KURUGENZI ya Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inapenda kutoa taarifa kuhusu habari zilizoripotiwa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, juu ya maombi ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinafanya usiku na mchana ili eti Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, agombee ubunge, kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Jimbo la Arumeru Mashariki, Aprili 1, 2012.

Ingawa haijajulikana maombi hayo yanafanyika msikiti upi au kanisa lipi au sehemu ipi yoyote ile nyingine ya kufanyia maombi, Kurugenzi imeshangazwa sana na mantiki ya kuwepo kwa maombi hayo ya CCM yakionesha upendo wa kutiliwa mashaka kuwa chama hicho kimefikia mahali kinaweza kufanyia maombi vyama vingine ili vipate wagombea makini wa kukibwaga vibaya sana katika uchaguzi.

Kurugenzi inapenda kusema yafuatayo juu ya maombi hayo ya CCM, ambayo kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, kama ilivyoripotiwa katika njia mbalimbali za upashanaji habari, imedhihirika dhahiri kuwa ni maombi yanayoongozwa zaidi na hila, husuda kwa CHADEMA na Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa;

Tunapenda CCM wajue kuwa CHADEMA na viongozi wake makini, akiwemo Katibu Mkuu, Dkt. Slaa, si watu wa kurudi nyuma. Chama hiki daima muda wote kinapanga mikakati na mipango ya kusonga mbele, kikionesha utawala mbadala, kikijiandaa kushika dola na kutekeleza malengo ya Watanzania!

Kwa mantiki hiyo, chama hiki hakiwezi kurudi nyuma, hakiwezi kumrudisha nyuma Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa kuwania ubunge. Kiongozi huyu makini, ambaye umma wa Watanzania una imani kubwa naye, ameshavuka viwango vya ubunge, si mtu wa kuwania nafasi ya ubunge tena, (is not parliamentary material).
Kwa nafasi yake ndani ya CHADEMA, anao wajibu mkubwa kujenga chama. Kwa kutimiza wajibu huo, Dkt. Slaa anafanya kazi ya kutengeneza na kuivisha watu wengine makini zaidi, kuweza kuwa viongozi ndani ya chama, nafasi za udiwani na ubunge, ili kuendeleza umakini na uimara wa chama hiki ambacho dhahiri ni tumaini jipya la Watanzania katika kutoa uongozi mbadala wa nchi.

Kwa umakini wa CHADEMA, uwezo wa Dkt. Slaa na matumaini makubwa ya Watanzania, ambayo wameendelea kuyaonesha kwa chama hiki tangu mwaka 2007, kilipoanzisha rasmi mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi, kisha kudhihirika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, nafasi pekee inayomstahili Dkt. Slaa ni urais kwa maana ya kuwa ni ‘presidential material’, si ubunge.

Lakini pia, tunatambua kuwa CCM, wameweza kutoa kauli hiyo ya kukurupuka baada ya Dkt. Slaa kuwa tayari ametamka wazi tangu awali na kurudia kauli yake thabiti mara kadhaa kuwa hana nia wala mpango wa kuwania ubunge mahali popote pale nchini. Hawezi kufanya hivyo kwani hata ubunge wa Karatu hakushindwa bali aliacha mwenyewe kwa hiari yake, ili kutekeleza mahitaji ya umma wa Watanzania.

Kurugenzi ya Habari na Uenezi inatumia nafasi hii kuwaambia CCM kuwa watambue CHADEMA ni chama makini. Kimedhihirisha hivyo mara kadhaa katika masuala makubwa kwa maslahi ya Watanzania. Kitaendelea kudhihirisha hivyo pia katika uchaguzi wa Arumeru kwani kina utaratibu wa kuwapata wagombea wake, kutokana na maamuzi ya wanachama wake.

Tunatambua kuwa kauli hiyo ya CCM pia ni sehemu ya mkakati wa makusudi kuwakatisha tamaa baadhi ya watu wanaotaka kugombea jimbo hilo kupitia CHADEMA. Kurugenzi ya Habari na Uenezi inapenda kusisitiza taarifa ya awali, kuwataka wanachama wetu wajitokeze kwa wingi kuwania uteuzi wa kugombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki.

Tunataka CCM wajue kuwa suala la kuteua mgombea wa CHADEMA ni la CHADEMA yenyewe, kwa kutumia utaratibu wake, ikiongozwa na katiba, kanuni na mahitaji ya umma, wala hatuhitaji ushauri wa chama ambacho kadri siku zinavyokwenda, kinadhihirisha kila dalili ya kuchoka kujisimamia chenyewe, kusimamia wanachama wake, kusimamia serikali na maendeleo ya watu, hivyo kupoteza kabisa ushawishi kwa wananchi. Wala hatujawahi kuomba ushauri kutoka kwao hata siku moja.

Lakini maombi hayo ya CCM, kama ambavyo Nape amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema, yamedhihirisha namna ambavyo chama hicho bado kinaandamwa na mzimu wa CHADEMA na Dkt. Slaa tangu baada ya uchaguzi mkuu, kwa kuiba kura na kuvuruga matokeo ya uchaguzi huo.

Kauli ya Nape kuwa iwapo maombi yao yatafanikiwa na Dkt. Slaa akawania ubunge, CCM watakuwa wamemaliza kazi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, inathibitisha tuhuma hizo na namna ambavyo CCM hakikushinda kwa haki uchaguzi huo.

Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya pia inataka CCM waelewe kuwa umaarufu wa CHADEMA hautokani na umaarufu wa mtu mmoja mmoja wala hausubiri matukio pekee, bali unatokana na uongozi makini, kuanzia ngazi ya taifa hadi ya msingi, kikijikita katika kusimamia masuala yenye maslahi kwa Watanzania na nchi yao muda wote!


Imetolewa leo Februari 18, 2012, Dar es Salaam na


Tumaini Makene
Afisa Habari wa CHADEMA