Mtakumbuka
kwamba mwezi Januari 2013 nilitoa taarifa kwa umma ya kueleza kuwa
niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi wa Sheria ya Baraza la
Vijana la Taifa na kuomba hatua za ziada toka ofisi ya Bunge kwa
kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Toka
wakati huo muswada huo mpaka sasa Mei 2013 haujachapwa katika gazeti
la Serikali na nimepokea barua toka kwa ofisi ya Bunge kwamba wamepokea
ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa muswada huo hauwezi
kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya
ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi.
Sababu
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri huo ni kuwa muswada
unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha
kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya
kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na
kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.
Kwa
maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo bila
kuzingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili kinataja vyanzo
mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko
zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya
Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Ibara
ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka kuwa “fedha ambazo hazitawekwa
kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile zote ambazo zimetajwa na
sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe kwenye mfuko
mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Hivyo,
ni maoni yangu kuwa ibara hiyo ya Katiba ya Nchi inaweza kutumika
kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho
kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya
mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba
jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe
limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”
Kifungu
cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja na
muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya
fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko
mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote
isipokuwa kupunguza”.
Toka
Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 itamke kwamba
Serikali itawezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na suala hilo
kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; miaka takribani 17 imepita
marais wote wa awamu husika na mawaziri wenye dhamana hawajawasilisha
bungeni muswada huo hali ambayo imenifanya niandae muswada binafsi
kuwezesha baraza kuundwa.
Muswada
wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa 2013 niliouwasilisha kwa maoni
yangu hauna lengo la kuagiza malipo au matumizi ya fedha yafanywe
kutokana na Mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali au Mfuko mwingine wowote
kwa mujibu wa ibara ya 99 bali unalenga kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 135.
Hata
hivyo, kwa kuwa muswada huu unahusu mustakabali wa vijana na ni suala
la kitaifa kupitia waraka huu naomba kupata maoni yenu kuhusu suala
hili, mapendekezo ya marekebisho yanayohitajika kufanyika na hatua
zinazopaswa kuchukuliwa.
Maoni, mapendekezo na hatua hizo zitumwe kupitia mbungeubungo@gmail.com au kwa Afisa wa Ofisi ya Mbunge Ubungo Gaston Garubimbi (0715825025) kabla ya tarehe 24 Mei 2013.
Nakala ya rasimu ya muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 inapatikana katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa ajili ya rejea.
Aidha,
nawaalika kushiriki mikutano ya kupokea maoni kupitia mtandao huo
tarehe 20 mpaka 23 Mei 2013 saa 9 alasiri mpaka 10 Jioni ambayo
nitashiriki na kutoa maelezo ya zaidi kwa kadiri itakavyohitajika.
Natarajia
kupokea maoni ya vijana na wananchi wengine bila kujali tofauti
mbalimbali kwa kuwa madai ya kutaka kuundwe Baraza la Vijana la Taifa
yamekuwa yakitolewa na vijana, asasi na taasisi kwa muda mrefu.
Vyama
vya siasa kwa kuzingatia matakwa hayo viliahidi kutekeleza azma hiyo
kwa mfano Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010-2015 kipengele 6.4.1 (viii)
ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai
wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya
CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo
limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
Kwa
upande mwingine, Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 iliahidi katika
kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali
za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishaji wa Baraza la
Vijana”.
Mwaka
2011 niliihoji Serikali bungeni ni lini itakamilisha uanzishwaji wa
baraza hilo na ikaahidi kwamba kazi hiyo itakamilishwa katika mwaka wa
fedha 2011/2012 hata hivyo sasa ni Mei 2013 Serikali haijakamilisha.
Hivyo
vijana, wabunge na wananchi kwa ujumla ni muhimu kuboresha muswada huo
na uwasilishwe bungeni kuwezesha baraza la vijana na mfuko wa maendeleo
vijana kuanzishwa; maslahi ya umma kwanza.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
19 Mei 2013
Dodoma
Muswada wa Baraza la Vijana 2013-Rasimu ya Kwanza; pakua hapa (download here):
https://docs.google.com/file/
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.