Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, March 2, 2012

RAIS JK AWATETEA WANAISHI KUIZUNGUKA MIGODI

RAIS Jakaya Kikwete amewaagiza wawekezaji katika sekta za madini, gesi na mafuta, kuhakikisha misaada kwa jamii inayowazunguka inakuwa moja ya sera zao za kibiashara ili kutoa fursa ya wananchi kufaidika na rasilimali zao.

Akizindua Tuzo ya Rais kwa kampuni zinazojihusisha na sekta ya uziduaji juzi usiku Dar es Salaam, pia aliwaagiza wawekezaji hao wa ndani na nje, kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za Serikali kwa wakati bila kusukumwa.

“Cha msingi hapa ni kulipa kodi na jamii ifaidike na rasilimali zake na ninyi pia mfaidike na uwekezaji wenu,” alisema Kikwete na kuongeza kwamba iwapo kampuni hizo zitatekeleza masuala hayo zitafanya biashara zao ziwe endelevu zaidi.

Rais alisema kuwapo vurugu katika baadhi ya maeneo ya uwekezaji, kunachangiwa na wananchi kutoona faida kutokana na rasilimali zao na akaongeza kuwa iwapo wawekezaji watawajibika kwa jamii walimowekeza, kutakuwa na maelewano mazuri ya kibiashara baina yao.  

“Hii italeta maelewano mazuri kati ya wawekezaji na jamii katika maeneo mlimowekeza, la sivyo uhusiano unaweza kuwa mbaya na kuibuka misiguano mibaya katika masuala ya kibiashara,” alionya Rais na kutoa mfano kwa wazalishaji wa sukari wanavyoshirikiana na wakulima wadogo wa miwa katika maeneo yanayowazunguka.

Katika hotuba yake, Rais aliagiza pia kampuni za uwekezaji kuwa na sera za kununua bidhaa za nchini. Alisema kuna bidhaa na huduma ambazo zinapatikana nchini na hivyo kutokuwapo haja ya kuagiza nje. Alisema hiyo ni njia mojawapo ya kuwawezesha wananchi na kuinua uchumi wa mahali kuliko na uwekezaji.

Alitoa mfano alivyokwenda hoteli ya kitalii nchini na kukuta maji ya kunywa yanatoka nje ya nchi, jambo ambalo halikumfurahisha na akagoma kuyanywa. “Kwa nini muagize maji nje ya nchi wakati tuna Uhai, Ndanda, Kilimanjaro na Masafi? Haya mambo hayafurahishi wananchi,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Kuna bidhaa na huduma nyingi ambazo mnaweza kununua nchini na hii ni moja ya kukuza uchumi wa wananchi wetu.” Rais alisema utaratibu huu wa kampuni kushirikiana kiuchumi na jamii zinazozunguka miradi yao ya uwekezaji, utasaidia kuongeza ajira na kipato kwa jamii husika.

“Hii itawafanya watu wajihisi na wao ni sehemu ya umiliki na wana wajibu wa kulinda wawekezaji … lakini kama hilo halifanyiki, watu hawatafurahishwa na shughuli zenu za uwekezaji na matokeo yake hawatajali uwekezaji huo; hivyo nakuombeni suala hili mlitilie maanani.
“Watu watajiuliza wanapata nini, dhahabu yetu inachukuliwa, kampuni hizi zina misamaha ya kodi, lakini hata hawatuungi mkono kiuchumi kwa kununua bidhaa zetu. Hawatakuwa na chochote katika biashara hii,” alisema.

Eneo lingine ambalo Rais aliagiza wawekezaji walifanye kama sera yao ya uwekezaji ni kujenga uhusiano kati ya kampuni kubwa, ndogo na wananchi ambao wamo kwenye sekta inayofanana. Alisema ni wajibu wa kampuni kubwa za kigeni kusaidia ndogo za wananchi ili nazo zifanikiwe.


“Kampuni kubwa zitumie uchumi wao na maendeleo yao ya kiteknolojia, kusaidia kampuni ndogo za wananchi ili kuboresha na kuongeza uzalishaji. Ninaamini hii itaisaidia kupunguza wivu, misuguano na kuongeza urafiki na uhusiano mzuri,” alisema Rais Kikwete.

Mapema akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema sekta ya uziduaji imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto za namna wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji wanavyoweza kufaidika na miradi ya uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tuzo ya Rais ambayo lengo lake ni kuhamasisha wawekezaji wawe karibu na jamii zinazowazunguka itakuwa inatolewa kila mwaka kwa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo katika sekta hii ya uziduaji,” alisema Ngeleja.

Tuzo hiyo imeandaliwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Madini (MISF). MISF ni asasi ya faida na inahusisha kampuni ambazo zimesaini hati ya makubaliano (MoU) na Wizara ili kuwa na jukwaa lenye jukumu la utetezi wa sera, utafiti, elimu na namna ya kutatua migogoro kati ya wawekezaji na wanajamii.
Tuzo hiyo inatarajiwa kuhamasisha sekta za madini, gesi na mafuta kushirikiana na jamii katika kuboresha uchumi wa maeneo ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii ya maeneo husika.


No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.