Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, March 2, 2012

WATUMISHI WA SERIKALI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA BIDII KISHA KUDAI HAKI ZAO

Watumishi wa serikali ambao ni wanachama wa TUGHE wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza wajibu wao na hatimaye waweze kupata haki ya kudai nyongeza ya maslahi kwa mwajili.

Rai hiyo Imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Tughe Taifa Ally Kiwenge wakati akiongea na watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali hiyo.

Bw Kiwenge alisema ili Wafanyakazi waweze kuwa na sauti ya kudai hali bora ya maslahi kwa mwajili ni budi wao kwanza wakafanya kazi kwa bidii na kuzingatia taratibu.

Alizitaja taratibu kama kuwahi kazini na kuwajibika katika sehemu zao za kazi pia kuacha uzembe,uzururaji na kupiga majungu kuwa ndio nguzo za kuwa na Utendaji mzuri mahala pa kazi

“Watumishi wa serikali tuache maneno ya kejeli na uchochezi na tutumie vikao halali kuwasilisha kero na matatizo yetu kwa mwajili” alisema Bw Kiwenge na kuongeza kuwa kwa watumishi wazembe na wapika maneno sehemu za kazi Tughe haitojishughulisha kuwatetea endapo hatua za kinidhamu zitachukuliwa na waajiri.

Aidha katika hatua nyingine Katibu huyo wa Tughe Taifa amepongeza kitendo cha Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari kwa kuonyesha umakini wa kushughulikia kero za watumishi wa sekta ya afya kupitia tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kufuatia mgogoro wa madaktari nchini.

Alisema “namshukuru Rais Kikwete kwa kuwahakikishia watumishi wa sekta ya afya nchini kuwa atahakikisha kero za Wafanyakazi kama si kuzimaliza zote basi atasimamia kuona zinapungua “.na kuongeza kuwa Rais akishasema wao viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wanafarijika kuona serikali inasikia kilio cha watumishi nchini.

Katika kikao hicho Bw Kiwenge alitaja matatizo makuu manne ambayo serikali inapaswa kuyafanyia kazi kwa kipindi hiki .Kwanza,watumishi wanahitaji nyenzo za kufanyia kazi za kisasa katika hospitali zote nchini ili wananchama wa Tughe watekeleze vema majukumu yao.

Aliongeza na kuiomba serikali na kuishauri ihangaike na kutoa nyenzo za kufanyia kazi kwenye hospitali zote nchini.

Pili,Wafanyakazi wanataka kuwa na majadiliano na viongozi wao ili kuwe na ushirikiano katika kutatua kero zinazojitokeza mahala pa kazi kabla madhara hayajawafika wananchi.

Tatu,amewasihi na kuwaonya watumishi wa serikali kutojiingiza katika siasa.”Kuwa na chama chako na hisia zako ni haki ya mtumishi lakini usilete na kuingiza siasa zako kazini” alisema Kiwenge

Nne,ameitaka serikali ichukue maamuzi magumu ya kuboresha maslahi ya watumishi wake wa sekta ya afya kama kweli inasema sekta hii ni muhimu . “Tughe inaishauri serikali ifanye maamuzi magumu ya kupandisha mishahara ya watumishi ili ikidhi mahitaji ya mwezi mzima ”.

Ameongeza kusisitiza kuwa kiwango cha kima chini i kinacholipwa sasa na serikali cha shilingi laki moja na nusu hakitoshi kumwezesha mtumishi kukidhi mahitaji yake kwa mwezi mzima ambapo kwa wastani mtumishi mwenye familia yenye mke na watoto wanne anaishi kwa shilingi mia nane .

Alisema Tughe inaiomba na kuisisitiza serikali anagalau ihakikishe mtumishi anaishi kwa zaidi ya dola moja yaani shilingi elfu moja na mia sita kwa siku kwani kinyume na hapo watumishi wa serikali wataendela kuishi katika umasikini kinyume na sera ya maisha bora kwa mtanzania.

“Mtumishi yeyote anyeishi chini ya dola moja kwa siku anaishi katika umasikini mkubwa” alisema Bw.Kiwenge na kusisitiza kuwa ni wakati sasa umefika kwa serikali kusikia kilio cha watumishi na kupandisha mishahara kwa kima cha chini hadi shilingi 350,000/=kwa mwezi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma Dkt.Benedict Ngaiza aliwataka viongozi wa Tughe kuwa mfano wa kuigwa kwa kuonyesha njia badala ya wao kuwa walalamikaji kwani hilo likifanyika litaendeleza na kudumisha ushirikiano mahala pa kazi.

…………………………………………………………………………………………………………………………..

Na Revocatus A.Kassimba

Afisa Habari

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.