Mch Mtikila amekusudia kutoa tamko leo saa tano asubuhi, Hotel
Traventine la kumtaka Rais Kikwete atangaze Kusitishwa kwa mradi wa
Kusafirisha gas Kutoka Mtwara kuja Dar Mara moja ili kudumisha amani
Mtwara!!!.Asipofanya hivyo ipo hatari mapinduzi ya utawala wake yaka
anzia Mtwara.
Update: Mtikila ameshatoa Tamko:
TAARIFA YA DEMOCRATIC PARTY (DP) KUHUSU
GESI NA MASLAHI YA MTWARA CORRIDOR
DP tunatoa
tahadhari kwamba hali inayoendelea kuwa mbaya huko Kusini mwa Nchi yetu,
inazidishwa na ukosefu mkubwa wa uzalendo na hekima katika utawala wa
juu wa CCM, kiasi cha kuzidi kuumwagia gesi moto unaowaka badala ya
kutumia historia ya tatizo lenyewe ambayo peke yake ndiyo inayoweza
kuwapa busara ya zimamoto! Tunapenda
ieleweke kuwa madai kwamba umeme wa gesi hiyo ufuliwe kule kule Kusini
yanatoka katika uchungu wa wananchi wote wa Kusini mwa Tanganyika yaani Mtwara Corridor, uchungu wa kudhulumiwa, kudhalilishwa na kusahauliwa kabisa kimaendeleo tangu tulipotapata uhuru mpaka leo. Serikali
ndiyo chombo hasa cha kuzungushia gurudumu la maendeleo, ambalo
lilielekezwa Kaskazini tu mpaka Kusini kukabaki pori na giza nene, kiasi
kwamba watumishi wa umma walipokuwa wanapangiwa kufanya kazi Kusini,
mara nyingi ikiwa kama adhabu, waliamua kuacha kazi. Kupuuza upande
mmoja wa nchi kimaendeleo huwa ni bomu la hatari litakaloteketeza hapo
baadaye, kama inavyokuwa hivi leo Wananchi wa Mtwara Corridor
wanafahamu kwamba sumaku ya wawekezaji wa miradi mikubwa ya kuwaletea
maendeleo ni nishati na miundombinu, lakini watawala wa CCM
waliwanyang’anya Reli ya Kusini kwa uharamia wa kung’oa mpaka mataruma
na kufutilia mbali hata na tuta lenyewe! Wananchi
wa Kusini ni binadamu wanaoumia kwamba hata barabara ya kuwaunganisha
na dunia nyingine haijaisha mpaka leo, lakini wanayaona makufuru ya
ufujaji wa kutisha wa serikali ya CCM hiyo hiyo wa mabarabara ya Jijini
Dar es Salaam sasa kukwanguliwa lami nzuri kabisa ya mabilioni ya fedha,
ambayo ingeishi zaidi ya miaka saba mingine! Serikali
ndiyo yenye jukumu la kuweka misingi yote ya uchumi wa nchi, kwa ajili
ya maendeleo ya Taifa na maisha bora ya wananchi wenyewe, lakini mbali
ya ule uharamia wa kuwang’olea ile reli, fungu la uboreshaji wa Bandari
ya Mtwara ambayo ndiyo yenye kina kikubwa zaidi cha asili kinachofaa
zaidi kuliko hata bandari ya Dar es Salaam, sasa ni fungu la kujengea
bandari ya Bagamoyo nyumbani kwa Kikwete, ambapo ni hatua kadhaa tu
jirani ya Dar es Salaam! Zao
la pamba ambalo utawala wa mkoloni ulilijengea msingi imara kwa ajili
ya uchumi wa nchi na wananchi wake, lilishamiri vizuri zaidi Kusini kama
ulivyoshamiri hata mkonge. Lakini kwa kutowathamini watu wa Kusini na
kutojali kabisa hatima yao kiuchumi na kimaisha, utawala wa CCM
uliyanyima mazao hayo kipaumbele kule na hata ule msukumo unaopasa,
wakati kule Kaskazini mwa nchi hiyo hiyo umeme ulisha sambazwa mpaka
migombani!
Zao la korosho lililobaki
angalau katika uwezo wao ulio duni, limekuwa kama mnyororo wa utumwa,
kwa sababu wakivuna hawapati kitu bali kupunjwa kabisa bei kama
zikinunuliwa. Ni zao linalotajirisha sana ma--------- kwa kuwakondesha
vibaya sana walalahoi wa Kusini.
KUHUJUMIWA KWA MAONO YA SHUJAA OSCAR KAMBONA
Watu
wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba shujaa Oscar Kambona ndiye hasa
aliyefanikiwa kuiombea Nchi yetu msaada wa China wa Reli ya Uhuru, na
uwezo wake wa kisiasa na hasa baada ya kung’ara katika ukombozi wa
Afrika na uhusiano wake binafsi na Chou en Lai ulivyotusaidia. Tunajua
kwamba kwa ajili ya hazina za Taifa letu za mafuta na gesi kule Kusini,
pamoja na rutuba isiyo kawaida kwa ajili ya kilimo, pamoja na raslimali
za madini ya thamani njia yote, achilia mbali wanyamapori Selous, na
chuma cha Liganga na mkaa wa mawe Mchuchuma, reli hiyo ilikuwa ianzie
Bandari ya Mtwara iliyopangiliwa pia uboreshwaji wa nguvu, na ilikuwa
iende mpaka Ziwa Nyasa baada ya kona ile ya kwenda Liganga na Mchuchuma
hadi Rukwa kwenye shaba. Hauwezi
kusahaulika ushuhuda kwamba baada ya shujaa Kambona kuelezea baraza la
mawaziri mafanikio haya ya safari yake China, na hasa Bandari ya Mtwara
na reli ya uhuru wetu wa kiuchumi, alitukanwa na mkuu wake kwamba ni
mkabila sana, kwa ‘kosa’ la kutaka hiyo miundombinu ya bandari na reli
iwe Kusini! Mzalendo
Oscar Kambona alijitetea kwa hekima ya rohoni kiasi cha kuwatoa machozi
baadhi ya wenzake kwamba, “Mimi si mkabila wala sina kosa, kama kuna
mwenye makosa basi ni Mwenyezi Mungu”. Alipotakiwa aeleze ana maana gani
alisema, ‘Kwa sababu Mungu angetuwekea kule Kilimanjaro au Musoma hizi
hazina za gesi, mafuta, madini ya thamani na Selous ya wanyamapori,
chuma na mkaa wa mawe na shaba reli ingepita, lakini sasa alikosea akaweka Kusini. Hakuna
mwehu wa kubisha kwamba maono haya ya hayati Oscar Kambona yalikuwa ya
uzalendo wa hali ya juu kwa ajili si ya watu wa Kusini, bali kwa muujiza
wa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa la wana wa Tanganyika kuwa katika kilele cha Afrika na hata dunia. Hatushangai
kwamba ingawa shujaa Oscar Kambona ndiye aliyeanzisha Kamati ya
Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kwa maono yake binafsi
ambayo Nyerere ilibidi ayaafiki, Kambona akayauza kwa rafiki yake mpenzi
Ahmed Sekou Toure aliyempa cheki tupu ya kwanza, wakamhusisha shujaa
Kwame Nkurumah aliyetoa cheki ya pili, na walipomshirikisha Mfalme Haile
Selasie naye akatoa cheki ya tatu, shujaa Oscar Kambona akaupambisha
moto wa ukombozi wa Afrika, mpaka wivu ulipompiga vita kali hadi
akaikimbia Nchi yake. Ni
dhahiri kwamba watu wa Kusini ya Tanganyika au Mtwara Corridor walikuwa
na sababu ya kumpenda na kumheshimu hayati Oscar Kambona, kwa sababu
maono yake kwa ajili ya hatima ya Taifa letu yalikuwa baraka kwao.
Lakini hakuna hata choo ya Jiji iliyoweza kuitwa jina la shujaa Oscar Kambona, licha ya sifa na heshima aliyoiletea Nchi yetu, hii ni aibu! Nyerere
alipogeuka kuwa adui mkuu wa shujaa Oscar Kambona watu wengi wa Kusini
waliteseka kwa ajili hiyo, na koroboi ya maendeleo Kusini ilionekana
kuzimika kiaina, hadi ilipoibuliwa upya na Shirika la Maendeleo la Taifa
(NDC) mikakati mipya ya maendeleo ya Kusini, kwa jina la Mtwara Corridor,
iliyofanyiwa kazi kwa dhati na mzalendo Simbakalia ambaye sasa ndiye
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Koroboi hiyo ikazimika tena alipoondolewa huyu
kutoka NDC.
UFUMBUZI WA MOTO WA HASIRA ULIOLIPUKA KUSINI
Moto
huu usipozimishwa kwa hekima ya hali ya juu, si ajabu ukaimeza mikoa
yote ya Kusini yaani Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na
hata Rukwa, tukakuta yanazaliwa mataifa mawili mpaka ukiwa Reli ya Kati!
Tumeeleza kwa kifupi
sana historia na sababu za msingi za hasira za watu wa Kusini, kwamba
wao pia ni binadamu, na kwamba lugha yao ya amani ilipuuzwa kwa miaka
yote 52 tangu nchi yetu ilipopata uhuru. Lakini tunapinga propaganda za
uwongo za watawala waliosababisha hasira hii, kwa ukweli kwamba: 1. Watu
wa Kusini hawazuii gesi isitoke kwa sababu ni nyingi sana na hazina
yetu ni ya pili duniani kwa uwingi. Wao wanataka umeme ufuliwe kule kule
kwa sababu utaleta mapinduzi ya maendeleo kule. 2. Faida
ya pili ni kwamba nyaya zitakazo zoubeba umeme kuupeleka mpaka Kenya na
Uganda tukitaka, lazima njia nzima zitakuwepo transfoma za kuusambaza
mpaka miisho yote ya nchi mpaka vitongoji vyote. Kwahiyo wananchi wa
Kusini ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 3. Wanataka
mabomba ya gesi yaanze kuisafirisha baada ya kufuliwa umeme, ili na
yenyewe pia humo njiani yachomekwe mabomba yatakayoieneza nchini kote,
kusudi iwe nishati mbadala ya Taifa kwa ajili ya kuiokoa miti yetu kwa
ajili ya vizazi vyetu vyote vijavyo. Mungu ametuzibulia hazina ya gesi
wakati nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kutokana na kuteketezwa miti yote
kwa kutumiwa kama nishati. Hawa ndio wazalendo na siyo watawala wa
CCM. 4. Ukweli
kwamba ufisadi wa kutisha umetembea katika mikakati hiyo ya kuufulia
hapa Jijini umeme wa gesi ya Kusini, hivyo kwamba kiburi cha watawala na
kutojali maslahi ya Taifa kama umeme utafuliwa kule kule Kusini, ni kwa
sababu mafisadi hawana jinsi kwavile mabilioni ya watu walishakula
sehemu kubwa, na sasa wanatafuta kulazimisha ili wapate lile fungu nono
la mwisho. Saa ya ukombozi ni sasa! Njia
pekee ya kuzimisha moto huu kule Kusini na kurejesha amani ni Rais
Jakaya Kikwete kutoa Tamko la kukubali kufuliwa umeme kule kule Kusini
kwa sababu ni kwa maslahi ya Taifa. DP tupo tayari kufanya usuluhishi
kama kutakuwepo uwazi kwa upade wa serikali, kwa ajili ya hatima ya Nchi
yetu. Rais
Jakaya Kikwete analazimika pia kutamka bayana kipaumbele kwa ubereshaji
wa Bandari kuu ya Mtwara, ikibidi hata kwa kusitisha mradi wa Bandari
ya Bagamoyo. Hii ni kwa maslahi ya Taifa letu. Rais Jakaya Kikwete
anapaswa kutamka bayana kuhusu ukamilishaji wa barabara ya Kusini.
Rais
Kikwete anakabiliwa na utanguaji wa ufisadi wote uliofanyika Mtwara
Corridor mpaka Ludewa kwenye miradi ya Chuma cha Liganga na Mkaa wa mawe
Mchuchuma. Saa ya ukombozi ni sasa! Mchungaji C. Mtikila, Mwenyekiti0713 430516
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.