Je unahisi umeshaanza kumchoka mmeo ama mkeo????!!!!Chanzo: http://www.jamiiforums.com/mahusiano-mapenzi-urafiki/78716-chanzo-cha-kuchokana-katika-mahusiano-ndoa-na-ushauri-wa-kukabiliana-na-tatizo-hili.html
Imeandikwa na Shams Elmi (Abu 'Ilmi)
Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.
Utoto wa Ndoa:
Wengine hukiita kipindi hiki (Honey Moon) mwezi wa asali, kipindi cha raha, utulivu, mapenzi, maelewano baina ya wanandoa. Si lazima kiwe mwezi mmoja kama watu wengi wanavyoamini, bali kinaweza kikawa chini ya mwezi mmoja au zaidi ya mwezi mmoja.
Ujana wa Ndoa:
Hiki ni kipindi kinachofuatia baada tu ya utoto wa ndoa, ni kipindi ambacho kila mmoja miongoni mwa wanandoa anakuwa tayari ameshamtambua mwenzake katika shaksia yake (personality) kwa maana ya jinsi anavyoangalia mambo, jinsi anavyofikiri, mitazamo yake, mielekeo yake na matarajio yake.
Uzee wa Ndoa:
Kipindi hiki ni kipindi ambacho wanandoa wanakuwa tayari wameishaingia katika majukumu ya kulea kwa kupata matunda ya ndoa yao ambayo ni mtoto au watoto.
Kuchokana kwa wanandoa ni tatizo ambalo linatokea kwa familia nyingi, na kusababisha migogoro mingi na hata kufikia familia kuvunjika au kuishi kwa ajili tu ya kulea watoto na si vinginevyo.
Utakuta katika baadhi ya familia, Baba na Mama wanaishi katika nyumba moja, ukiwaona utadhani ni mume na mke wanaopendana, kumbe wanaishi kwa ajili tu ya kuwalea watoto wao na kuogopea maneno ya watu, hali hii ni hali ya talaka ya kimapenzi (emotional Divorce) na ni hali mbaya ambayo mara nyingi humpa msukumo mwanamume wa kuoa mke wa pili katika harakati za kutafuta utulivu na sehemu ya kukimbilia
Tatizo hili la kuchokana kwa wanandoa linasababishwa na wanandoa wote wawili kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki za mume na mke.
Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao, na hapa nitajaribu kujadili baadhi ya visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana visababishi ambavyo huwa vinadharaulika na kuonekana vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.
a) Kuzoeana: kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla. Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini. Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau.
b) Mazungumzo: Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake. Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote. Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.
c) Kusomana Tabia: ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa ambao wana mwaka mmoja katika ndoa yao wakawa bado hawajasomana tabia, au wakawa wameishasomana tabia, lakini kila mmoja akawa anataka tabia zake ndio ziwe dira. Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano, aidha hutafuta fursa muafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo yeye haridhiki nayo. Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha.
d) Kutamka na kudhihirisha mapenzi: Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi wowote, kwa mume au mke kumwambia mwenzake NAKUPENDA kuna athari nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama.
e) Kupeana zawadi: Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na nafasi ya mwenzako katika maisha yako, na zawadi ambayo mtu huitoa kwa mwenzake bila ya utangulizi au mnasaba maalum huleta athari njema na huimarisha mapenzi. Na katika zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa, na iwe ni zawadi maalum kwa mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo, kwa mfano, si vema kwa mwanamme kumletea mkewe zawadi ya sufuria, microwave, pazia, Dinner set, hiyo haitaitwa zawadi, lakini ni juu yake kumletea manukato ayapandayo, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu, na vitu ambavyo ni maalumu kwa matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mumewe achunge vigezo hivyo.
f) Kualikana vyakula: Inaweza kushangaza kuwa vipi wanandoa wataalikana chakula wakati wenyewe ni mume na mke, na ni lazima wale pamoja?! Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili mazingira na kufanya vitu makhsusi kwa kushtukizana, huwafanya wanandoa kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku humfanya mtu kuyachoka, ni vema wanandoa na hasa mwanamke kuwa mbunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyo tia ladha mpya katika nyumba, njia mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula maalum mumewe peke yake, na hata kama itamlazimu kununua au kuagiza aina tofauti ya chakula basi afanye hivyo, na ampe mwaliko mumewe wa kutokosa kuhudhuria katika mnasaba huo. Aidha mwanamume naye anaweza kumualika mkewe katika hoteli ya heshima mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliopita.
g) Kubadilisha mpangilio wa nyumba: Wanawake wengi huwalalamikia waume zao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala yake kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao. Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yale yale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanamume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu, na huu ndio mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba.
h) Usafi wa mwili na mavazi: Moja miongoni mwa mambo yanayokera kwa wanandoa ni uchafu wa mmoja wao, uchafu ni sifa isiyovumilika hususan kwa mwanamke, baadhi ya wanawake hudhani kuwa manukato, vipodozi ndio usafi, utakuta anapitisha masiku bila kuoga kikamilifu, bali anapitisha pitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani, kisha kujijaza manukato, lotion na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi na mumewe harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya, hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mkewe, atakaa nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mke huyu. Wanaume nao hudhani kuwa kwao wanaume ndio wamepewa kibali cha kuwa wachafu, kwa mfano wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho, na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu, huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi, aidha baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao, na jinsi wanavyojiweka, jambo ambalo linaweza kumsababishia mke maudhi, na hata kujihisi aibu kunasibishwa na mume wake.
i) Kufanya Ibada kwa pamoja: Nguzo muhimu na mhimili wa maisha ya ndoa ni kumcha Mungu/Allaah, Sala za usiku humkurubisha mja karibu zaidi na Mungu, hivyo mume na mke kuhimizana kufanya ibada hii pamoja huwazidishia imani na mapenzi baina yao na kuifanya ndoa yao kuwa imara zaidi.
Jisikie huru kabisa kuchangia lolote linalohusiana na jamii, uchumi, siasa, imani na elimu katika Blog yetu. Tunakaribisha habari, taarifa, picha za matukio, maoni na ushauri ili kuwekana sawa katika dunia yetu hii ndogo. Wote mnakaribishwa katika kuimarisha mshikamano wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini mwetu!!
Pages
Forums
- Critical Analysis (11)
- Education Issues (15)
- Geology and Mining (21)
- International News (37)
- National News (147)
- Political Issues (67)
- Religious Issues (28)
- Social Issues (79)
- Sports (19)
Saturday, October 27, 2012
Chanzo cha kuchokana katika mahusiano/ndoa na ushauri wa kukabiliana na tatizo hili
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.