Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Thursday, March 1, 2012

Barua nzito ya JK yawasilishwa mahakamani


na Happiness Katabazi

HAKIMU Mkuu Mfawidhi, Elvin Mugeta, jana alitupilia mbali pingamizi la wakili wa serikali Ponsian Lukosi, Ben Lincol, lililotaka mahakama hiyo isipokee barua ya Machi 21 mwaka 2001 iliyoandikwa na Mahalu kwenda kwa Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akimwarifu kuhusu jengo hilo litauzwa na mwenye jengo kwa mikataba miwili.
Badala yake mahakama iliipokea barua hiyo kama kielelezo cha ushahidi, kinyume na madai ya Wakili Lukosi aliyesema kuwa ilikuwa ni ya siri na binafsi na si ya kiserikali. Hakimu Mugeta alisema kuwa barua ilikuwa ni ya kiserikali kwani ina nembo ya serikali na inatunzwa na ofisi za serikali na Mahalu aliituma pia kwa viongozi wengine wa serikali.
Katika utetezi wake aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyempatia mamlaka ya kisheria (Special Power of Attorney) ya kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchi Italia kwa kutumia njia ya mikataba miwili kwa thamani ya euro 3,098,034.
Profesa Mahalu alitoa maelezo hayo kwa maandishi jana wakati akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake, Mabere Marando, ambapo jana mshitakiwa huyo alimaliza kujitetea.
Profesa Mahalu alisema akiwa Balozi mjini Rome, Kikwete ambaye wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alimpatia nguvu maalumu ya kisheria (Special Power of Attorney) ya kununua jengo hilo kwa thamani ya euro milioni tatu, Septemba 2002 na kwamba aliipokea na kuifanyia kazi kwa vitendo na ilikuwa na saini ya Rais Kikwete.
Aliendelea kueleza kuwa Machi 24 mwaka 2004 , alimwandikia barua Kikwete akiambatanisha nyaraka zote za ununuzi na nakala ya barua hiyo kumtumia Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Mhasibu Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Brandina Nyoni na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.
Mahakama pia ilikubali kupokea barua hiyo kama moja ya kielelezo.
“Mheshimiwa hakimu, Aprili 23 mwaka 2008 shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri ambaye alikuwa ni mhasibu wa ubalozi huo, Steward Migwano, alipotoa ushahidi wake alileta nyaraka ya mikataba hiyo miwili na nyaraka za kibenki za kibalozi zilizoonyesha jinsi ofisi ya ubalozi ilivyopokea fedha kutoka Serikali ya Tanzania na jinsi ubalozi wetu ulivyotoa fedha hizo kwa awamu na kwenda kumlipa mmiliki wa jengo hilo kwa awamu na itoshe kusema kuwa ushahidi wa shahidi huyo wa tatu wa Jamhuri unaunga mkono utetezi wangu.
“Na Oktoba 24 mwaka 2008 shahidi wa tano ambaye ni Mchunguzi kutoka TAKUKURU, Isidori Kyando, alitoa ushahidi unaotofautiana na wangu na hotuba ya Kikwete aliyoitoa bungeni Agosti 3, mwaka 2004 , ambapo shahidi huyo alidai yeye anautambua mkataba mmoja tu wa (official price) ambao unaonyesha jengo hilo lilinunuliwa kwa euro 1,032,913.80,” alidai Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alidai ushahidi wa Kyando unatofautiana na wake na hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete katika mkutano wa 16 wa Kikao cha 39 cha Bunge, Agosti 3 mwaka 2004, ambapo wao wawili, yaani (Mahalu) na Kikwete kwa maandishi walieleza kutambua kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni ule wa (book value ) ambao unaonyesha jengo lilinuliwa kwa euro 1,032,913.80 na katika tarehe tofauti likanunuliwa katika mkataba wa pili uliotambulika kwa bei ya kibiashara (Commercial price) ambapo katika mkataba huo wa pili unaonyesha jumla jengo hilo lilinunuliwa kwa thamani ya euro 3,098,034.
Aidha, aliendelea kueleza kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake bungeni kuhusu sakata la ununuzi wa jengo hilo kwa mikataba miwili, alilieleza Bunge kupitia Hansard ya Bunge ukurasa wa 166 alisema: “Naibu Spika, mwaka 2001-2002 Wizara ya Mambo ya Nje ilinunua jengo hilo la ubalozi kwa thamani ya euro 3,098,034 ili serikali iweze kuondokana na mzigo wa kupanga ofisi na ununuzi wa jengo hilo ulifuata taratibu zote za serikali.”
Mahalu alisema taratibu hizo zilipata baraka za wizara yake, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha na kwamba Machi 6, 2002 serikali ilituma fedha za awali kwa ajili ya manunuzi hayo katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, na akaomba kumbukumbu hiyo ya Bunge ipokewe kama kielelezo ambapo Hakimu Mugeta aiipokea.
“Kwa hiyo mheshimiwa hakimu utaona bei ya manunuzi ya jengo hilo iliyotajwa na Rais Kikwete bungeni na bei ya jengo hilo niliyoitaja mimi na yule shahidi wa upande wa Jamhuri, Migwano, zinafanana,” alidai Mahalu.
Hata hivyo alidai kuwa anashangazwa na upande wa Jamhuri kumfungulia kesi hiyo ya uhujumu uchumi kuhusu ununuzi wa jengo hilo kwasababu hadi upande wa mashitaka unaifunga kesi yake mwaka juzi, haujaleta ushahidi unaoonyesha aliyekuwa akiuza jengo hilo alikuwa hajapata fedha ambazo zilitumwa na serikali katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ili wamlipe muuzaji na pia upande wa mashitaka haujaleta ushahidi wowote wa maneno au nyaraka kuonyesha serikali iliwahi kukataza au kulalamikia utaratibu wa ununuzi wa jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili:
“Na ili kuithibitishia mahakama hii kuwa nchini Italia, kununua ardhi, jengo au kupangisha jengo, mikataba miwili haizuiwi kisheria, naomba nitoe kitabu kilichoandikwa na mwandishi aitwaye Tobias Jones, ambacho kina kichwa cha habari kisemacho ‘ The Dark Hearty Italy’ kama kielelezo.
“Ukurasa wa 139-140 wa kitabu hicho, mheshimiwa hakimu, mwandishi huyo raia wa Italia, anaeleza wazi kuwa suala la mikataba miwili nchini ni la kawaida na wananchi wa Italia wamekuwa wakifuata utaratibu huo ambao hauzuiwi kisheria na akafafanua kuwa mkataba wa kwanza ambao unaitwa (book value) ndio mwisho wa siku unakuwa hati ya mali, liwe jengo au ardhi na kwamba katika ununuzi wa kupitia mikataba miwili risiti ya ununuzi inakuwa ni moja tu,” alidai Profesa Mahalu.
Hata hivyo wakili Marando alipomuuliza Mahalu kuwa amewahi kupata rekodi yoyote ya ubadhirifu wa mali ya umma, Mahalu alikanusha hilo na kuonesha zaidi ya medali tano mahakamani hapo alizotunukiwa na rais wa Italia na marais wengine duniani na mashirika mengine ya kimataifa kwa ajili ya uadilifu, uchapa kazi wake na jitihada zake za kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali ya Italia na Tanzania.

Tanzania daima

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.