Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Saturday, June 7, 2014

MASHABIKI MILIONI 3.5 KUTAZAMA MECHI 64 ZA KOMBE LA DUNIA BRAZIL

 

Na James Truman, brotherdanny5.blogspot

Sao Paulo, Brazil

JUMLA ya mashabiki 3,531,211 wanatarajiwa kuingia viwanjani kutazama mechi 64 za fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil kuanzia Juni 12, mwaka huu.
Mashabiki hao watatinga kwa nyakati tofauti katika viwanja 12 vitakavyotumika katika fainali hizo za 20, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na fainali za mwaka 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limetenga jumla ya tiketi 3,334,524 kwa ajili ya fainali hizo, lakini ikiwa mashabiki wataingia kwa idadi halisi ya viwanja hivyo, jumla yake watakuwa 3,531,211.
Sehemu kubwa ya tiketi zilizotengwa na FIFA zitagawiwa kwa makundi kama ya wafanyabiashara washirika, wanahabari na wageni maalum. Tiketi zitakazouzwa zinakadiriwa kuwa 1.1 milioni ambapo 400,000 kati yake ni kwa ajili ya Wabrazili na 700,000 kwa mashabiki kutoka nje. Kwa kila mechi, asilimia 8 ya mauzo ya tiketi itakwenda kwa timu zinazoshiriki.
Hadi kufikia Agosti 20, 2013 jumla ya tiketi 2.3 milioni zilikuwa zimeuzwa ndani ya saa 24 tu na hadi kufikia Oktoba 2013 kulikuwa na maombi ya tiketi milioni 6. Bei ya tiketi hizo inaanzia Dola 12.50 kwa mechi za awali wakati mechi ya fainali tiketi zitauzwa kwa Dola 990.
Estadio do Maracana

Taarifa zinaonyesha kwamba, uwanja wa Maracana ulioko jijini Rio de Janeiro umekarabatiwa upya kwa ajili ya fainali za mwaka huu zinazofanyika miaka 64 tangu zilipofanyika nchini humo mwaka 1950. Uwanja huo unaotumiwa na klabu kongwe nchini humo za Fluminense na Flamengo na ulifunguliwa Juni 2013 kwa mechi baina ya Brazil na England.
Estadio do Maracana ulitumiwa kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1950, ambapo mashabiki 174,000 waliingia na kuishuhudia Uruguay ikiichapa Brazil 2-1.
Uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 73,531 ndio utakaotumika kwa mechi ya fainali Julai 13, 2014, lakini pia utahusisha mechi nyingine sita na hivyo kufanya jumla ya watazamaji watakaoingia uwanjani hapo kuwa 514,717.
Mechi nyingine zitakazochezewa hapo ni mechi za Kundi F baina ya Argentina na Bosnia&Herzegovina (Juni 15, 2014); Hispania na Chile (Juni 18, 2014); Ubelgiji na Russia (Juni 22, 2014); Ecuador na Ufaransa (Juni 25, 2014); Mshindi Kundi C na Mshindi wa Pili Kundi D (Juni 28, 2014); na Robo Fainali (Julai 4, 2014).
Arena de Sao Paulo (Corinthians)

Uwanja huu uko jijini hapa Sao Paulo, ambako ndiko soka ilikozaliwa kwa nchi ya Brazil. Unatumiwa na klabu kongwe ya Corinthians na una uwezo wa kuingiza watazamaji 65,000. Sao Paulo ni mji ulioko Kusini Mashariki ma Brazil na unafahamika kama Terra da Garoa kutokana na mvua kunyesha mara kwa mara.
Katika uwanja huu jumla ya mechi sita zitachezwa na kuingiza watazamaji 390,000 katika fainali hizo.
Mechi zitakazochezewa hapo ni ile ya ufunguzi baina ya wenyeji Brazil na Croatia (Juni 12, 2014); Uruguay na England (Juni 19, 2014); Uholanzi na Chile (Juni 23, 2014); Korea Kusini na Ubelgiji (Juni 26, 2014); Mshindi Kundi F na Mshindi wa Pili Kundi E (Julai 1, 2014); na Nusu Fainali (Julai 9, 2014).
Estadio Nacional Mane Garrincha

Uwanja huu wenye uwezo wa kuingiza jumla ya watazamaji 68,009 kwa wakati mmoja, uko jijini Brasilia, mji mkuu wa Brazil tangu mwaka 1960 uliochukua nafasi ya Rio de Janeiro.
Jina la uwanja huo limetokana na nyota wa zamani wa klabu ya Botafogo na Brazil, Manuel ‘Mane’ Garrincha, ambaye alikuwa mmoja wa wanasoka mahiri nchini humo katika miaka ya 1950 na 1960.
Ndani ya uwanja huo mpya kutachezwa mechi 7 na jumla ya mashabiki 476,063 anatarajiwa kuhudhuria mechi hizo.
Mechi zitakazochezwa hapo ni baina ya Uswisi na Ecuador (Juni 15, 2014); Colombia na Brazil (Juni 19, 2014); Cameroon na Brazil (Juni 23, 2014); Ureno na Ghana (Juni 26, 2014); Mshindi Kundi E na Mshindi wa Pili Kundi F (Juni 30, 2014); Robo Fainali (Julai 5, 2014); na Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu (Julai 12, 2014).
Estadio Castelao

Uwanja huu uko jijini Fortaleza, Kaskazini Mashariki mwa Brazil, na una uwezo wa kuingiza watazamaji 58,704. Klabu zinazoutumia uwanja huu ni Ceara SC na Ferroviario AC na ndio utakaotumika kwa mechi ya pili ya Brazil ya hatua ya makundi.
Fortaleza ni maarufu kwa utalii, fukwe nzuri na vyakula vya aina yake na unatajwa kuwa na hali ya Kitropiki.
Jumla ya mechi sita zitachezwa hapa na mashabiki 352,224 wanatarajiwa kuingia uwanjani. Mechi hizo ni Uruguay na Costa Rica (Juni 14, 2014); Brazil na Mexico (Juni 17, 2014); Ujerumani na Ghana (Juni 23, 2014); Ugiriki na Ivory Coast (Juni 24, 2014); Mshindi Kundi B na Mshindi wa Pili Kundi A (Juni 29, 2014); na Robo Fainali (Julai 4, 2014).
Estadio Mineirao

Huu ni uwanja unaotumiwa na klabu ya Cruzeiro. Uko katika Jiji la Belo Horizonte, umbali wa saa moja tu kutoka Jiji la Rio de Janeiro na ni mji usio na gharama kubwa sana kwa mashabiki wa kigeni.
Hapa ndipo mwanasoka mahiri duniani, Ronaldo de Lima, alipoanza kung’ara akiwa na klabu ya Cruzeiro.
Uwanja huu una uwezo wa kuingiza watazamaji 57,483 ambao utachezewa pia mechi ya nusu fainali.
Jumla ya mashabiki 344,898 wanatarajiwa kuingia kwenye uwanja huu katika mechi sita zitakazochezwa hapa.
Mechi zitakazochezwa ni baina ya Colombia na Ugiriki (Juni 14, 2014); Ubelgiji na Algeria (Juni 17, 2014); Argentina na Iran (Juni 21, 2014); Costa Rica na England (Juni 24, 2014); Mshindi Kundi A na Mshindi wa Pili Kundi B (Juni 28, 2014); na Nusu Fainali (Julai 8, 2014).
Estadio Beira-Rio

Uwanja huu uko jijini Porto Alegre na una uwezo wa kuingiza watazamaji 48,849 ambapo pia unatumiwa na klabu mbili za Internacional na Gremio. Upo kando ya Mto Guaiba.
Porto Alegre ni mji wenye mvua kipindi cha Juni na Julai na visiwa kadhaa, kimojawapo ni Lago de Patos kilichozungukwa na miti karibu milioni moja.
Hapa patachezewa mechi tano na hivyo watazamaji 244,245 wanatarajiwa kuingia uwanjani.
Mechi zitakazochezewa hapo ni Ufaransa na Honduras (Juni 15, 2014); Australia na Uholanzi (Juni 18, 2014); Korea Kusini na Algeria (Juni 22, 2014); Nigeria na Argentina (Juni 25, 2014); na Mshindi Kundi G na Mshindi wa Pili Kundi H (Juni 30, 2014).
Arena Pernambuco

Huu ni uwanja ulioko jijini Recife na unatumiwa na klabu maarufu za Nautico, Santa Cruz na Port ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 44,248.
Recife ni mji ulioko kwenye Pwani ya Kaskazini Mashariki ya Brazil, ulitumika mara ya mwisho katika mechi ya Kombe la Dunia 1950.
Huu ni mji maarufu kwa uchumi wa Brazil, lakini wakazi wake ni mashabiki wa soka waliopitiliza.
Jumla ya mechi tano zitachezwa hapa na mashabiki 221,240 wanatarajiwa kushiriki. Mechi hizo ni kati ya Ivory Coast na Japan (Juni 14, 2014); Italia na Costa Rica (Juni 20, 2014); Croatia na Mexico (Juni 23, 2014); Marekani na Ujerumani (Juni 26, 2014); na Mshindi Kundi D na Mshindi wa Pili Kundi C (Juni 29, 2014).
Arena Fonte Nova

Huu uwanja uko kwenye Jiji la Salvador ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 52,048 na unatumiwa na klabu za Bahia na Vitoria. Uwanja huo utashuhudia mechi sita kwenye fainali hizo. Waandaaji wanasema uwanja huo mpya umejengwa kisasa na una migahawa, makumbusho ya soka, maduka, hoteli na kumbi za sherehe.
Mji wa Salvador ni uko Kaskazini mwa Brazil na ndio uliokuwa mji mkuu wa kwanza wa nchi hiyo.
Mechi zitakazochezwa hapo ni kati ya Hispania na Uholanzi (Juni 13, 2014); Ujerumani na Ureno (Juni 16, 2014); Uswisi na Ufaransa (Juni 20, 2014); Bosnia&Herzegovina na Iran (Juni 25, 2014); Mshindi Kundi H na Mshindi wa Pili Kundi G (Julai 1, 2014); na Robo Fainali (Julai 5, 2014).
Jumla ya watazamji 312,288 wanatarajiwa kushuhudia mechi hizo uwanjani hapo.
Arena Pantanal

Uwanja huo upo kwenye mji wa Cuiaba, Magharibi mwa Brazil, Kusini mwa Misitu ya Amazon. Unafahamika kama ‘Green City’ na ni maarufu kwa utalii licha ya kwamba kwa kipindi cha Juni hadi Julai hali ya hewa inakuwa tatizo kutokana na joto kufikia nyuzi 40.
Uwanja huo uliboreshwa kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia na utatumika kwa ajili ya mechi nne. Una uwezo wa kuingiza watazamaji 42,968. Ni nyumbani kwa klabu za Cuiaba na Mixto.
Hapa jumla ya mashabiki 171,872 wanatarajiwa kushuhudia mechi hizo nne za Chile na Australia (Juni 13, 2014); Russia na Korea Kusini (Juni 17, 2014); Nigeria na Bosnia&Herzegovina (Juni 21, 2014); na Japan na Colombia (Juni 24, 2014).
Arena Amazonia

Uwanja huu uko mjini Manaus, mji ambao upo katikati ya misitu ya Amazon. Una uwezo wa kuingiza watazamaji 42,374.
Mji huo unaelezwa kwamba siyo mahali pazuri sana kwa soka kutokana na kuwa katikati ya misitu, hata hivyo waandaaji wameamua fainali za Kombe la Dunia zichezwe kila kona ya nchi baada ya kuzikosa kwa miaka 64.
Huenda baada ya michuano ya Kombe la Dunia uwanja huo utageuka kuwa mahali pa wanyama.
Inatazamiwa kwa mashabiki 169,496 watahudhuria mechi nne zitakazochezwa hapo.
Mechi hizo ni baina ya England na Italia (Juni 14, 2014); Cameroon na Croatia (Juni 18, 2014); Marekani na Ureno (Juni 22, 2014); na Honduras na Uswisi (Juni 25, 2014).
Estadio das Dunas

Huu ni uwanja ulioko jijini Natal ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 42,086. Unatumiwa na klabu ya America na umemalizika kujengwa kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Estadio das Dunas utatumika kwa mechi nne za makundi katika fainali hizo. Natal ni mji unaofahamika kama Cidade do Sol (Sun City) kwa sababu umekuwa na joto linalokaribia nyuzi 28. Fukwe zilizopo Kaskazini Mashariki mwa jiji hilo zinalifanya jiji hilo lizidi kupendeza.
Jumla ya mashabiki 168,344 wanatarajiwa kuingia kutazama mechi baina ya Mexico na Cameroon (Juni 13, 2014); Ghana na Marekani (Juni 16, 2014); Japan na Ugiriki (Juni 19, 2014); na Italia na Uruguay (Juni 24, 2014).
Arena da Baixada

Uwanja huu uko jijini Curitiba ambao kwa mara ya kwanza ulijengwa mwaka 1914 lakini ukafanyia ukarabati maka 1999 na umerekebishwa zaidi baada ya Brazil kupata fursa ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia.
Unatumiwa na klabu ya Atletico Paranaense na una uwezo wa kuingiza watzamaji 41,456.
Jumla ya mechi nne zitachezwa hapa na mashabiki 165,824 wanatarajiwa kutinga.
Mechi hizo ni Iran na Nigeria (Juni 16, 2014); Honduras na Ecuador (Juni 20, 2014); Australia na Hispania (Juni 23, 2014); na Algeria na Russia (Juni 26, 2014).
Curitiba ni mji wa aina yake ndani ya Brazil na unatajwa kuwa na uchumi mkubwa. Hali yake ya hewa inafanana na Rio de Janeiro na Belo Horizonte.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.