Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, March 9, 2012

Mkapa aitosa CCM

UZINDUZI wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi uliokuwa ufanyike Machi 10 imeingia dosari kubwa kufuatia kukataa kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kufanya kazi hiyo.

Habariza kuaminika kutoka ndani ya CCM zimedai kuwa Mkapa amegoma kufungua kampeni hizo zilizokuwa zifanyike eneo la Usa River nje kidogo ya jiji la Arusha nakuna habari kuwa uongozi wa juu umelazimika kuahirisha na kusogeza mbele siku ya uzinduzi.

Ofisa mmoja mwandamizi wa CCM ameliambia Tanzania Daima kuwa Mkapa amechukua uamuzi huo baada ya kubainika kuwa ataaibika kutokana na msuguano mkali wa chini kwa chini baina ya makundi yaliyoibuka tangu wakati wa mchakato wa kura za maoni.

Mtoa taarifa wetu amesema kuwa Mkapa ametoa sharti zito la kuutaka uongozi wa wilaya, mkoa na taifa kuhakikisha kuwa umeshughulikia kikamilifu msuguano wa makundi hayo, la sivyo hataweza kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo. Habari zimedai kuwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Elishiria Kaaya, na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa, James Milya, wameitwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili msuguano huo.

Imedaiwa kuwa wengine walioitwa ni pamoja na wagombea wawili waliokuwa wakichuana kuwania kuteuliwa kugombea ubunge wa jimbo hilo, William Sarakikya, na Elirema Kaaya (ambaye aliwahi kushikiliwa na Takukuru akituhumiwa kutoa rushwa kwa wagombea).

Taarifa zimedai kuwa hali ndani ya chama hicho ngazi ya mkoa ni mbaya pamoja na wagombea walioangushwa na Siyoi Sumari kukubaliana kuwa wataungana pamoja kumpigia kampeni mwezao ili ashinde. Hata hivyo, habari zimethibitisha kuwa uhasama baina ya makundi hayo, lile la James Milya na Mary Chatanda, kwa upande mwingine, yamekuwa katika mvutano wa siku nyingi na kwamba uchaguzi huo mdogo umeibua uhasama huo.

Alipopigiwa simu kuthibitisha kusogezwa mbele kwa uzinduzi wa kampeni hizo na ukweli wa kugoma kwa Mkapa, Chatanda alidai kuwa yuko barabarani na akaombwa apigiwe simu kesho (leo). Hata hivyo, alipoambiwa ni jambo la dharura, alikata simu na kuzima.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nnauye, alipoulizwa juu ya kukataa kwa Rais Mstaafu Mkapa, alikana kujua lolote huku akitaka mwandishi amuulize aliyemwambia habari hizi. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Arusha, James Millya, hakupatikana na mmoja wa watu wake wa karibu, alilieleza Tanzania Daima kuwa kiongozi huyo machachari wa UVCCM, alikuwa jijini Dar es Salaam kikazi.

Mkapa aliteuliwa hivi karibuni na makao makuu ya CCM kuzindua rasmi kampeni za ubunge wa jimbo hilo, ikidaiwa kuwa ndiye mmoja wa viongozi wachache wenye uwezo mkubwa wa ushawishi katika masuala ya kampeni. Itakumbukwa kuwa Mkapa ndiye aliyezindua na kisha kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, ambako kampeni zake baina ya CCM na CHADEMA zilivunja rekodi kwa mbwembwe, mikikimikiki na tambo za kila aina ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha.

Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki unatabiriwa kuwa utakuwa na ushindani mkubwa kati ya wagombea wawili wa vyama vya CCM (ambacho kimemsimamisha mtoto wa marehemu Jeremiah Sumari), Siyoi Sumari, na CHADEMA ambacho kimemteua Joshua Nassari kupeperusha bendera yake.


Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.