Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Wednesday, December 7, 2011

Mzee Mwanakijiji Azungumzia Kauli Za Cameroon,Ushoga Na Mwitiko Wa Tanzania


Sijui ni kwanini watu wanashindwa kutoa jibu jepesi kabisa kwa Uingereza na Marekani kuwa katika Tanzania mashoga wanazo haki zote ambazo Watanzania wengine wanazo. Tena hakuna nchi ambayo ina uvumilivu sana wa mashoga katika Afrika kama Tanzania kwa sababu tayari katiba yetu imewawekea ulinzi kama ulivyo kwa Watanzania wengine. Kwamba 'kila mtu ana haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake". Na hii "kila mtu" inajumlisha watu wa dini tofauti, makabila tofauti, rangi tofauti naam hata mwelekeo wa jinsia tofauti.

Shoga wa Tanzania anazo haki zile zile ambazo anazo mtu mwingine:
a. Ana haki ya kupiga kura
b. Ana haki ya kuishi
c. Ana haki ya kufanya kazi (wengine wameshika hata nafasi za juu tu nchini)
d. Ana haki ya kuishi popote (shoga halazimishwi na jamii kuishi mahali asipotaka yeye)
e. Ana haki ya kupata elimu (wapo wanasoma na wamesoma kwenye shule na vyuo vyetu)
f. Ana haki ya kusafiri ndani na nje ya nchi
f. Ana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yake (na wametoa hata kama yanawaudhi wengine - hatujaenda kuwafunga watu kwa kutoa maoni ya kutetea ushoga)n.k
Kwa hiyo - maelezo ya Cameron na Obama hayahusu Tanzania na sioni sababu kwanini Watanzania wanashtuka sana au kukereka. Jibu letu ni jepesi - mashoga wanazo haki zile zile za binadamu ambazo wananchi wengine wanazo na hakuna sababu ya kutengeneza kundi jingine la haki nje ya zile ambazo kila Mtanzania anazo.
Kuondoa ushoga kama kosa la kihalifu (decriminalization of homosexuality)
Sasa wanapozungumzia "haki za mashoga" wakati mwingine wanaaminisha kuwa tuondoe kwenye sheria zetu ushoga kama kosa (a criminal offense). Sasa hili siyo jambo la Marekani au UK kwani masuala ya makosa yanaamuliwa na jamii husika na kwa hoja walizonazo. Japo sheria ipo Tanzania haitekelezi sheria hiyo na kuanza kwenda kila nyumba na chumba na kuwafunga watu ati kwa vile wameonekana wameshikana mikono au wameingia chumba kimoja. Hivi kweli kuna mtu anafikiria tunaweza kuzitekeleza hizo sheria kwa kila mji, mkoa, nyumba na mitaa? Huo uwezo uko wapi? Halafu kati ya matatizo yetu yote ambayo tunayo leo kama taifa hili la kukamata mashoga mbona halipo? Hatujasikia watu wanaenda na viboko au kuwacharaza watu kwa vile ni mashoga. Watanzania wamekuwa wavumilivu mno na wengi wamekubali kuwa hilo ni suala la mtu binafsi tena mtu mzima na Katiba inawalinda watu hao pale inaposema kuwa kila mtu ana haki ya kulindwa faradha yake.
Vinginevyo, itabidi tuunde kikosi maalumu cha Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa au hata Magereza ili kufuatilia vitendo vya ushoga (Anti-Homosexuality Police Squad). Sasa kama suala ni kuifuta sheria kwa vile haitekelezeki au kuibadilisha ili ishughulikia makosa ya sodomy, molestation n.k (ambayo tayari yako chini ya SOSPA 1998 as ammended) basi ifanyike hivyo.
Ukweli ulio wazi ni kuwa anti-homosexuality laws are outdated and unforceable. Zipo sheria lakini hatuwezi kuzitekeleza au kuzisimamia na labda sisi wenyewe wananchi kama kweli tunakereka sana na ushoga kuliko mambo mengine tuwasisitize polisi wakusanye kodi zaidi ili waanze kuwa na vikosi vya kuangalia vitendo vya ushoga kwenye mahoteli.
Vitendo vya ushoga ni zaidi ya vile vya watu wa jinsia moja
Wengi ambao wanakereka na vitendo vya ushoga na kuona ni vya kuchukuliwa hatua hawajui kuwa sheria hiyo hiyo inakataza vitendo vya mwanamme kumuingilia mwanamke kinyume na maumbile (a.k.a tigo). Je, tuko tayari kuona na wanaume na wanawake wanaufanyiana hivyo -hata kwenye ndoa- wanafikishwa mahakamani kwa kuvunja sheria. Tutawatambuaje na kuwafuatilia vipi?
Wengine wanafikiria kwa mfano ushoga ni kwa wanaume ni yule anayefanyiwa (*******) na yule anayefanya (basha) siyo shoga. Kumbe wote wawili ni mashoga (homosexuals) kwani wanavutiwa na watu wa jinsia yao whichi is the essence of what homosexuality is. Maana wengine wanapozungumzia mashoga wanawafikiria wale wanaume ambao wanaonekana kama wanawake au wanajirembesha kama wanawake lakini hawawafikirii mabasha. Je, polisi na vyombo vyetu vya sheria vifuatilie vipi hapa?

Ndoa za mashoga


Hata hivyo tatizo kubwa ambalo linagongana na watu wengi na kwa haki kabisa ni suala la ndoa. Kila jamii tangu kale kabisa zimetambua kuwa ndoa ni mahusiano ya mwanamme na mwanamke. Japo katika historia nyingi na jamii za kale kumekuwepo na mashoga lakini hakukuwa na ndoa za mashoga. Wagiriki wa kale walikuwa na haya mambo lakini hawakuwa na ndoa za mashoga. Na kutokana hivyo tangu kuumbwa mwanadamu ndoa imekuwa ni taasisi takatifu ambayo inahusisha wanaume na wanawake.
Ni kutokana na hilo hata Marekani na Uingereza hakuna kitu kama ndoa ya mashoga na hata pale walipojiundia kitu chao cha kiserekikali kuwa ni "ndoa" ukweli ni kuwa taasisi za kidini na jamii kwa ujumla hawakubali kitu hicho. Ndio maana Marekani kwa mfano wamepitisha sheria ya Defence of Marriage Act (DOMA) ya 1996 ambayo ilipitishwa wakati wa Bill Clinton. Sheria hiyo inatambua kuwa ndoa ni muungano kati ya mume na mke. Sasa leo kwanini watu wafikirie kuwa Marekani inaweza kutulazimisha tuvunje mfumo wetu wa maisha kwa sababu ya misaada? Kwanini wao wenyewe wasifute kwanza sheria yao na kutambua Ndoa ya wake wengi kama sisi tunavyofanya?
Tutofautishe "ndoa za mashoga" na 'haki za mashoga'
Mojawapo ya matatizo ambayo Uingereza na Marekani yameleta katika hili la kuhusisha misaada na masuala ya mashoga ni kuchanganya mambo haya mawili. Hakuna kati yao aliyesema wanataka nchi zinazopokea misaada zitambue "ndoa za mashoga" kama wengi walivyotafsiri au kuripotiwa. Hawa walikuwa wanazungumzia "haki za mashoga" kwa maana ya kwamba kuna jamii au nchi ambazo zinatumia muda wao mwingi na raslimali zao kuwanyanyasa na kuwatesa mashoga. Napendekeza kwamba Tanzania siyo nchi mojawapo ya hizo.
Hatuwatesi mashoga
Hatuwafungi
Hatuwakatazi au kuwanyima haki zao ambazo ni haki za kila Mtanzania
Na wakifanya uhalifu wanaadhibiwa kama Mtanzania mwingine. Hakuna upendeleo wa mashoga. Ushoga usiwe kisingizio cha mtu kufanya uhalifu halafu akikamatwa adai kuwa ati kakamatwa kwa vile yeye shoga. Jamii yetu ina sababu ya kulinda watoto na vinana wake katika kuwapa malezi ya kifamilia na huu ni wajibu ambao hatuhitaji Marekani, China, Uingereza au Iran kutuambia. Binafsi napuuzia hoja za Cameron na Obama kwani hazihusu Tanzania labda nchi nyingine na nina uhakika hat aakiulizwa balozi wa Marekani au Uingereza atakiri tu kuwa yote wanayoyazungumzia ni nchi zile ambazo hazina haki za binadamu.
Binafsi ningependa kusikia Uingereza na Marekani wanaunganisha haki za kisiasa (political and civil rights) na misaada. Kwa sababu hapo wataigusa na Tanzania hili la "haki za mashoga" halituhusu. Maana kama kuna haki zinavunjwa sana Tanzania ni hizo.

Na Mzee Mwanakijiji kutoka Jamiiforums

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.