UTEUZI wa wakuu wa wilaya na wale wa mikoa mitatu mipya unaotarajiwa kufanywa wakati wowote na Rais* Jakaya Kikwete, umezua tafrani kubwa katika baadhi ya wilaya na mikoa baada ya kuvuma kwa taarifa kwamba miongoni mwa wateuliwa hao ni wabunge wa zamani waliokataliwa na wananchi katika kura za maoni kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Taarifa za kuaminika zilizolifikia Tanzania Daima zimesema kuwa mmoja wa watu wanaotajwa kuwa watateuliwa kushika nafasi ya ukuu wa mkoa, kati ya ile mitatu mipya, tayari ameanza kupita mitaani akitamba na kuanza maandalizi ya sherehe ya kujipongeza.

‘Mteuliwa’ huyo aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo moja lililoko katika moja ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambaye inadaiwa anapigiwa chapuo kwa kiwango kikubwa na kigogo mmoja wa Ikulu ambaye wana uhusiano wa kirafiki wa siku nyingi.

Kigogo huyo wa Ikulu (jina linahifadhiwa) anadaiwa kutumia wadhifa wake kupenyeza jina la mbunge huyo wa zamani ambaye alianguka vibaya katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi na tayari ameanza tambo dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa mahasimu wake walioongoza mapambano yaliyomwangusha katika uchaguzi mkuu uliopita.

Habari zaidi zimesema kuwa mbunge huyo wa zamani amekuwa akipita katika baadhi ya wilaya za mkoa mpya wa Njombe akiwataarifu rafiki zake juu ya kuteuliwa kwake kushika nafasi ya ukuu wa mkoa huo na kwamba uteuzi huo umesimamiwa kikamilifu na kigogo huyo wa Ikulu.

Hata hivyo, kuvuja kwa siri hiyo kumewachefua wananchi wengi wa mkoa huo mpya na wameliambia Tanzania Daima kuwa hawako tayari kumpokea mbunge huyo wa zamani kama mkuu wao wa mkoa ikiwa taarifa hizo ni za kweli.

Baadhi ya wananchi wameliambia gazeti hili kuwa mbunge huyo anayeandaliwa kushika nafasi ya ukuu wa mkoa wa Njombe, hafai kwa kuwa ni mtu wa visasi na hivyo ataacha kufanya kazi za kuendeleza mkoa wao mpya, badala yake ataleta malumbano ya kisiasa pasipo na sababu za msingi.

Wananchi hao pamoja na kumpongeza Rais Kikwete kwa kuwapatia mkoa mpya, walimtaka asikubali kupotoshwa na msaidizi wake huyo na kukubali kuwateua watu waliokataliwa na wananchi kuwa viongozi wao.

“Kitendo cha Rais* Kikwete* kuwateua** wabunge* waliokataliwa na* wana* CCM katika* kura za maoni* kuwa wakuu* wa mikoa mipya* kutaleta matatizo makubwa…ni vema aangalie hili kwa makini,” alisema mkazi mwingine wa Ludewa.

Baadhi ya watu wanaotajwa kuwa wakuu wa mikoa mipya ni pamoja na aliyewahi kuwa waziri mwandamizi katika serikali tatu zilizopita, wabunge wawili kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mkuu mmoja wa wilaya moja mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi Philimon Luhanjo alikataa kutoa kauli yoyote kuhusiana na madai hayo, kwa maelezo kuwa hawezi kuzungumza jambo lolote mara baada ya kutajiwa jina la mwandishi na sababu za kutafutwa kwake.

“Ni nani mwenzangu…. hapana kwa sasa sina utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa magazeti; tafadhali nakushuru,” alisema Luhanjo na kukata simu.

Rais* Kikwete* anatarajiwa kutangaza majina ya wakuu* wa wilaya* na mikoa mipya iliyoongezwa hivi karibuni ya Njombe, Katavi, Geita na Simiyu.

source: tanzania daima