Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe


  • Zimekuwa zikijizalisha maalumu kushambulia ngozi


WAKATI bado kukiwa na hali ya kutothibitishwa kitabibu Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameathirika kiafya kwa kupewa sumu au la, taarifa za awali zinabainisha kuwapo kwa ‘kitu’ kwenye ute ute (bone marrow) ndani ya mifupa yake, chenye uwezo wa kuzalisha kemikali zinazoshambulia chembe hai za ngozi, Raia Mwema, limeelezwa.


Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizotufikia kutoka vyanzo mbalimbali vya habari hospitalini Apollo, India, awali alipofikishwa nchini humo, jopo la madaktari bingwa walifanya uchunguzi na kubaini ‘kitu’ hicho kwenye ute ute ndani ya mifupa yake.

Hata hivyo, taarifa hizo zinabainisha kuwa baada ya kufanya utafiti wa kina, madaktari hao ambao miongoni mwao ni mabingwa wa kutafiti kemikali, walifanikiwa kubuni chembe nyingine za kudhibiti kemikali (kitu) zilizobainika ndani ya ute ute huo.


“Katika hali ya kushangaza, baada ya kubaini kuwapo kwa kemikali ndani ya ute ute wake na jopo la maprofesa ambao ni madaktari bingwa kufanikiwa kubuni namna ya kudhibiti hicho kilichogundulika, walishtushwa kemikali hizo kuwa na uwezo wa kuendelea kujizalisha na kuendelea kushambulia ngozi yake,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka hospitalini Apollo, nchini India ambako Dk. Mwakyembe alikwenda kutibiwa kwa mara ya kwanza.


“Kwa hiyo, walianza kazi ya kupambana na kemikali hizo zisiweze kuendelea kujizalisha na walipoona dalili za kufanikiwa walimruhusu kurejea Dar es Salaam, lakini wamechukua kemikali hizo kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Sasa ni majopo ya kitabibu yanayokusanya maprofesa kadhaa ndiyo wanaoendelea na uchunguzi wa kina kubaini ni kemikali za aina gani, zimeingizwa vipi mwilini mwake.”


“Na sasa amekuja hapa India kwa ajili pia ya kuangaliwa maendeleo yake. je, kemikali zile zimefanikiwa kuangamizwa kama bado zimepungua kwa kiasi gani au bado zina uwezo wa kuendelea kujizalisha kama ilivyokuwa awali? Kwa hiyo, uchunguzi bado haujakamilika,” kinaeleza chanzo hicho chetu cha habari kutoka Apollo.


Kwa upande mwingine, mara baada ya kurejea kutoka India kwa mara ya kwanza alikokwenda kutibiwa, mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kuona baadhi ya picha za hali ya Dk. Mwakyembe na namna ngozi yake ilivyokuwa imeathirika, mwili ukiwa umevimba na ngozi kuchanika na kuwa kavu na ngumu na yenye magamba mithili ya ngozi ya mamba.


Ni wakati huo ambao, Dk. Mwakyembe mwenyewe alipata kumdokeza mwandishi wetu kwamba; “Hali ilikuwa mbaya sana alipokuwa India kwa matibabu kwa mara ya kwanza.”


Lakini kwa upande mwingine, wataalamu wengine wa kemia na baiolojia nchini kwa nyakati tofauti bila kutaka majina yao yaandikwe gazeti kutokana na namna suala la Dk. Mwakyembe linavyozungumziwa na viongozi wa taasisi nyeti nchini, wameelezea uwezekano wa kurutubishwa kwa kemikali za namna hiyo ili kushambulia baadhi ya chembe hai katika mwili wa binadamu na hatimaye kusababisha kifo cha mhusika na baadaye, kifo hicho kuaminika kimetokana na ugonjwa fulani.


Katika hatua nyingine, taarifa za “internet” zinabainisha kuwa kemikali za namna hiyo huweza kutengenezwa na wakemia sambamba na wanabaiolojia kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwadhuru watu mashuhuri kwa malengo mbalimbali.


Kazi za ute-ute (bone marrow) mwilini

Kazi kubwa ya ute uliopo ndani ya mfupa wa mwanadamu (bone marrow) ambao humo ndimo inaelezwa kuwa kemikali zinazomdhuru Dk. Mwakyembe zilipo, ni kuzalisha aina tofauti za chembe hai za damu ambazo ni muhimu kwa afya ya mwanadamu kwa ujumla.

Kuna aina mbili za ute huo katika mifupa ya mwanadamu ambazo ni kwanza; ute wa njano (yellow bone marrow) ambao umesheheni kiwango kikubwa cha chembe hai zenye mafuta (fat cells).


Lakini aina ya pili ni ute mwekundu (red bone marrow) ambao hujumuisha chembe nyingine hai muhimu katika uzalishaji wa chembe damu mpya (new blood cells).


Kazi ya chembe damu na ute-ute

Ute mwekundu ndani ya mfupa (red bone marrow) na hasa katika mifupa mikubwa wajibu au kazi yake ya msingi ni uzalishaji wa shehena ya chembe damu hai mpya.

Ute ute huo unatajwa kujihifadhi katika mifupa ya mwanadamu hususan katika maeneo matano ya aina ya mifupa.


Mifupa hiyo ni; mosi, mifupa ya mkono (arm bones), pili; mifupa ya kifuani (breastbone); tatu, mifupa ya miguu (leg bones); nne, mifupa ya mbavu (ribs) na tano, uti wa mgongo (spine)


Kwa upande wa Dk. Mwakyembe, picha za mionzo zilizopata kuonwa na mmoja wa watu wake wa karibuni akiwa katika matibabu India zinadaiwa kuonyesha mifupa iliyoanza kuathiriwa kwa kuwa na alama za awali tofauti na mingine ni ya mifupa ya mikono kuelekea mifupa ya kifuani, na kwa hiyo, kama ni kitu (sumu?) kilichokuwapo kwenye ute wa mifupa yake basi kiliingia ,inawezekana kupitia viganja vya mikono yake na kupenya kwenye ute ndani ya mifupa ya mikono.


Dk. Mwakyembe na DCI Manumba

Kama vile mtu ambaye amekerwa na namna Jeshi la Polisi, kupitia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, Dk. Mwakyembe Februari 18, wiki iliyopita, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kujibu kile kilichoelezwa na Manumba kuhusu afya yake.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, DCI alieleza bayana kwamba Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu na kwamba kinachomsumbua ni ugonjwa wa ngozi tu, maelezo ambayo yamepingwa na Dk. Mwakyembe mwenyewe akisema kinachomsumbua bado hakijawekwa bayana na jopo la madaktari bingwa wanaomtibu India.


Taarifa hiyo ya Mwakyembe ilieleza : “Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.


“Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika).

Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:


  1. Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
  2. Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza.
  3. Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!
  4. Ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.


Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe. Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi? Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru, wamekuwa wakikerwa na tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe kwa kina?


Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti/kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!


Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.


Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.