Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, December 3, 2011

Mchakato huu wa Katiba ni haramu – chini ya ibara ya 98

NAOMBA nipendekeze kuwa mchakato mzima ambao umependekezwa na Chama cha Mapinduzi na kupitishwa na sehemu kubwa ya wabunge ili kusimamia mchakato wa kuelekea Katiba Mpya hauna msingi wa kikatiba, unahamisha madaraka kutoka kwa wananchi na unapakana na uhaini wa wazi. Ninaamini pasipo chembe ya shaka kuwa sheria ambayo imepitishwa na hatimaye kusainiwa na Rais Kikwete ni kinyume cha Katiba ya sasa na unastahili kupingwa na kukataliwa.
Ninafahamu viongozi wa CHADEMA na labda “wadau” wengine wanaamini kabisa kuwa mchakato huu tayari ni halali na hivyo, hakuna jinsi isipokuwa kudandia treni kwani limeshatoka stesheni. Hili ni kweli lakini dhamira ya mwanadamu haiwezi kuvutwa kwa mnyororo. Kwa upande wangu ninaamini kabisa mchakato ulivyo sasa na hasa kama Rais ataridhia na kuufanya sheria ni mchakato usio halali.
Kauli ya Kikwete
Wakati Rais Kikwete anazungumza na wazee wa CCM kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam siku chache tu zilizopita alisema hivi; Mimi na wenzangu serikalini tumefanya yote ambayo Katiba ya nchi na sheria vinaruhusu.” Alikuwa anaelezea kuhalalisha uamuzi wa kuandika Katiba Mpya. Kwamba, mchakato aliouanzisha na sasa kutungiwa sheria uko ndani ya Katiba ya nchi ya sasa na hivyo ni halali. Pendekezo langu ndugu zangu ni kuwa kinachofanywa sasa na Serikali chini ya Rais Kikwete juu ya suala hili la Katiba hakina uhalali wa Katiba ya sasa jinsi ilivyo na hivyo madai kuwa yeye na “wenzake” wamefanya kile ambacho Katiba ya nchi na Sheria “vinaruhusu” hayana msingi wowote. Kuna hoja kadhaa ya kuliangalia hili.
Mosi; Katiba ya sasa ni nzuri
Katika hotuba yake ile Rais Kikwete alisema maneno ambayo yalikuwa yanapingana na lengo zima la Katiba Mpya. Alisema; “Nilifafanua siku ile kwamba tunataka kufanya hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni mbaya, la hasha.
Nilieleza kwamba Katiba yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu. Tuna nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja na watu wake kuwa wa rangi, makabila, dini na itikadi mbalimbali za kisiasa. Tunayo nchi ambayo imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.”
Sasa mtu mwenye hekima lazima ahoji kuwa kama katiba ya sasa si mbovu kwa nini tunataka mpya? Kama Katiba ya sasa inakidhi mahitaji yetu ya kuleta amani, umoja na utulivu na kupiga hatua ya haraka ya maendeleo kwa nini tunahitaji Katiba Mpya?
Tukimsoma vizuri Rais ni kuwa tunahitaji Katiba Mpya kwa sababu tumechoka na katiba ya sasa- si kwa sababu ni mbaya ‘la hasha’ bali ni kwa sababu ni ya zamani. Hii ni sababu mbaya sana ya kuamua kuandika Katiba Mpya. Wamarekani kwa miaka karibu 300 wanayo Katiba ile ile wanaifanyia marekebisho tu.
Hivyo, kama Katiba ya sasa ni nzuri basi hakuna haja ya Katiba Mpya isipokuwa kufanyia marekebisho machache tu ya kuiboresha ambayo hayahitaji mchakato mwingine nje ya ule uliopo Kikatiba. Tungeweza kabisa kufanya marekebisho ya hapa na pale na Katiba yetu ikaendelea kututumikia kwa miaka mingine hamsini. Ukweli ni kuwa tunataka Katiba Mpya kwa sababu ya sasa ni mbaya!
Pili; Katiba ya sasa haitoi madaraka kuandikwa Katiba Mpya
Hii ni hoja kubwa zaidi ambayo ningependa niangalie japo kwa undani kidogo. Kwamba Katiba ya sasa ni halali haina shaka; na kwamba ina upungufu hilo halina shaka. Kuwa na upungufu hakuondoi uhalali wa Katiba. Ni kutokana na hili, Katiba ya Sasa ikaweka Ibara ya 98.
Ibara hii inafuatia Ibara ya 97 ambayo imeweka utaratibu wa Kikatiba wa kubadilisha sheria mbalimbali. Ibara ya 98 inahusiana na “Utaratibu wa kubadilisha Katiba hii na baadhi ya sheria.” Kifungu hicho cha Katiba kinasema hivi:
98.-(1) Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata Kanuni zifuatazo:-
(a) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote;
(b) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya Sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni wa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.
(2) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya sheria maana yake ifahamike kuwa ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.
Naomba tuangalie mambo kadhaa kutoka Ibara ya 98 na ni kwa nini sheria iliyopitishwa inapingana moja kwa moja na Ibara hii na hivyo, kwa maoni yangu ni sheria ambayo ni kinyume cha Katiba na ambayo haipaswi kuitii (tunayo haki ya kutii sheria halali tu na ambayo haipingani na haki za binadamu).
Bunge lina madaraka ya kufanyia marekebisho ya masharti ya Katiba “hii”.  Kifungu kinafunguliwa kwa kusema kitu ambacho labda wengine hawajakifikiria sana kuwa “Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii”
Kwa maneno mengine, Bunge lina uwezo wa kufanyia marekebisho masharti ya Katiba hii peke yake, halina madaraka ya kuifuta Katiba ya sasa na kuandika Katiba nyingine bila kufanyia marekebisho katiba ya sasa kwanza.  Sheria iliyopendekezwa na sasa kukubaliwa na Rais Kikwete inatoa madaraka kwake (Rais) na wabunge kushiriki mchakato wa kuifuta Katiba ya sasa na kuleta Katiba Mpya – madaraka ambayo hawana.
Ikumbukwe kwamba wabunge wote na Rais wote wameapa “kuilinda, kuitetea na kuihifadhi” Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Sasa iweje watu walioapa kulinda, kuitetea na kuihifadhi Katiba hii ya sasa wajipe madaraka ya kuifuta na kuamua kuleta nyingine madaraka ambayo hawana?
Ibara ya 98 inatoa madaraka kwa wabunge kubadilisha masharti ya Katiba ya sasa na hili limo ndani ya uwezo wao lakini kuna mtu anaweza akamuuliza Kikwete, Spika au msomi yeyote wa sheria kuwa Katiba ya sasa inatoa wapi madaraka kwa Bunge au Rais kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya?
Maana Rais amesema anafuata Katiba ya sasa – ni wapi ambapo yeye amepewa madaraka ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya? Hakuna na hivyo mchakato mzima si halali.
Masharti ya kupitisha mabadiliko ya Katiba ya sasa ni mazito mno kulinganisha na masharti yanayopendekezwa ya kupitisha Katiba Mpya. Ibara hii ya 98 inaweka kiwango cha wabunge kukubaliana kupitisha Katiba kuwa cha juu sana. Ukisoma Ibara hiyo utaona kuwa mabadiliko ya sharti lolote la Katiba ya sasa hayawezi kupita isipokuwa yameungwa mkono na idadi ya wabunge “isiopungua theluthi mbili ya wabunge wote”. Kwa maneno mengine, Katiba ya sasa haiwezi kubadilishwa kwa asilimia 50 ya wabunge ila lazima iwe ni zaidi ya asilimia 66.
Cha kushangaza hata hivyo, CCM na Rais Kikwete wanataka kupitisha sheria (wameshaipitisha) ya kusema kwamba Katiba Mpya inaweza kupitishwa na asilimia 50 ya wapiga kura. Fikiria kidogo – kama masharti ya sasa ya Katiba hii hayawezi kupitishwa bila kushawishi zaidi ya asilimia 66 ya wabunge iweje kwenye Katiba mpya kiwango cha kuipitisha ni asilimia 50 ya wapiga kura?
Ikumbukwe siyo asilimia 50 ya Watanzania bali asilimia 50 ya wapiga kura wanaweza kuamua kupitisha Katiba Mpya. Kama tukichukulia tu kuwa upigaji kura ya maoni unakuwa kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi uliopita ina maana asilimia 61 ya wapiga kura (waliomchagua Kikwete) ndio wanapitisha Katiba Mpya. Japo namba hiyo inaonekana ni kubwa ukweli ni kuwa ni watu kama milioni tano tu waliomchagua – sasa kweli tunataka Katiba Mpya ya Tanzania ipitishwe na watu milioni tano  hivi au hata chini ya hapo alimradi wanafikisha asilimia 50?
Je, hii haina maana ya kwamba CCM na Serikali haihitaji kushawishi Watanzania wengi zaidi kukubali Katiba Mpya isipokuwa inahitaji kushawishi – kwa mfano wanachama wake kupigia kura?
Bila kufunganisha asilimia ya upigaji kura na idadi ya watakaopiga kura mchakato huu utatuletea katiba ya watu wachache zaidi. Fikiria kwa mfano mchakato unasema ili Katiba Mpya iwe halali ni lazima asilimia 70 wa wapiga kura wajitokeze kupiga kura na kati yao asilimia zaidi ya 65 (pande zote za Muungano) ndio itafanya Katiba iwe halali.
Hicho ni kiwango cha juu sana. Hii ina maana kama waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 20 basi ili mchakato uwe halali milioni 14 kati yao wajitokeze kupiga kura ya maoni na kati yao ili Katiba iwe halali milioni 9.6 wapige kura ya ndio! Hii ina maana mchakato lazima uwe wenye kuhitaji kushirikisha na ridhaa ya wananchi wengi zaidi.
Kutokana na hayo mawili tunaweza kuona mambo yaliyo dhahiri. Kwanza mchakato ni kinyume cha Katiba – kwamba bila kubadilisha Katiba ya sasa mchakato wote unaofuatia na kutetewa unakosa uhalali – mtu mmoja kasema mahali fulani kuwa ‘ni uhaini’ japo miye naamini unakaribiana kabisa na uhaini. Viongozi walioapa kulinda Katiba ya sasa wamejipa madaraka ya kuifuta Katiba hii na kuleta nyingine – madaraka ambayo hawana.
Mchakato huu ukiendelea jinsi ulivyo bila kufanyiwa marekebisho husika (kwenye Katiba ya sasa na kwenye Sheria inayopendekezwa) utasababisha Watanzania kushindwa kushiriki kuandika Katiba yao kihalali. Kama watu wanalalamika kuwa Watanzania hawajawahi kushiriki kuandika Katiba yao mchakato huu hauondoi tatizo hilo kwani Katiba itakuwa imeandikwa kwa matakwa ya Rais, kwa mfumo usio halali na matokeo yake kuamuliwa na watu wachache zaidi. Kwa kifupi ni mchakato usio halali.
Mapendekezo yangu
Kwanza, mchakato usitishwe na mabadiliko ya Katiba ya sasa yafanyike kwanza. Ni lazima tuweke kwenye Katiba ya sasa namna ya kuhalalisha uandikaji wa Katiba Mpya ya nchi yetu. Sasa hivi tunaruhusiwa kufanyia mabadiliko tu Katiba hii ya 1977 chini ya Ibara ya 98. Ina maana ipo haja aidha ya kuongeza Ibara ya 98B, itakayoelezea ni wakati gani nchi inaweza kuangalia uwezekano wa kuandika Katiba Mpya.
Yakishafanyika mabadiliko hayo ndiyo sheria iletwe bungeni ya kusimamia mchakato wa Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 97. Sheria hiyo ni lazima iendane na kukubaliana na matakwa ya Ibara ya 98.
Kama Serikali haitatekeleza mapendekezo haya, basi ni wajibu wa kila raia mwenye dhamiri safi kuukataa na kuupinga mchakato mzima hata kama unapigiwa chapuo kuwa ni ‘halali’. Mchakato huu hauna uhalali wa Kikatiba na hauna uhalali wa kimantiki ni kunyang’anya wananchi madaraka (usurpation of power) uliofanywa na Ikulu na hivyo kulazimisha watu wote kukubaliana nao.
Kama vyama vyote vya siasa vilivyopo sasa vinakubali kushiriki katika mchakato huu haramu ipo haja ya kuanzisha chama kingine cha kisiasa ambacho kitasimamia kanuni za msingi na ambacho kitatuahidi kufuata kanuni sahihi za “hakimiya ya wananchi” yaani sovereignty of the people- ili kiweze kutuongoza kufikia Katiba Mpya ambayo itatoka, itaandikwa, kusimamiwa na kupitishwa na wananchi wengi kuliko mchakato huu unavyopendekeza.
Ndugu zangu, kuna vitu vya kubambikizwa na Katiba si kimojawapo. Kama chama hicho cha siasa hakijaundwa basi kuunga mkono chama ambacho kitakataa kabisa kuutambua mchakato huu kwa sababu nilizozianisha hapa.
Kama hukubali niandikie:
lulawanzela@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.