by Strictly Gospel |
Baada ya kufuatilia kwa undani, na kwa upana kuhusu swala la gesi ambalo linaendelea kuwa ni mgongano au, ni mgogoro kati ya Serikali na wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda kinyerezi Dar- es –Salaam, tumebaini yafuatayo:-
1.
Hakuna Sera ya gesi ambayo husababisha kupatikana Sheria baada ya
kupelekwa Bungeni na kuidhinishwa bali kilichopo ni rasimu ya sera
ambayo haina ushirikishwaji wa mawazo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara na
Lindi, ambako vyanzo vya gesi hiyo ipo.
2.
Elimu kuhusu gesi na manufaa yake kwa wananchi haikutolewa ili kujua
haki zao kwa madhara yatokanayo na (Uvunaji) uzalishaji wa gesi hiyo, na
jinsi watakavyonufaika.
Chama
cha Mapinduzi katika Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 inatamka wazi
katika Ibara ya 63 kifungu cha H na K juu ya gesi ya Mnazibay Mtwara na
Songo songo Kilwa, Lindi kuhusu umeme wa (240 MW) Kinyerezi na (300MW)
Umeme wa Mnazi bay Mtwara……
-Vifungu hivi vinafafanua:
• Mitambo ya kuchakata gesi kujengwa Mtwara
• Ujenzi wa viwanda Mtwara ili malighafi itokanayo na gesi itumike kutengeneza mbolea, plastic vikiwemo na viwanda vya Cementi
2. Gesi ya Songo songo inafafanua wazi kuwa gesi hiyo itapelekwa Kinyerezi . Dar –es –Salaam kwa madhumuni hayo hayo.
• Kuendeleza viwanda mbali mbali
• Kuzalisha umeme (240 MW)
• Kuchakata gesi kwa kujenga mitambo
Katika
ahadi ya Rais wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati wa
Kampeni za uchaguzi katika hotuba yake ya tarehe 29/10/2010 alitamka
wazi kuwa Mkoa wa Mtwara uwe tayari kwa maendeleo makubwa ambayo
yanakuja kutokana na gesi iliyogunduliwa katika Mkoa wa Mtwara huko
Mnazi bay
Alimainisha/aliainisha
juu ya viwanda mbalimbali vitakavyojengwa hapa mkoani vya
mbolea,cement, plastic n.k na kuwataka wananchi wajiandae kupokea
maendeleo hayo kwa kujenga nyumba nzuri zenye sifa kwa ajili ya wageni.
Pia wawasomeshe watoto wao ili wawe na elimu ya juu na kupata ajira
katika Makampuni yanayokuja.
Hata
baada ya uchaguzi Rais wetu alipokuja kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa
Mtwara kwa kumchagua, alitamka tena katika hotuba yake akisisitiza ahadi
yake ya kujenga viwanda ambavyo vitaleta maendeleo kwa Mikoa ya Kusini
na kusababisha ajira kwa wana kusini, na kuagiza kwa Meya wa Manispaa
Mtwara/Mikindani kuwapa maeneo ya kujenga viwanda hivyo, kwa kile
kilichoonekana kukosa maeneo ya ujenzi huo kwa makampuni hayo. Ahadi
hizi alizozitoa kwa wananchi kwa ujumla wao wamezipokea na kuendelea
kuzifanyia kazi.
Chanzo cha Matatizo: Mara
baada ya kuonekana kile walichokitarajia wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa
kutumia gesi ya Mnazi bay kuleta maendeleo yao kuwa imeamriwa
kusafirishwa kwa bomba na kupelekwa Kinyerezi Dar –Es –Salaam ili
kuzalisha umeme na kuchakata gesi na mitambo hiyo iwe huko.(Mgeuko wa
Ilani ya Uchaguzi, na kutozingatia ahadi zake mwenyewe Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa kinyume na kauli za usemi wake mwenyewe
kwa kukitangaza kituo cha Kinyerezi kuwa ni sehemu ya mitambo ya gesi
ya Mnazi bay-Mtwara na Songosongo-Lindi na kwamba bomba hilo litachukua
miezi (18) mpaka kukamilika kwake, kwa matamshi haya ndiyo yaliyoleta
hasira na chuki kwa wananchi wa Mtwara/Lindi kwa ujumla.
Hali
hii imewafanya wananchi wa Kusini kutokuwa na Imani na Serikali na
viongozi wake wahusika na sakata hili la gesi kwa semi mbalimbali za
viongozi hawa-Mfano.
(1) Kwa hali yoyote gesi lazima itoke Mtwara (Kwa gharama yoyote ile) kwa kukubali ama kutokubali itakwenda Kinyerezi kwa bomba
(2) Kuitwa wahaini wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kuandamana
(3) Kuitwa wajinga, hawakusoma na kuwa watu wa vijiweni wasio na elimu ya gesi
(4)
Nitafanya lolote hata kama nitalaumika na Mataifa mengine lakini wapo
watakaochekea yatakayotokea na kauli zinazobadilika kila kunapokucha.
(5) Usemi wa kuigawa nchi vipande vipande
Viongozi
hawa hawajui kuwa chanzo kipo kwao wenyewe, kwa kutozingatia kuwa
wananchi hao ambao hawana elimu kama yao wanao upeo mkubwa wa kufikiri
na kutoa maamuzi kama wanavyotoa wao….
Mfano.
(1) Gesi haitoki Mtwara
(2) Tupo tayari kufa wote kwa ajili ya gesi
(3) Haiwezekan mitambo ya aina zote
-Kufua umeme
-Kuchakata gesi
-Kunufaisha viwanda vya Dar-es-Salaam kwa gesi yetu
-Mikataba ya gesi ya Mnazibay kufutwa ili kuanzisha mikataba iliyo na manufaa kwa Mkoa wa Mtwara na wananchi wake.
(4)
Kwa nini bomba la gesi kujengwa kwa muda wa miezi 18 na bara bara kwa
miaka 51 ya uhuru haimalizwi kujengwa. Je kwenye gesi kuna nini nyuma
yake.?
Hiki
ni kiini cha matatizo yote kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuandamana na
mikutano mbalimbali ya kuhamasisha kutokubali gesi kuondoka Mtwara
Nukuu za Wananchi wa Mkoa wa Mtwara/Lindi
1-Kung’olewa kwa Reli
2-Kung’olewa kwa mashine za maji Newala na kupelekwa Dodoma.
3-Kung’olewa kwa taa za kuongoza ndege uwanja wa Mtwara na kupelekwa Uwanja wa KIA Moshi
4-Kuondolewa kwa Mtwara Korido
5-Kuwekezwa
kwa bandari ya Mtwara kwa muda usiojulikana inaonyesha jinsi Serikali
na viongozi wake wanavyohujumu Mikoa ya Kusini na wananchi wake kwa
ujumla.
-Wananchi
wa Mkoa wa Mtwara na Lindi wamefikia ukomo sasa wa kutengwa
kimaendeleo, kimazingira na kutendewa uonevu wa makusudi na kilio chao
cha mwisho ni hiyo gesi ambayo kauli mbiu yao ni GESI HAITOKI MTWARA KWA BOMBA KWENDA KINYEREZI DAR-ES-SALAAM.
-Wananchi
wote wameungana juu ya kuitetea gesi kutoka Mtwara, badala yake
Serikali ifuate mikataba ya kwanza inayohusu gesi ya Mtwara pamoja na
Ilani ya uchaguzi ya CCM ifuatwe na Rais atekeleze ahadi zote alizotoa
hapo kwanza na afute kauli yake ya kupeleka gesi Kinyerezi, na wala
Serikali isitumie nguvu katika swala zima la gesi ya Mnazibay Mtwara.
TAMKO LA UMOJA WA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE –P.C.T MKOA WA MTWARA
1.
P.C.T kwa kuzingatia mwono uliopo wa hali tete yenye mwelekeo wa
kumwagika damu na kuigawa nchi vipande vipande na kuondokewa amani,
yafuatayo yafanyike
•
Serikali isitishe mpango wake wa kuondoa gesi kutoka Mnazi bay Mtwara
kwa kuisafirisha kwenda Kinyerezi Dar –es Salaam kwa bomba.
•
Mitambo ya kuchakata gesi ijengwe Mtwara ili gesi isafirishwe kama
mazao ya gesi na mabaki yake kutumiwa katika viwanda vya mbolea na
plastic.
• Mitambo ya kuzalisha umeme ijengwe Mtwara na kusafirisha umeme na kuunganisha gridi ya Taifa.
•
Viwanda vilivyoahidiwa vya mbolea,plastic,cemet n.k vianze kujengwa
sasa na isiwe propaganda tu ya kisiasa toka kwa viongozi kwa kuondoa
dhana iliyotokea huko nyuma ya kuonekana Kusini ni ukanda wa vita
usiendelezwe.
Mfano
kule Kilwa Lindi ambako ahadi ya kujenga kiwanda cha mbolea kwa gesi ya
Songo songo mpaka leo hakijajengwa kwa kuwapatia nafasi ya ajira na
kujiajiri kutokana na viwanda hivyo
•
Serikali iwe sikivu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Mikoa ya
Mtwara na Lindi ambako vyanzo vya uchumi wa gesi vipo kwa kutekeleza
madai yao, kwa kuwa hawapingi kupelekwa umeme gridi ya Taifa na kuuza
gesi iliyochakatwa tayari kwa kuliingizia Taifa mapato.
•
Serikali ikamilishe sera za gesi na mafuta na kupatikana sheria ambayo
italinda mikataba yote inayofanywa na serikali juu ya gesi na kulinda
wananchi wa eneo husika mikoa ya Mtwara na Lindi kwa madhara
yanayotokana na gesi kwa kuwashirikisha kutoa mawazo yao.
•
Mazungumzo yafanyike kati ya Serikali na wananchi katika kupata
ufumbuzi wa swala la gesi kwa njia ya Amani na wala isitumie nguvu
zilizonazo kwani kufanya hivyo ni kuleta maafa yasiyo ya lazima kwa
Taifa.
•
-Serikali isisikilize wabunge wadanganyifu ambao hawana makubaliano na
wananchi katika majimbo yao wanayotoka, ambao huchochea mgogoro huu kwa
lengo lao binafsi.
•
Viongozi ambao wametoa matusi kwa wananchi wafute usemi wao kwa
wananchi wa Mkoa wa Mtwara ambao wamewaita wahaini kwa kuwaomba radhi
bila masharti yeyote kwani semi hizo huleta chuki, uhasama, na matengano
katika nchi, na kusababisha nchi isitawalike.
•
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka
2010 Ibara 63 Kifungu H na K ambavyo vipo wazi, hasa kwa kuzingatia kuwa
sera zinazotekelezwa sasa na Serikali ni zile zote zilizoandikwa kwenye
Ilani ya uchaguzi.
•
Serikali irudishe tumaini kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na amani
inayoonekana kutoweka kwa matamshi yanayoashiria kumwagika kwa damu bila
kujali kuwa nchi ilipatikana bila kuwaga damu.
•
Serikali iwatambue wananchi wa Mikoa ya Kusini kuwa wana haki ya
kutimiziwa matakwa yao kama wananchi wa mikoa mingine kwa kupata
maendeleo kutokana na vyanzo vya uchumi vilivyopo katika maeneo yao.
-Sisi
viongozi wa dini tunamwomba Mungu awape hekima viongozi wetu wa
Serikali kwa sababu wamepewa dhamana na Mungu kuliongoza Taifa.
-Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza, bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza Methali 11:3
-Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake, bali wenye haki watapona kwa maarifa. Methali 11:9
Imesainiwa na
BISHOP C. CHILUMBA
MWENYEKITI MKOA
PAMOJA NA:-
PASTOR SELEKWA
KATIBU PCT- MKOA WA MTWARA
Nakala:
• Mwenyekiti PCT Taifa-Dar –es –Salaam
• Maaskofu na Wachungaji wote wa PCT Mkoa wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.