maana hiyo, Rais anapoacha shughuli zake nyingi nyingine za kitaifa ili kuzungumza na watu ambao wala hawajibiki kisheria kukutana au kuzungumza nao kwa jambo lolote lile; Rais anapotumia siku nne na masaa karibu ya ishirini kuzungumza nao juu ya jambo moja; Rais anapokubali kukaa hadi saa sita za usiku kujadiliana nao juu ya jambo hilo; na Rais anapokubali kuacha shughuli zake nyingi nyingine ili kukutana na viongozi wa vyama vingine vya siasa, viongozi wa kidini na wawakilishi wa taasisi za kiraia kujadiliana nao juu ya jambo hilo hilo, yote hayo yanadhihirisha umuhimu kwa taifa wa jambo hilo!

Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, tumekutana hapa leo kutafakari Sheria hii kwa sababu Mheshimiwa Rais mwenyewe – kwa muda mkubwa alioutumia kukutana na kujadiliana nasi pamoja na wadau wengine - ameonyesha dhahiri kwamba Bunge hili tukufu linahitaji kuitafakari upya Sheria hii muhimu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba busara zetu na ufahamu wetu wa umuhimu wa Sheria hii kwa mustakbala wa baadae wa nchi yetu na uzalendo wetu kwa taifa letu – na kwa kutambua kazi kubwa, mchango na maelekezo ya Mheshimiwa Rais - vitatuongoza katika kuyajadili na ya kuyapitisha mapendekezo ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011, ili kumwezesha Mheshimiwa Rais kuunda Tume itakayoanzisha rasmi mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Naomba nizungumzie jambo lingine la mwisho kabla sijafanya uchambuzi wa Muswada wenyewe na Jedwali la Marekebisho lililoambatanishwa nao. Ni kweli, kama nilivyosema awali, kwamba Muswada huu unaletwa Bungeni kabla hata ya miezi miwili kupita tangu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipopitishwa na Bunge lako tukufu na kupatiwa kibali cha kuanza kutumika na Mheshimiwa Rais. Ni kweli, kama nilivyosema mwanzoni, kwamba Muswada huu unakuja Bungeni kabla tendo la kwanza lililoidhinishwa na Sheria yenyewe halijafanyika. Ni kweli, kwa vyovyote vile, kwamba hiki ni kipindi kifupi sana kwa Sheria kufanyiwa marekebisho. Kwa sababu hizi, Mheshimiwa Spika, wapo watakaohoji – na wana haki ya kufanya hivyo – sababu au uhalali wa mapendekezo ya marekebisho haya katika kipindi hiki. Aidha, wapo watakaodhani kwamba mapendekezo haya ni ishara ya dharau kwa Bunge hili tukufu.

Kwa watu hao, Mheshimiwa Spika, nitasema yafuatayo. Kwanza, Katiba yetu haina na haijawahi kuweka muda au ratiba ya kufanya marekebisho ya Sheria yoyote ile. Badala yake, kifungu cha 24 cha Sheria ya Tafsiri za Sheria (The Interpretation of Laws Act), Sura ya 1 ya Sheria za Tanzania, kimeweka wazi kwamba “Sheria inaweza kurekebishwa au kufutwa kabisa katika Mkutano wa Bunge ule ule uliopitisha.” Kwa maana hiyo, mapendekezo ya marekebisho haya yangeweza kuletwa hata kabla Mkutano uliopita wa Bunge hili tukufu kumalizika na bado yangekuwa halali kisheria!

Mfano wa karibuni kabisa wa jambo ni Sheria ya Gharama za Uchaguzi, 2010 iliyopitishwa katika Mkutano wa Thelathini na Nane wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano mwezi Februari, 2010. Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho katika Mkutano wa Thelathini na Tisa uliofanyika Aprili 2010, na mara mbili katika Mkutano wa Arobaini wa Bunge la Bajeti la mwaka huo. Aidha, Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, 2001 iliyopitishwa tarehe 28 Machi, 2001 na kufanyiwa marekebisho katika Mkutano wa Bajeti uliofuatia tarehe 9 Agosti, 2001! Kwa maana hiyo, hii sio – na haitakuwa – mara ya kwanza kwa Bunge lako tukufu kufanya marekebisho ya Sheria iliyotungwa katika Mkutano uliopita.

Mheshimiwa Spika,
Sababu ya pili inatokana na umuhimu wa Sheria inayofanyiwa marekebisho pamoja na umuhimu wa marekebisho yenyewe. Katika hili, Mheshimiwa Spika, ni vema nikanukuu sehemu ya waraka tuliomkabidhi Mheshimiwa Rais siku ya tarehe 27 Novemba, 2011: “Sheria hii ni ... muhimu kuliko pengine sheria nyingine yoyote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama uliowekwa katika Sheria hii.”

Na kama nilivyosema wakati nawasilisha Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Mkutano uliopita: “Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka.” Muswada huu ni sehemu ya jitihada hizo za kuhakikisha tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka.

MUSWADA NA JEDWALI LA MAREKEBISHO LA SERIKALI

Mheshimiwa Spika,

Muswada huu ulichapishwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 23 Desemba 2011, wakati majadiliano kati ya Mheshimiwa Rais na Kamati Maalum ya CHADEMA na wadau wengine yakiwa hayajakamilika. Kama ulivyo sasa, Muswada huu una mapendekezo ya marekebisho ya vifungu viwili tu, yaani kifungu cha 6 na 18, vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, Jedwali la Marekebisho lililoandaliwa na Serikali na kuwasilishwa Bungeni sambamba na Muswada linapendekeza marekebisho katika vifungu vingine vya Sheria hii. Hii ni kwa sababu ilibidi Muswada uchapishwe kwenye Gazeti hata kabla mazungumzo kati ya Mheshimiwa Rais na wadau hayajakamilika ili kutimiza masharti ya kanuni ya 80(2) ya Kanuni za Bunge inayotaka Muswada kuwasilishwa kwa Katibu wa Bunge siku ishirini na moja kabla ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza Bungeni.

Mheshimiwa Spika,

Ni vema na ni haki kuweka kwenye kumbukumbu za Bunge lako tukufu kwamba Jedwali la Marekebisho la Serikali ni matokeo ya ushiriki wa moja kwa moja wa Mheshimiwa Rais na washauri wake Mheshimiwa Lukuvi, Mwanasheria Mkuu Werema, Mwandishi Mkuu wa Sheria Casimir Kyuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahuasiano na Uratibu) Mheshimiwa Stephen M. Wassira na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Emmanuel J. Nchimbi. Aidha, kwa upande wa CHADEMA ni vema na ni haki kutambua kwenye kumbukumbu za Bunge lako tukufu ushiriki na kazi kubwa iliyofanywa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Mbowe, Katibu Mkuu Dkt. Wilbrod P. Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara) na Mbunge wa Mpanda Mjini Mheshimiwa Said Amour Arfi, Mheshimiwa John J. Mnyika, Mbunge wa Ubungo na wajumbe wengine wa Kamati Maalum ya Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari na Mkurugenzi wa Utafiti, Bunge na Halmashauri katika Makao Makuu ya CHADEMA John Mrema.

Mheshimiwa Spika,

Sasa naomba, kwa ruhusa yako, niwasilishe uchambuzi wa Muswada wenyewe pamoja na Jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Serikali, nikianzia na mapendekezo ya marekebisho ya vifungu mbali mbali vinavyohusiana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

Mheshimiwa Spika,

Ibara ya 2 ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 6(5)(a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kufuta maneno “au kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi yoyote.” Jedwali la Marekebisho la Serikali lililowasilishwa sambamba na Muswada linapendekeza marekebisho sio tu ya ya kifungu cha 6(5)(a), bali pia kinapendekeza kuongezwa masharti ya ziada katika kifungu cha 6 cha Sheria. Kwanza, inapendekezwa kwamba maneno “, diwani au kiongozi wa chama cha siasa katika ngazi zote” yafutwe na badala yake yabaki maneno “Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.”

Mheshimiwa Spika,

Ili kuelewa maana ya marekebisho yanayopendekezwa, ni muhimu kurejea katika kifungu cha 6(5) kinachopendekezwa kurekebishwa na Muswada huu. Kifungu hiki kinaweka masharti ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwaondolea sifa za kuteuliwa Wabunge, Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote. Kwa mapendekezo ya Muswada huu na Jedwali la Marekebisho la Serikali, watu pekee ambao sasa hawatakuwa na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ni Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar. Kwa maneno mengine, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote watakuwa na sifa za kuteuliwa ili mradi tu wanazo sifa za kitaaluma na nyinginezo zilizotajwa katika kifungu cha 6(3) cha Sheria.

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa kupitishwa kwa Sheria hii tarehe 15 Novemba mwaka jana, tuliliambia Bunge lako tukufu kwamba, kwa kukataza viongozi wa vyama vya siasa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume, kifungu cha 6(5)(a) “... k(i)naondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii. Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya.” Pendekezo letu kwamba Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar nao wawe na sifa za kuteuliwa wajumbe wa Tume halipo katika mapendekezo ya Muswada huu na Jedwali la Marekebisho la Serikali. Hata hivyo – katika kuendeleza moyo wa maridhiano na give and take - Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaridhika na kuunga mkono mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 6(5)(a) ili kuwapa madiwani na viongozi wa vyama vya siasa sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.

Mheshimiwa Spika,

Kuna mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 6(5)(c) ambayo hayapo katika Muswada lakini yameletwa kwa njia ya Jedwali la Marekebisho la Serikali. Kifungu cha 6(5)(c) cha Sheria ya sasa kinawaondolea sifa za kuteuliwa watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa, au ni watuhumiwa katika mashauri ya jinai yaliyopo mahakamani yanayohusu mashitaka ya kukosa uaminifu au uadilifu. Jedwali la Marekebisho linapendekeza, na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaunga mkono, kukifuta kabisa kifungu hicho kwa sababu zifuatazo. Kwanza, tayari kifungu cha 6(4) cha Sheria ya sasa kimewaondolea sifa za kuteuliwa kama wajumbe watu wasiokuwa “... [wa]aminifu wa hali ya juu na [w]ana tabia i[na]yotiliwa shaka na jamii.” Mtu aliyewahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa la kukosa uaminifu au uadilifu anakuwa automatically disqualified na kifungu hicho na kwa hiyo hakukuwa na sababu yoyote kisheria ya kuwa na kifungu cha 6(5)(c). Pili, mapendekezo ya marekebisho ya kifungu hiki yanaenda sambamba na presumption of innocence iliyoko kwenye ibara ya 13(6)(b) ya Katiba yetu na kwa sababu hiyo yanahifadhi haki za watuhumiwa wa makosa ya jinai ya kupata ulinzi wa sheria hadi hapo watakapopatikana na hatia.

Mheshimiwa Spika,

Yapo mapendekezo mengine ya marekebisho ya kifungu cha 6 ambayo yameletwa kwa njia ya Jedwali la Marekebisho la Serikali. Kwanza inapendekezwa kuongezwa kifungu kipya cha 6(6) kinachosema kwamba “... Rais ataalika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe.” Pili, inapendekezwa katika kifungu kipya cha 6(7) kwamba “katika kualika jumuiya za kidini, asasi za kiraia, jumuiya, taasisi zisizo za kiserikali au makundi ya watu ... kuwasilisha orodha za majina ya watu ... kama ilivyoelekezwa kwenye kifungu kidogo cha (6), Rais atazingatia umoja unaosimamia jumuiya au asasi hizo.” Na tatu, kifungu kipya cha 6(8) kinapendekeza kwamba Rais asizuiliwe na masharti ya kifungu kipya cha 6(6) “... kuteua watu wengine kuwa wajumbe wa Tume.”

Mheshimiwa Spika,

Mapendekezo haya mapya ni ya kihistoria. Kwanza, tangu tupate uhuru miaka zaidi ya hamsini iliyopita na tangu Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32 ya Sheria za Tanzania ilipotungwa mwaka 1962, Tume zote ambazo zimeundwa kuchunguza mambo mbali mbali makubwa yaliyogeuza taswira ya kikatiba ya taifa letu zilikuwa Tume za Rais kwa maana kwamba Rais alikuwa ni alfa na omega wa Tume hizo. Rais ndiye alikuwa mteuzi wa Tume hizo, bila mashauriano na makubaliano na mtu mwingine yeyote. Rais ndiye aliyezipa Tume hizo hadidu za rejea na ndiye aliyepokea ripoti za Tume hizo. Rais ndiye aliyeamua kutoa hadharani ripoti za Tume au la na ndiye aliyeamua kipi akikubali na kipi akikatae katika mapendekezo ya ripoti za Tume hizo. Mifano ya Tume za aina hii ni Tume ya Kawawa iliyopelekea kuanzishwa kwa mfumo wa siasa wa chama kimoja na kupigwa marufuku kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1964/65; Tume ya Kombo na Msekwa iliyopelekea kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP na kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977; na Tume ya Nyalali iliyopelekea kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991/92. Zote hizi zilikuwa Tume za Rais par excellence!

Mheshimiwa Spika,

Pendekezo la kumwezesha Mheshimiwa Rais kualika vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha majina ya watu watakaoteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba linakata uzi mwekundu ambao umeshonea vazi letu la kikatiba katika nusu karne ya uhai wetu kama taifa huru. Wajukuu wa wajukuu zetu, na vizazi vyao vitakavyofuata kwa miaka mingi baada ya sisi tuliopo humu ndani kuwa tumeondoka kwenye dunia hii, wataandika kwamba Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuanzisha dhana ya Tume ya Katiba ya Wadau, badala ya utaratibu wa Tume ya Rais aliourithi kutoka kwa Marais waliomtangulia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo katika maoni yake ya tarehe 15 Novemba mwaka jana ilipendekeza kwamba “wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini”, inayaunga mkono mapendekezo ya marekebisho haya ya kihistoria.

Mheshimiwa Spika,

Kuna mambo mawili muhimu ya nyongeza kuhusu pendekezo hili la kihistoria. Kwanza, kwa kuzingatia wingi wa asasi za kiraia, taasisi za kidini, jumuiya na taasisi zisizo za kiserikali na makundi mengine ya watu yenye malengo yanayofanana, kifungu kipya cha 6(7) kinapendekeza kumrahisishia Rais kazi kwa kumwelekeza azingatie muungano au umoja wa makundi hayo pale anapoyaalika kumpelekea orodha ya watu wa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Pili, kwa kuzingatia kwamba Rais na Serikali anayoingoza pia ni wadau wakubwa na muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, kifungu kipya cha 6(8) kinapendekeza kumpa Rais mwanya wa kuteua wajumbe wengine kwenye Tume nje ya wajumbe watakaopendekezwa na wadau kwa mujibu wa mapendekezo ya kifungu kipya cha 6(6). Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na common sense iliyoangika mapendekezo yote mawili na inayaunga mkono.

Mheshimiwa Spika,

Jedwali la Marekebisho la Serikali linapendekeza kufanyiwa marekebisho kwa kifungu cha 12 cha Sheria kinachohusu ukomo wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Itakumbukwa kwamba katika hotuba yake ya tarehe 15 Novemba mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza kwamba namna mojawapo ya “... kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni kuhakikisha [kwamba] wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao ... sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe [hao] kuondolewa kwa sababu zisizotokana na utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili.”

Mheshimiwa Spika,

Pendekezo hili sasa limekubaliwa na Serikali kwani Jedwali la Marekebisho linapendekeza marekebisho ya kifungu cha 12 kwa kuongeza kifungu kidogo kipya cha (4) kinachoweka utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya wajumbe wa Tume. Kwa mujibu wa utaratibu unaopendekezwa, endapo suala la kuondolewa kwa mjumbe kwa ukiukwaji wa Kanuni za Maadili litajitokeza, Rais ataunda Kamati itakayochunguza suala hilo na kutoa mapendekezo kwake. Kamati hiyo inapendekezwa kuongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania huku wajumbe wengine wakiwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar aliyependekezwa na Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS) na wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyependekezwa na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS). Inapendekezwa kwamba endapo, baada ya uchunguzi wake, Kamati hii itapendekeza kwamba mjumbe wa Tume asiondolewe basi suala la kumwondoa litasitishwa.

Mheshimiwa Spika,

Sambamba na mapendekezo ya kifungu kipya cha 12(4), Jedwali la Marekebisho linapendekeza pia kwamba kifungu kipya cha 12(5) kiongezwe ili kuiwezesha Kamati kutengeneza utaratibu wake yenyewe wa kufanya uchunguzi. Aidha, inapendekezwa kuongeza kifungu kipya cha 13(7) kwa lengo la kuifanya Tume kuwa mamlaka ya kinidhamu kwa wajumbe wa Sekretarieti ya Tume. Kama ilivyo kwa Tume, pendekezo hili vile vile linalenga kuwahakikishia ulinzi wa kisheria watendaji na watumishi wa Sekretarieti ili kuwawezesha kutekeleza wajibu wao kwa uhuru na bila kuingiliwa na mtu yeyote kama inavyotakiwa na kifungu cha 10 cha Sheria hii. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na mapendekezo yote mawili.

Mheshimiwa Spika,

Mapendekezo mengine muhimu yanayopendekezwa na Jedwali la Marekebisho la Serikali yanahusu marekebisho ya kifungu cha 17 cha Sheria kinachoweka utaratibu wa utendaji kazi wa Tume. Kwa mujibu wa kifungu cha 17(5) cha Sheria ya sasa, Tume inaweza kumtaka Mkuu wa Wilaya, Afisa Mtendaji wa Kata au Mtaa au Afisa Mtendaji wa Kijiji (au Sheha kwa upande wa Zanzibar) kuitisha mkutano wa wakazi wa mji, kata, mtaa au kijiji au shehia kwa madhumuni ya kukusanya maoni ya wananchi hao kuhusu masuala ya Katiba.

Mheshimiwa Spika,

Kuna hofu kubwa sana juu ya nafasi ya Wakuu wa Wilaya katika mchakato wa Katiba Mpya kama ilivyowekwa na Sheria hii. Hofu hii sio unfounded kwani tangu Sheria hii itungwe mwaka jana, Wakuu kadhaa wa Wilaya wamenukuliwa na vyombo vya habari wakitishia kuamuru wawakilishi wa mashirika ya kiraia yanayoendesha elimu kwa umma juu ya mchakato wa Katiba Mpya wakamatwe kama watafanya programu za elimu hiyo katika maeneo yao. Vile vile, kwa mujibu wa Katiba ya CCM na tangu kuanzishwa kwa CCM mwaka 1977, Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM katika ngazi ya Wilaya. Kwa mfano, kwa mujibu wa Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya (ibara ya 42(3); ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 44(3); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 46(3).

Hata baada ya miaka thelathini tangu toleo hilo la Katiba ya CCM litolewe, na licha ya miaka ishirini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, hali bado iko vile vile kuhusiana na nafasi ya Wakuu wa Wilaya katika vikao rasmi vya CCM. Ndio maana, kwa mujibu wa ibara ya 76(1)(c) ya Katiba ya CCM Toleo la 2010, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya; ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 78(1)(c); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 80(1)(c).

Mheshimiwa Spika,

Hivi vyote ni vikao muhimu vya maamuzi ndani ya Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya. Kuwapo kwa Wakuu wa Wilaya katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kunaleta hofu ya msingi kwamba wanaweza kuhujumu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kwa sababu au malengo ya kisiasa. Kwa sababu hiyo, pendekezo la kuwaondoa Wakuu wa Wilaya – na badala yake kuwaweka Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa - katika mchakato wa kuitishwa kwa mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba Mpya linajenga imani kwa wadau wengine hasa hasa vyama vya siasa vya upinzani. Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa hawafungamani na chama chochote cha siasa ndio maana wamefanywa kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria zetu za uchaguzi. Vile vile pendekezo hili linawawezesha wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kufanya kazi kwa urahisi na watendaji wa Kata na wa vijiji ambao pia ni watumishi wa mamlaka hizo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayakaribisha na kuyaunga mkono mapendekezo ya marekebisho haya ya kifungu cha 17(5) ya Sheria.

Mheshimiwa Spika,

Moja ya mapungufu makubwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni kutokuwepo kwa utaratibu wowote wa utoaji wa elimu kwa umma juu ya mchakato wa Katiba Mpya. Ni ajabu kwamba wakati Sheria haijaweka utaratibu wowote, kifungu cha 21(2)(c) cha Sheria hiyo hiyo kimetangaza kwamba “mtu yeyote atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya Katiba kinyume na masharti ya Sheria hii atakuwa ametenda kosa”! Hii sio tu inapingana moja kwa moja na hifadhi ya uhuru wa maoni iliyowekwa na ibara ya 18 ya Katiba yetu, bali pia inaendeleza ujinga wa wananchi katika masuala muhimu ya kikatiba. Jedwali la Marekebisho ya Serikali linapendekeza kuondoa mapungufu hayo kwa kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa umma juu ya mabadiliko ya Katiba.

Kwa mujibu wa kifungu kipya cha 17(9), inapendekezwa kuwa mtu au taasisi yoyote inayotaka kuendesha programu ya elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya Katiba anatakiwa kutoa taarifa ya maandishi kwa Tume, au kwa Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na makatibu wa mabaraza ya miji kwa upande wa Zanzibar. Mtu au taasisi hiyo sharti iwe imesajiliwa na sharti ibainishe chanzo cha fedha zitakazotumika kuendeshea programu hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayakaribisha na kuyaunga mkono mapendekezo ya marekebisho haya kwa sababu yatawezesha wananchi kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba wakiwa na ufahamu mkubwa zaidi wa masuala ya kikatiba ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Sambamba na kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya mabadiliko ya Katiba kwa umma, kifungu kipya cha 17(10) kinapendekeza kuhifadhi uhuru wa asasi, taasisi au makundi ya watu “... kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wao kutoa maoni yao kuhusu Katiba na kisha kuyawasilisha kwenye Tume.” Mapendekezo haya sio tu yanatambua ukweli kwamba, kutokana na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa watu wake, haitawezekana kwa Tume kukutana na kila mtu kwa lengo la kukusanya maoni yake kuhusu mabadiliko ya Katiba. Pendekezo hili pia linaendana na haki na uhuru muhimu wa kufanya mikutano kwa mujibu wa ibara ya 17 ya Katiba yetu na wa maoni kwa mujibu wa ibara ya 18. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayaunga mkono mapendekezo ya marekebisho haya ya Serikali.

Mheshimiwa Spika,

Jedwali la Marekebisho la Serikali linapendekeza kupunguzwa kwa adhabu za watakaopatikana na hatia ya makosa ya kumkwamisha au kumzuia mjumbe wa Tume au Sekretarieti kutekeleza majukumu yake; kumkwamisha au kumzuia mtu au kundi la watu kutoa maoni kwenye Tume; kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kinyume na Sheria hii; kujifanya mjumbe wa Tume au Sekretarieti; na kuendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya Katiba kinyume na masharti ya Sheria hii. Makosa haya yako kwenye kifungu cha 21(1) na (2) cha Sheria na adhabu zake, kwa mujibu wa kifungu cha 21(3), ni faini ya kati ya shilingi milioni tano hadi milioni kumi na tano au kifungo cha kati ya miaka mitatu hadi miaka saba au vyote kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika,

Katika waraka wake kwa Mheshimiwa Rais, Kamati Maalum ya CHADEMA ilipendekeza kwamba vifungu vyote vinavyokiuka haki za kimsingi za kikatiba vifutwe na kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi juu ya utungaji wa Katiba Mpya na kuyawasilisha kwa Tume. Pamoja na kwamba vifungu vinavyofanya ukusanyaji na uratibu wa maoni ya wananchi na uendeshaji wa elimu kwa umma kuwa kosa la jinai havikufutwa kama tulivyopendekeza kwa Mheshimiwa Rais, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri, kwa kuzingatia haki zilizohifadhiwa na ibara za 17 na 18 za Katiba yetu ya sasa, kwamba Bunge hili tukufu litafakari kama kuna haja ya kuendelea kuwepo kwa makosa haya na adhabu zake katika Sheria itakayotuletea Katiba Mpya na bora kwa nchi yetu.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,

Naomba, katika kuhitimisha maoni yangu, kwa kusisitiza kwa mara nyingine tena mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais katika kuletwa kwa Muswada huu pamoja na Jedwali la Marekebisho lililoambatanishwa nao miezi miwili tu baada ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupitishwa na Bunge lako tukufu na kupata kibali cha Rais. Naomba nisisitize tena kwamba, katika jambo hili muhimu kwa taifa letu, Mheshimiwa Rais amekuwa msikivu kweli kweli kwani amejiweka juu ya the partisanship and factionalism of party politics na ameangalia maslahi mapana ya taifa letu. Ni wajibu wetu sasa kuwathibitishia Watanzania kwamba kazi kubwa ya Mheshimiwa Rais, na usikivu wake na uongozi wake katika jambo hili haukuwa wa bure.

Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafarijika kwamba Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge lako tukufu imeridhia na kukubali mapendekezo yote ya Muswada huu na Jedwali la Marekebisho la Serikali. Kwa sababu zote hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni sio tu inaunga mkono Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011, bali pia inatoa rai kwa waheshimiwa Wabunge wote, bila kujali the narrowness of our political party affiliations, tuungane na Mheshimiwa Rais katika kulipatia taifa letu utaratibu wa kutengeneza Katiba Mpya wenye muafaka wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza, naomba kuunga mkono hoja hii.---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
&
WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA

FEBRUARI 9, 2012

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.