Uzinzi unampelekea mtu kuingia Motoni. Kama ilivyokuja katika Qur-ani, Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Israa (Bani Israil) aya ya 32, "
وَلا تَقْرَبُوا الزِّنَى إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلا
Maana yake, "Wala msikaribie zina. Hakika hiyo ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa)."
Na pia imetajwa adhabu ya zina duniani na Akhera kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Furqaan aya ya 68 mpaka 70, "
وَالَّذِينَ لا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَلا يَزْنُونَ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا * يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا * إِلاَّ مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلا صَالِحًا...
Maana yake, "Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakaefanya hayo atapata madhara (papa hapa ulimwenguni kabla ya Akhera). Na atazidishiwa adhabu siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka (muda mrefu kabisa) milele. Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri..."
Na Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratin Nuur aya ya 2, "
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ وَلا تَأْخُذْكُمْ بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِنْ كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِنْ الْمُؤْمِنِينَ
Maana yake, "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao mijeledi (bakora) mia. Wala isiwashikeni huruma kwa ajili yao katika (kupitisha) hukumu hii ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao (hii) kundi la Waislamu."
Wanavyuoni wamesema kwamba aya hii iliyotajwa juu (Surat Nuur aya ya 2) ni ile adhabu ya duniani kwa mwasherati (mzinifu) ambaye hakuoa/hakuolewa. Ikiwa mtu aliwahi kuoa/kuolewa kabla, akazini, kwa sheria iliyotolewa na Mtume S.A.W. adhabu ya duniani ya yule mzinifu mwanaume au mwanamke ni kupigwa mawe mpaka afe, hii adhabu kali huamrishwa baada ya mashahidi wanne kutoa ushahidi wao ya kwamba wameona kitendo cha kweli cha zina, au baada ya kukiri mmoja wao kati ya wawili waliozini kuwa kweli katenda kile kitendo. Kama ilivyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Jaabir bin Abdallah R.A.A. na kutolewa na Abu Daud Mtume S.A.W. kasema, "
"أَنَّ رَجُلاً زَنَى بِامْرَأَةٍ ، فَأَمَرَ بِهِ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَجُلِدَ الْحَدَّ ، ثُمَّ أُخْبِرَ أَنَّهُ مُحْصَنٌ فَأَمَرَ بِهِ فَرُجِمَ."
Maana yake, "Hakika mwanaume alimzini mwanamke. Mtume S.A.W. akaamrisha aadabishwe kisheria akapigwa mijeledi (mia). Kisha akaambiwa kuwa yeye kaoa. Akaamrisha apigwe mawe mpaka afe."
Ikiwa hawataadhibiwa hapa duniani na wakafa bila kutubia, wataadhibiwa katika Moto wa Jahannam kwa kupigwa mijeledi ya moto. Na hatari ya Mwislamu wakati wa kufanya kile kitendo, Mwenyezi Mungu Mtukufu humnyang`anya Uislamu wake. Kwani hakiwi kitu kizuri na kibaya kukutanika pamoja sehemu moja wakati mmoja. Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari na Muslim, "
"لا يَزْنِي الزَّانِي حِينَ يَزْنِي وَهُوَ مُؤْمِنٌ ، وَلا يَسْرِقُ السَّارِقُ حِينَ يَسْرِقُ وَهُوَ مُؤْمِنٌ وَلا يَشْرَبُ الخمر حِينَ يَشْرَبُهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ ، وَالتَّوْبَةَ مَعْرُوضَةٌ بَعْدُ."
Maana yake, "Hazini mzinifu wakati anapozini naye ni Mwislamu, wala haibi mwizi wakati wa kuiba naye ni Mwislamu, wala hanywi ulevi wakati wa kuunywa naye ni Mwislamu. Lakini toba inarejesha imani."
Na katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Ttirmidhi na Abu Daud na Baihaqi, Mtume S.A.W. kasema, "
"من زَنَى أو شرب الخمر نزع الله مِنْهُ الإيمَانُ كما يَخْلَعُ الإنسان القميص من رَأْسِهِ."
Maana yake, "Atakaezini au kunywa ulevi (naye ni Mwislamu) Mwenyezi Mungu anamnyang`anya imani kama anavyovua shati kutoka kwenye kichwa chake."
Tukirejea wakati wa zama za Mtume S.A.W., alikuwa akiwaapisha na kuchukua ahadi kutoka kwa wanawake na wanaume kabla ya kuingia katika Uislamu. Na hicho kiapo cha ushahidi wa kutokuuwa au kuiba au kuzini kinachukuliwa kuwa ni ahadi ya kweli kwamba haya mambo yameharamishwa katika Uislamu. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Mumtahinah aya ya 12, "
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا جَاءَكَ الْمُؤْمِنَاتُ يُبَايِعْنَكَ عَلَى أَنْ لا يُشْرِكْنَ بِاللَّهِ شَيْئًا وَلا يَسْرِقْنَ وَلا يَزْنِينَ وَلا يَقْتُلْنَ أَوْلَادَهُنَّ وَلا يَأْتِينَ بِبُهْتَانٍ يَفْتَرِينَهُ بَيْنَ أَيْدِيهِنَّ وَأَرْجُلِهِنَّ وَلا يَعْصِينَكَ فِي مَعْرُوفٍ فَبَايِعْهُنَّ وَاسْتَغْفِرْ لَهُنَّ اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ
Maana yake, "Ewe Nabii! Watakapokujia wanawake walioamini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawaua watoto wao, wala hawataleta uzushi wanaozusha tu wenyewe baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana ahadi nao na uwatakie msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwingi wa rehema."
Na adhabu ya mzee mzinifu siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu S.W.T. hatasema naye wala kumtazama (kwa jicho la rehema) na wala kumtakasa (madhambi yake) na atakuwa na adhabu kali. Kama alivyosema Mtume S.A.W. katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Muslim na Nnasaai, "
ثَلاثَةٌ لا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ وَلا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ: شَيْخٌ زَانٍ ، وَمَلِكٌ كَذَّابٌ ، وَعَائِلٌ مُسْتَكْبِرٌ
Maana yake, (Aina ya watu) watatu Mwenyezi Mungu hatasema nao siku ya Kiyama wala hatawatazama na wala kuwatakasa na watakuwa na adhabu kali: Mzee mzinifu, na mfalme mwongo, na maskini anayejivuna."
Na sababu kubwa ya Uislamu kuharamisha kuzini na mke wa jirani kwani dhambi yake ni mara kumi kuliko kuzini na mwanamke asiyekuwa wa jirani. Kama ilvyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Masoud R.A.A. na kutolewa na L-Bukhari na Muslim kasema, alimuuliza Mtume S.A.W., "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Jee, ipi dhambi kubwa? Mtume S.A.W. akamjibu kama ifuatavyo, "
أَنْ تَجْعَلَ لِلَّهِ نِدًّا وَهُوَ خَلَقَكَ . فقُلْتُ: إن ذلك لعظيم ، قُلْتُ: ثُمَّ أَيٌّ ؟ قَالَ: أَنْ تَقْتُلَ وَلَدَكَ مِنْ خشية أَنْ يَطْعَمَ مَعَكَ ، قُلْتُ: ثُمَّ أَيٌّ ؟ قَالَ: أَنْ تُزَانِيَ حَلِيلَةَ جَارِكَقَالَ: وَأَنْزَلَ اللَّهُ تَعَالَى تَصْدِيقَ قَوْلِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سورة الفرقان آية رقم 68-70.
Maana yake, "Usijaalie kitu chochote sawa na Mwenyezi Mungu, na hali Yeye kakuumba." Nikasema: "Hakika hiyo ni kubwa." Nikauliza: "Ipi nyingine?" Akajibu: "Usimwue mtoto wako kwa khofu atakula na wewe." Nikauliza: "Ipi nyingine?" Akajibu: "Usimzini mke wa jirani yako." Kasema: Ndipo Mwenyezi Mungu alipoteremsha Suratil Furqaan tokeya aya ya 68 hadi 70 kusadikisha ukweli wa kauli ya Mtume S.A.W., "
وَالَّذِينَ لا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَلا يَزْنُونَ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا * يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا * إِلاَّ مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلا صَالِحًا¦
Maana yake, "Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakaefanya hayo atapata madhara (papa hapa ulimwenguni kabla ya Akhera). Na atazidishiwa adhabu siku ya Kiyama na atakaa humo kwa kufedheheka (muda mrefu kabisa) milele. Ila yule atakaetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri..."
Kama inavyojulikana Iblisi daima ni adui wa binadamu, anamkimbilia kumpoteza na kumwangamiza na bila mtu yule kuhisi kuwa anayoyafanya yote hayo mabaya Iblisi ndiye anayemchochea na kumshangilia na kumpambia uovu na kuona huo uovu ni mambo mazuri wala hayana kitu akiyafanya. Iblisi pia anayafumba macho ya binadamu na huwa mtu yule haoni na kumtumainisha kuwa wewe utaishi miaka mingi wala usijali tumia uhai wako. Ukifikia umri wa uzee hapo ndipo unaweza kutubu. Jee! Kuna mtu anaejua ataishi miaka mingapi hapa duniani?" Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Jaabir bin Abdallah R.A.A. na kutolewa na Muslim, "
"إِنَّ إِبْلِيسَ يَبْعَثُ جنوده في الأرض وَيَقُولُ لهم: أيكم أضل مسلما ألبسته التاج على رأسه ، فأَعْظَمُهُمْ فِتْنَةً أقربهم إليه مَنْزِلَةً ، فيَجِيءُ إليه أحدهم فيقول له: لم أزل بفلان حتى طلق امْرَأَتِهِ ، فَيَقُولُ: مَا صَنَعْتَ شَيْئًا سوف يتزوج غيرها ، ثُمَّ يَجِيءُ الآخر فيقول لم أزل بفلان حتى ألقيت بَيْنَهُ وَبَيْنَ أخيه العداوة ، فَيَقُولُ: مَا صَنَعْتَ شَيْئًا سوف يصالحه ، ثم يجيء الآخر فيقول: لم أزل بفلان حتى زنى ، فيقول إِبْلِيسَ . نعم فعلت فَيُدْنِيهِ مِنْهُ ويَضَعُ التاج عَلَى رأسه ، نعوذ بالله من شرور الشيطان وجنوده."
Maana yake, "Hakika Iblisi anatuma askari wake (wa Kijini) katika ardhi na kuwapa ahadi kuwa yeyote yule atakayempoteza Mwislamu atavikwa taji. Kwa mfanyaji fitina mkubwa kabisa kati yao ni karibu naye huyo Ibisi katika cheo. Kisha (Shetani) mmoja wao akirejea baada ya kazi yake kwa Iblisi husema: "Sikumwacha fulani mpaka amemwacha mkewe. Iblisi anajibu; "Hukufanya kitu; ataoa mwingine!" Shetani mwingine humsogelea Iblisi na kumwambia: "Sikumwacha fulani mpaka yeye na kaka yake wakawa maadui." Ibisi anajibu " Hukufanya kitu; watapatanishwa." Mwingine anakuja kwake na kumwambia: "Sikumwacha fulani mpaka amezini." Iblisi husema (kumwambiya huyo Shetani): "Naam. (Ama wewe, naam) umefanya kazi nzuri!" Kisha humkalisha karibu yake na kumvika taji. Mwenyezi Mungu atuepushe na shari za Shetani na askari wake."
Pia Hadithi iliyopokelewa na Abdallah bin Haarith R.A.A. na kutolewa na Ahmad na Tabarani, Mtume S.A.W. kasema, "
"ما من ذنب بعد الشرك بالله أعظم عند الله من نطفة وضعها رجل في فرج لا يحل له."
Maana yake, "Hakuna dhambi kubwa baada ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu mbele ya Mwenyezi Mungu kama mwanamume kuweka mbegu ya uzazi (manii) katika utupu usio halali yake."
Kwa sababu anaemzini mke wa mtu anakuwa kamfanyia dhulma mumewe, na ikiwa kashika mimba basi mtoto anaezaliwa huwa si miongoni mwao. Na ikiwa kamzini msichana hajaolewa akizaa mtoto wa haramu huwa kamwangamiza maisha yake na mustakbali wake.
Na pia kamvunjia heshima yake na ya wazazi wake. Na zina imefananishwa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa sababu SHIRKI ni dhulma kubwa.
Na zina inakuja kwa njia tofauti kama alivyoelezea Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Ahmad, "
"الْعَيْنُ تَزْنِي وَالْقَلْبُ يَزْنِي فَزِنَا الْعَيْنِ النَّظَرُ وَزِنَا الْقَلْبِ التَّمَنِّي وَالْفَرْجُ يُصَدِّقُ مَا هُنَالِكَ أَوْ يُكَذِّبُهُ."
Maana yake, "Jicho linazini, na moyo unazini, na zina ya jicho ni kutazama, na zina ya moyo ni kutamani, na utupu pale pale unasadikisha au unakanusha."
Chanzo: http://sekenke.com/bodi/showthread.php?t=5
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.