Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Thursday, March 1, 2012

Gospel Live Ndani Pasaka


Na Mwandishi Wetu
KUNDI la muziki wa Injili la Glorious Celebration Spirit of Praise 'Gospel Live' nalo limejitosa kushiriki tamasha la Pasaka linalofanyika kila mwaka kwa kuandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam.

Kundi hilo linalotamba na albamu ya Niguse, limethibitisha kushiriki tamasha hilo, hivyo kuzidi kufanya wigo wa tamasha hilo kupanuka zaidi kwa kushirikisha wasanii nguli.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema kundi la Glorious Celebration Spirit of Praise limeahidi kukonga nyoyo za mashabiki watakaohudhuria.

Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu.

Glorious hivi sasa wanatamba na albamu ya Niguse yenye nyimbo za Unaweza Yesu, Ee Roho, Juu ya Mataifa, Mawazo, Ameni Haleluya, Nafsi Yangu, Nakupenda Yesu, Usilie na Niguse uliobeba jina la albamu.

Msama alisema mbali na Glorious, waimbaji wengine waliothibitisha kushiriki mpaka sasa ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava kutoka Mkoa wa Iringa.

"Tunaboresha mambo mengi kuliko miaka iliyopita, waimbaji mwaka huu watakuwa wachache kiasi wakiwamo wa kutoka mataifa mengine ya Afrika... hiyo yote tumefanya ili kukidhi matakwa ya wapenzi wa muziki wa injili.

"Mbali na Tanzania, pia tutakuwa na waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika tamasha hilo la nyimbo za injili za kumsifu Mungu.

"Waimbaji wengi maarufu wa muziki wa injili watakuwepo, tumejipanga vizuri kuhakiksha tamasha hili linakuwa gumzo kila mahali.

"Wapendwa wajiandae kushiriki kwa wingi kwani watashiba kiroho kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wenye hamasa ya kiroho," alisema Msama.

Msama alisema lengo la kuwajumuisha wasanii hao ni kutaka kulifanya tamasha hilo kuwa tofauti na miaka mingine.

Alisema tamasha hilo litakuwa na kiingilio cha chini zaidi (kitatangazwa wiki ijayo), ili kila mmoja ahudhurie na kupata baraka kutoka kwa waimbaji hao wanaomsifu Mungu.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.