Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 13, 2012

MAMBO YA KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA




Jambo la Pili

Unapoamua kuoa au kuolewa, fahamu ya kwamba hiyo ndoa
inakuunganisha na kukuingizakatika familia nyingine.

 Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana. Kwa sababu unapooa unaingia kwenye undugu na familia nyingine kabisa tofauti, na sio mahusiano ya kwenu tu wawili.  Ninyi ni kigezo tu cha kuunganisha hizo familia mbili, lakini mkiishaoana hizo familia zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.
 Ndio maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio suala la kumtazama kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake ili ujue unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika kwenye masuala ya namna hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.
 Unaweza ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu, mimi ninakuambia jasho litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata kijana toka kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi mwenzako juu ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa kuwa unaweza kuoa msichana hata kusonga ugali hajui. Sisi kwenye nyumba ya baba yetu, hatuna msichana, tumezaliwa watoto wa kiume watupu, msichana wa kwanza kuingia kwenye familia yetu ni mke wangu.
Lakini mama yetu alikuwa na bidii ya kutufundisha kila kitu, alitufundisha kupika, alitufundisha kufuma, alitufundisha kusuka nywele. Kwa hiyo nilijifunza kwanza kusuka tatu kichwa. Lakini sikuanzia kujifunzia kusuka nywele kwenye kichwa cha mtu, bali nilijifunzia kwenye majani; wao wakikaa wanasuka hapo na sisi tuko hapo tunafundishwa jinsi ya kusuka kwenye majani.
Sasa wengine hawapati nafasi ya namna hiyo, na ni mbaya zaidi kwa wasichana. Mungu amenipa nafasi ya kuwa na watoto wakike watatu na wa kiume mmoja, itakuwa ni aibu kwetu kama wazazi, ikafika wakati wanaingia katika ndoa zao na  hawajui kupika ni aibu; kwa hiyo lazima wajue kupika. Maana kwa kujua hilo anaonyesha anatoka familia ya namna gani, na imemlea kwa namna gani!
Unaweza ukafikiri unamlea mtoto wako vizuri, maana siku hizi kuna shida ya kuwa na wafanya kazi majumbani mwetu. Ukishakuwa na mfanyakazi nyumbani basi watoto wengine hawafanyi kitu, wakati mwingine wanakula  chakula na wanaacha sahani hapo hapo mezani.
Kuna watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari hawezi kufua nguo zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna mashine za kufulia. Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata mashine ya kufulia hawajawahi kuiona! Unafika pale na unauliza mashine iko wapi, wanakuambia yakufanyia nini, - ya kusagia mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa ndio mashine!
 Hujui hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli wala namna ya kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika ndoa unaenda kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule na unashangaa kweli maana hujui hata namna kuwasha taa ya chemli! Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala la kujifunza hivi vitu sio suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani wa kuwasaidia, ni lazima wajue kufanya kazi!
Nilienda kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka kuoa kwenye nyumba ya mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au vibaya wakasema usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye uwanja wa nyumba ya wazazi wake, na wanaangalia ile barabara inayokwenda nyumbani  kwao, na wakiikuta chafu, basi wanajua huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza, wanajua hapa kama tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana ni mchafu!
Ukienda kuoa kwenye familia nyingine utakuta wanasumbuliwa na ugonjwa wa kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza ukapata shida sana. Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au kuolewa unakuingiza kwenye familia nyingine kabisa, na inaunganisha  hiyo familia yao na familia yako; kwa hiyo hayo sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa au kuolewa  unawaingiza watu katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu inaweza ikaleta shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.

Mwl Mwakasege

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.