Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, October 27, 2012

Mbunge ala mamiloni! Awauzia TANESCO matairi 300 alipwa fedha ya matairi 600

 


SIKU chache kabla ya kikao cha Bunge kuanza mjini Dodoma, zimeibuka taarifa kwamba mmoja wa wabunge aliyekuwa mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa alishiriki kikamilifu kuendesha biashara na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambalo kimsingi anapaswa kulisimamia.

Taarifa hizo zimekuja huku tayari habari zilizovuja na kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari kudai kwamba uchunguzi wa kamati ya ndogo chini ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Maadili iliyokuwa chini ya Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali (mstaafu), Hassan Ngwilizi haikuwatia hatiani wabunge waliokuwa wakituhumiwa.


Hao walikuwa ni wabunge wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anne Makinda, waliokuwa wakituhumiwa kushiriki vitendo vinavyoashiria rushwa ndani ya TANESCO, kampuni ambayo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wake, William Mhando amesimamishwa kwa tuhuma mbalimbali.


Taarifa za karibuni zaidi zinaonyesha kwamba mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Sarah Msafiri, alikuwa na uhusiano na Kampuni ya M/S Sharrif’s Services & General Supply iliyokuwa ikifanya biashara na TANESCO na yeye kusimamia malipo yenye utata kutoka shirika hilo ambalo mbunge huyo analisimamia.


Kampuni hiyo ilikuwa inasambaza matairi ya magari kwa TANESCO ikiwa na mkataba wa matairi yenye thamani ya shilingi milioni 387.


Anasema mtoa taarifa wetu kuhusu biashara hiyo ya matairi: “Yule mbunge ndiye aliyekuwa akija TANESCO wakati wa kufunga mkataba. Mkataba ulikuwa awali wa matairi 652. Baadaye idadi hiyo ilipungua yakaletwa matairi 356, lakini pamoja na matairi kupungua, kiasi cha pesa zilizolipwa kilibaki kilekile”.


Lakini wakati hayo yakiendelea, zipo pia taarifa kwamba uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na hasa Waziri, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu Eliakim Maswi, umekuwa ukifuatilia kwa karibu taarifa zilizovuja za Kamati ya Ngwilizi zinazoonyesha kwamba ripoti ya Kamati hiyo imeukandamiza uongozi huo kwenye sakata linalouhusisha na tuhuma za rushwa za wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.


Anasema mtoa habari wetu: “Baada ya kuanza kuvuja kwa ripoti hiyo walikutana kwa nia ya kutaka kujua kwanza kwamba kweli ripoti ya kamati ile imewatuhumu na hali ikiwa ni hiyo wafanye nini, maana wao si wanasiasa, achilia mbali kwamba Profesa Muhongo ni Mbunge wa Kuteuliwa.


“Hilo la kwamba wamekwenda kumwona Rais kumwambia kwamba wanataka kuondoka sijalisikia. Ninachojua ni kwamba walikutana. Na hiyo inatokana na ukweli kwamba hawa ni watu wawili wanaoshirikiana kwa karibu katika kuendesha wizara, hivyo mmoja akiondoka sioni uwezekano wa mwingine kubaki.


“Wizara hii pamoja na taasisi zake inahitaji watu waliojitoa kusaidia nchi. Na hawa huwezi kuwalinganisha na ile timu iliyoondoka. Wanapishana sana kwa malengo na maono. Sijui maisha yao yalivyo, lakini nawaona kama watu wasio na makubwa na wasiokuwa na tamaa ya mali.


“Kwa hali ya kiwango cha ufisadi tulichofikia kama nchi unahitaji ujasiri mkubwa, kwa mfano, kusema waziwazi kwamba sasa hapatakuwa na mgawo wa umeme tena.


“Kusema hivyo maana yake unajitangazia vita na matajiri na wanasiasa wapenda mali. Lakini hawa wamesema, na wamerudia mara kadhaa, kwamba mgawo uliokuwapo ulikuwa wa kutungwa, hata hotuba ya Waziri wakati wa Bunge la bajeti ilieleza hivyo. Hiyo si kazi rahisi. Lazima watapigwa vita.


“Hivi unafikiri Kamati ya Bunge ni ya malaika? Ile ilikuwa sawa na kesi ya nyani unampelekea ngedere”.


Katika mkutano ujao wa Bunge matokeo ya uchunguzi wa kamati iliyoundwa kuchunguza sakata zima la wabunge kuhongwa na wengine kuwa na maslahi katika TANESCO licha ya kuwa wao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, yatawasilishwa kwa Spika na baadaye kuwekwa wazi kwa wabunge.


Wabunge walijikuta katika mpasuko miongoni mwao hasa baada ya kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TANESCO, William Mhando na wenzake ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu zilizokuwa zikiwakabili.


Tayari katika uchunguzi wa Mhando na wenzake zimebainika kasoro lukuki kuhusu mwenendo wao kama viongozi wa TANESCO. Hali pia si swari kwa upande wa Bodi ya TANESCO inayoongozwa na Jenerali (mstaafu) Robert Mboma, ikielezwa kuwa bodi hiyo kwa namna fulani ni sehemu ya uozo uliokuwa ukiendelea TANESCO ikiwa ni pamoja na kulea kile kinachoelezwa kuwa mgawo wa umeme wa kutengeneza ‘mezani.’


Na bado kachaguliwa CCM-NEC ?


CHANZO: Raia Mwema | 24 Oct 2012
        

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.