Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, March 2, 2012

JK: Nilisaini Sheria ya Katiba kuepuka hasira za wabunge

Rais Jakaya Mrisho Kikwete



Raymond Kaminyoge
RAIS Jakaya Kikwete amesema alisaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kukwepa hasira za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete alitoboa siri hiyo katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari aliyoitoa juzi kupitia vyombo vya habari.Uamuzi huo wa Rais kutia saini muswada huo ambao tayari ulikuwa umepingwa kila kona ya nchi licha ya kupitishwa na Bunge, ulizidi kuibua hasira za makundi mbalimbali ya kijamii.

Rais wakati akisaini muswada huo, Novemba mwaka jana, alikuwa ameanza  mazungumzo na makundi  ya  kijamii ukiwamo ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).   

Lakini, mwenyewe akifafanua ni kwa nini alisaini muswada huo wakati ulikua ukipingwa na wananchi na huku akiwa katika mazungumzo na wadau, ndipo alisema, “Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa wabunge walio wengi.

... ambao waliujadili muswada huo na kuupitisha. Wangeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana hawana thamani.”

Rais Kikwete alisema vyama vya siasa na asasi za kiraia waliomba asitie saini na badala yake aliagize Bunge liujadili tena muswada huo.

“Sikutaka kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba  usiokuwa wa lazima unaoweza kuepukwa kwa kutumia njia nyingine za kisheria na kikatiba,” alisema Kikwete.

Alisema, alipofanya mazungumzo  na vikundi hivyo vya kiraia, aliwaeleza kuhusu ugumu huo wa kuacha kutia saini na kuurudisha bungeni kujadiliwa upya.

Kikwete alisema kama muswada huo ungerudishwa kujadiliwa bungeni, kuna hatari asingeweza kupata ushirikiano wao na kushindwa kupata kile kilichotarajiwa.“Wangeweza kujadili na kuamua kuyakataa mapendekezo yote mapya na kubakia na msimamo wao ule ule,” alisema.

Mauaji ya Songea
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alizungumzia mauaji ya Songea akisema, amesikitishwa na mauaji hayo, lakini akaahidi kufanyika kwa uchunguzi ili kuwashughulikia waliohusika kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema yapo mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina na yapo yaliyotokea kwenye maandamano.

“Napenda kutumia nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa vifo hivyo na kutoa pole na rambirambi zangu na za wananchi wa Tanzania, kwa ndugu wa marehemu wetu hao,” alisema Kikwete.

Aliongeza;“Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji hayo hadi wahusika wote wapatikane,” alisema.

Kikwete alisema hadi sasa yametokea mauaji ya watu  13 yanayohusishwa na imani za ushirikina na kwamba watuhumiwa 26 wamekwishakamatwa kutokana na mauaji yao.

Kuhusu mauaji yaliyotokana na maandamano, alisema askari wanne wamekamatwa na upelelezi unaendelea.

Taarifa kutoka katika Mkoa wa Ruvuma zilisema watu wanne waliuawa na Polisi wakiwa kwenye maandamano hayo.“Nashukuru kwamba amani na utulivu vimerejea katika Manispaa ya Songea, nawapongeza viongozi wa ngazi zote na wananchi kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwezesha amani kupatikana,” alisema Kikwete.
  

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.