Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, April 6, 2012

Poleni watu wa Mtera kwa kuanguka mikononi mwa chizi

 
Mbunge wa Mtera CCM, Livingstone Lusinde aka Kichaa akirapu rapu zake za matusi  ya nguoni kule Arumeru Mashariki hivi karibuni.

KAMPENI zilizopita za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, zilifichua mambo mengi hasa uhovyo wa siasa na viongozi wetu. Mambo yalianza na wazee wazima Benjamin Mkapa, rais mstaafu, kujivua nguo kwa kujifanya msemaji wa ukoo wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alimtengeneza na kumnadi Mkapa lakini baadaye akamwangusha vibaya kiasi cha kufa akiwa analilia Watanzania wake.

Nani mara hii kasahau maneno ya mke wa marehemu, Mama Maria Nyerere aliyesema kuwa maneno ya mwisho ya mumewe yalikuwa, "Nawalilia Watanzania wangu"?

Hii maana yake Mwalimu alikufa na roho iliyojikunja; ikizingatiwa Watanzania aliokuwa akiwalilia walikuwa kwenye mikono ya mtu wake lakini aliyeonyesha wazi kuwa wa hovyo kisera.

Mwingine aliyejivua nguo ni mzee Stephen Wassira, Waziri wa Uhusiano na Uratibu Ofisi ya Rais ambaye alianzisha ligi ya matusi na uongo kwenye kampeni kiasi cha kugeuka kuwa uwanja wa wahuni wa chama chake kuja kuonyesha uhuni na uhovyo wao. Wassiara alikaririwa akimtuhumu katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kula pesa ya maandalizi ya ujio wa Papa John Paul II mwaka 1990, madai ambayo yalipingwa vikali na Kanisa Katoliki ambalo bosi wake ndiye alikuwa akitembelea Tanzania.

Rais wa TEC, Askofu Mkuu Juda Thaddeus Ruwa'ichi alimjibu Wassira kwa maneno haya, “Ukiona mwanasiasa anakurupuka na kuanza kumchafua mwenzake ujue amefilisika, vitendo hivyo vinaonyesha udhaifu kwa nchi katika nyanja za siasa,”

Hayo ya Mkapa na Wassira yalikuwa cha mtoto au tuseme ufunguzi tu. Maana baba yao katika ligi hii ya matusi, Mbunge Livingstone Lusinde wa Mtera (CCM) alikuwa hajaja kumaliza kazi hii aliyotumwa na chama chake. Alikaririwa akitamka maneno ambayo si vizuri kuyarudia na wala hayafanani na mtu wa umri na wadhifa wake kama mbunge mwakilishi wa wananchi. Hivi mtu anayeweza kusimama kwenye jukwaa la siasa kutangaza sera akatangaza matusi tena kwa kuiga maneno ya vikundi vya maigizo, umuweke kundi gani? Zamani wengi tulikuwa tukikwazwa na salamu za Mkapa za kihuni za “MAMBO” bila kujua kuwa kumbe kuna wahuni zaidi.

Lusinde alikaririwa akisema kuwa kama CHADEMA ni vichaa wa kurogwa basi yeye ni wa kuzaliwa. Ni bahati mbaya na hasara kuwa na viongozi aina ya Lusinde. Je, ilikuwaje watu wa Mtera wakamchagua chizi anayekiri kuwa chizi tena tangu kuzaliwa? Je, alipitaje kwenye mchujo au ni yale yale ya wananchi kuchoka utawala wa mtu mmoja na wa kurithishana kutokana na ukweli kuwa mbunge wao wa zamani John Malecela alikuwa amewachosha kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu?

Nashindwa kujua mantiki ya kumchagua mtu wa hovyo na kichaa kama huyu anayeweza kusimama jukwaani na kuwadhalilisha wenzake tena mbele ya watoto wadogo akionyesha uhodari wa kuchambua mavazi ya wenzake badala ya matatizo ya anaowawakilisha?
Hivi mbunge anaposimama jukwaani na kugeuza mdomo wake sehemu ya kutolea uchafu, tena mbele ya kadamnasi na watoto, anajenga picha gani? Je, huu si ushahidi tosha kuwa CCM imeishiwa kiasi cha kushabikia uhuni na mipasho ya kipumbavu? Je hii si kuigeuza CCM kuwa Chama Cha Matusi? Hata waimbaji wa taarabu za matusi na hata rap wana afadhali kwa vile wayafanyayo ni saizi yao.

Sijui kama Lusinde anasoma hata magazeti zaidi ya yale ya udaku kama alivyothibitisha kwa kauli zake za kichovu na kiwendawazimu. Je, maneno na tabia vya Lusinde vinakisaidiaje chama chake zaidi ya kukibomoa? Maana ukiangalia kuzodolewa, kwa mfano, kwa Wassira hata Mkapa ni ushahidi tosha kuwa CCM iko pabaya na imeishiwa.

Je yote haya ni matokeo ya kuua maadili na kuingiza madili kwenye nafasi yake? Maana kwa nchi yenye kufuata sheria na kanuni za maadili, tume ya uchaguzi (NEC) ilipaswa kutoa tamko hata karipio mara moja Lusinde alipogeuza kampeni uwanja wa kushindanisha ukichaa na matusi ya nguoni.

Hivi mtu anayeweza kuwaita wanaume wenzake mashoga na wajawazito ana akili kweli? Heri angeishia pale. Wenye mtindio wa akili wenzake wangedhani amewajibu wapinzani japo siyo. Nani mara hii alivyowaambia wapiga kura kuwa yeyote ambaye hataichagua CCM ni mjamzito? Je, ujauzito ni ugonjwa? Hivi bila ujauzito mama yake angemzaa kweli? Je kutukana watu kwa kutumia ujauzito si kuwadhalilisha wanawake na mama yake akiwamo? Maana huo ujauzito usio na baba maana yake ni umalaya.

Maneno ya Lusinde ni ushahidi kuwa hakupata malezi mema wala elimu ya kutosha kiasi cha kujenga taswira kuwa huenda alizaliwa mitaani. Maana hata tofauti na wahuni wanaopiga debe kwenye mabasi ya daladala wala wauza mitumba Mtaa wa Kongo. Heri ya wao wamefukarishwa na akina Lusinde kuliko Lusinde anayelipwa kodi ya wananchi kwa kuchafua maadili akilinda na kutetea uozo na mgando wa mawazo. Tena uoza wenyewe utawala wa kurithishana kama walivyoonyesha kwenye kuteua wabunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki!

Kama siyo CHADEMA kuchelea kukimbizana na kichaa, ilifaa afunguliwe mashitaka. Hata hivyo, kwa kauli za watajwa watatu, kama CHADEMA watashindwa basi wana kila sababu ya kwenda mahakamani na kudai uchaguzi haukuwa huru na wa haki. Maana haki na uhuru ni heshima na si kashfa tena za kuzua na matusi. Laiti Lusinde angewatuhumu CHADEMA mambo ya kweli, hakuna ambaye angehangaika naye. Litakuwa jambo la ajabu na hatari kama CCM na Tume ya Uchaguzi hawatamchukulia hatua za kinidhamu tena za wazi Lusinde.

Kuna haja ya wachambuzi wa mambo kudodosa na kupata historia ya Lusinde ili apewe msaada na wale waliofanya kosa kumwamini wadhifa wa heshima kama ubunge. Kimsingi lugha na matusi ya Lusinde yamewadhalilisha wabunge wote hasa wa chama chake na uongozi mzima. Hivi kama Lusinde ana mke na watoto hata wazazi wake sijui amewaumiza kiasi gani kwa kujivua nguo hadharani hivyo? Poleni sana watu wa Mtera. Huenda ni yale yale kuwa atukanaye wakubwa haishii na mmoja.

Alimtukana John Malecela akazoea sasa anataka kumtukana kila apitaye. Si ajabu akitofautiana hata na mwenyekiti wake hatakosa kumfurumshia mitusi ya nguoni kama alivyozoeshwa na chama chake. Poleni wapiga kura wa Mtera kwa kudhalilishwa na Lusinde ambaye aliwakilisha matusi badala ya heshima na matatizo yenu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 4, 2012.

Mbunge ‘Chichim’ alivyomwaga mitusi Arumeru

LEO tumeamua kukaa kikao cha wanakijiwe wote ili kumjibu chizi mmoja aitwaye mheshimiwa japo sisi si machizi. Kama mkituona machizi shauri yenu. Tunaweza kuonekana walevi kutokana na kunywa kahawa na shida nyingi lakini bado si machizi kama Leavingstorm Lushinde chizi nambari wani wa Chama Cha Machizi (CCM).

Mie kama mwenyekiti naanzisha mjadala.
Nilikohoa kidogo na kuanza, “Waheshimiwa wanywa kahawa, kwanza naona mmechukia kutokana na matusi yalivurumishwa na mbunge wa ndugu yetu na rafiki yetu Mbwamwitu ambaye ni mpiga kura wa jimbo la Mtela,”

Wote kwa pamoja wanatikisa vichwa wakiashiria kukubaliana na pwenti yangu. Naendelea, “Mie leo si msemaji bali mwezeshaji. Hivyo naomba rasmi nifungue kikao hiki kitukufu ambacho licha ya kumjadilli huyu bwana kitatoa maazimio.”

Mbwamwitu anaamsha mkono na ninamruhusu arambe mic. Anaanza, “Ndugu zangu nashukuru sana kwa kuliona hili na pole zenu nimezipokea ingawa bado roho inaniuma. Hata hivyo msishangae sana. huyu jamaa kama alivyosema kweli ni chizi na aliwahi kukamatwa mara nyingi kwa makosa ya kuvuta bangi, udokozi na mazambe mengine mengi. Hivyo nina wasi wasi alipokuwa akiwekwa ndani mara nyingi, huenda lolote limemtokea na ndiyo maana anawasingizia wenzake kufanyiwa mchezo mbaya kama alivyowahi kufanyiwa.”

Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anakula mic, “Hakuna kitu kimenikera kama jamaa kuwaita wenzake mashoga kiasi cha kutufanya tuamini yeye ndiye. Halafu anawatukana watu eti wana mimba, kwani mama yake alimzaa bila kubeba hiyo mimba? Huyu jamaa inaonekana anawadhalilisha akina mama akiwamo mama yake wallahi,”

Wakati Mchunguliaji akimwaga usongo wake, Mzee Kidevu anadandia, “Huyu jamaa kweli chizi nimeamini. Kwanza, huyu chizi kihiyo hajui hata Kiswahili. Mnakumbuka aliposema eti dokta Silaha aliposema ana uchungu na nchi hii eti alimshagaa mwanaume anawezaje kuwa na uchungu? Kwani uchungu ni wa kuzaa tu?”

Mara Mipawa anachomekea, “Jamaa ana ugomvi na mimba huyu. Huenda kichaa chake kinachukia mimba.”

Watu hawana mbavu wanacheka ingawa habari yenyewe si ya kuchekesha zaidi ya kuhuzunisha. Mara Mbwamwitu anakatua mic tena, “Basi mwenzenu nina uchungu naye. Laiti nikikutana naye kwenye kiza ataipata hiyo mimba anayowapa wenzake. Huyu inaonakana anataka kupewa mimba.”

Msomi Mkatatamaa aliyekuwa kimya muda wote aliamua kutia guu, “Jamani msijipasue vichwa. Kimsingi, Lushinde alichofanya ni kuthibitisha madai ya siku nyingi kuwa chama chake kimeishiwa sera. Kilianza na usanii, kikachemsha. Kilidandia uongo, kimechemsha. sasa kimeona haitoshi kimedandia matusi.” anavuta kombe lake na kubwia kahawa na kuendelea, “Matusi ya Lushinde kimsingi si ya kuwahuzunisha wala kuwalenga wapinzani bali chama chake na viongozi wake waliokuwa wakichekelea alipokuwa akitumia mdomo wake kutoa haja kubwa. This annoyed me to death so to speak.”

Anakatua kashata na kuendelea. “Kila mtu kwake shoga. Inakuwa vigumu kujua huyu bwana kwanini anapenda sana ushoga na kuchukia mimba,” Msomi Mkatatamaa alizidi kuchanja mbuga kwa taaluma na busara zake baada ya wazee kumwambia apunguze hasira kuongea kikameruni hata kama alikuwa akiongelea habari za mkameruni mhishimiwa.

Aliendelea, “Hakika wazazi wake, mke wake, watoto wa Mkameruni Lushinde wamekula hasara. Anavyowatia aibu sina hamu. Hata yule mheshimiwa Sonko wa Nonihino huvuta bangi, kunywa gongo na kupayuka lakini hajawahi kuona mdomo choo kama wa Lushinde. Maana kama sera basi chama chake cha Matusi (CCM) kimepata mpiga debe. Ila itakuwa muujiza kama walengwa wa makombora ya Lushinde wasipomfikisha mhakamani. Sisi kijiweni ukimtukana mjumbe au mwenyekiti tunasema umetukana kijiwe kizima. Hivi Lushinde anapotukana wabunge si kama anatukana jimbo zima?”

Nami sikujivunga. Nilichomekea, “Namkaribisha Lusenge sorry Lushinde aende Kijiweni Mwenge akapige debe au akiweza aende zake gerezani akauze unga. Namshauri Lushinde aje nimuonyesha picha niliyopiga na mzee Matonya ili aone tofauti ya masikio yaliyotobolewa kimila na haya ya kishoga.” wanakijiwe hawana mbavu.

Mgosi Machungi naye hataki kikao kiishe bila kukifunga. Anakula mic, “Mie sikujua kuwa kumbe Ushinde na wenzake wamechanjwa makalioni tena na poofesa Maji Mafupi. Angejua aipotoka kwao N’koogwe akaja Ushoto kue Irente kutafuta wachawi kioo chake kiivunjika akarudi kwa haraka.”

Mpemba “Yaelekea huyu jamaa ashafungwa sana na kufanyia nchezo mbaya kiasi cha kudhani kila aendaye jela afanyiwa nchezo kama alofanyiwa,” kijiwe hakina mbavu.

Mchunguliaji. Msomi mkatatamaa anaamua kurejea ili kutoa usomi na busara zake. Tunamheshimu na kumtegemea sana maana huwa hana mdomo mchafu ingawa leo ameudhika kiasi cha kuvunja mwiko na kutoa lugha ya ukali. Anakatua mic, “Nilipokuwa masomoni ulaya nilizoea kusikia watu wenye midomo mibovu kama hivi wakiitwa Chiwawa yaani vijimbwa vidogo vinavyobweka sana vikimuona mtu lakini akivikaribia vinafyata mkia na kutoka mkuku,”

Anakunywa kahawa yake na kuendelea, “Kwa hiyo sitashangaa kama Chakudema hawatamchukulia hatua chiwawa huyu maana wanajua chiwawa ni chiwawa hata ukimpeleka mahakani bado hakimu atamuachia kwa vile ni chiwawa.”

Mzee Kidevu anatuacha hoi. Anasema, “Ingawa mie sijawahi kwenda Ulaya, anawajua hawa mbwa ambao Kiswahili huitwa kusiri. Hivyo, tuna bahati mbaya kuwa na mbu… samahani simalizii mwenye tabia kama za kusiri. Je, tuseme hiki ni chama cha Makusiri?

Wanakijiwe tunaangaliana kuonyesha jinsi mzee mwenzetu alivyochomekea kitu kingine kwani Kusiri na Chiwawa ingawa wote ni mbwa. Wanakutana kwenye sifa moja yaani uchizi wa kubweka bweka hovyo.

Mpemba ambaye alikuwa akibofyabofya simu yake kiasi cha kuachwa nyuma kimaongezi anastuka na kula mic, “ Yakhe mie naona kama huyu jamaa ashaingiliwa na popobawa. Maana popobawa siku zote aja wakati wa uchaguzi na apenda sana wao wa chama cha Machizi kwani naye chizi.”

Wajumbe hawana mbavu. Wakati tukijiandaa kuendelea na kikao si chizi Lushinde alipita na mshangingi wake. Tuliinuka na kumtoa nje tayari kumfanyizia ili tumpige picha na kuonyesha umma alivyo chakula. Usimwambie mtu, kuwa kweli jamaa si riziki.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 4, 2012.

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.