MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, amesema yuko tayari kujiuzulu ikiwa itabainika kuwa alihusika kwa namna moja ama nyingine kukodishwa kwa Kampuni ya UDA kwa masilahi yake.
Mbali na msimamo huo, meya huyo sasa anatamani shirika la usafirishaji la UDA lifutwe na lisiwepo tena.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Masaburi, alisema jiji limekuwa na matatizo mengi na kila yakitafutiwa ufumbuzi, wapo wanasiasa wanaojaribu kuvuruga.
“Msimamo wangu ni bora Machinga likapewa wafanyabiashara wakubwa na UDA ikafutiliwa mbali isiwepo kabisa,” alisema.
Alisema amekuwa akisimamia shughuli za jiji kwa masilahi ya Watanzania lakini wapo wanaombeza na kudai kuwa amekuwa akifanya hivyo kwa masilahi yake binafsi.
“Uchunguzi ufanywe, kama ikithibitika ninafanya hivi kwa masilahi yangu, nitajiuzulu, lakini kama si hivyo, sijiuzulu,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la Machinga Complex, alisema jengo hilo lilijengwa kwa mkopo kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Benki ya Exim ya China, mkopo wa sh bilioni 12 na fedha zinazotakiwa kurejeshwa ni sh bilioni 32. Masaburi alisema jiji linatakiwa kurejesha sh bilioni 3.6 kila mwezi, fedha ambazo ni ndoto kwa jiji hilo kuzipata kwani hata makusanyo yake ya vyanzo vyake vya mapato havifikii kiwango hicho.
Alisema wamachinga hao awali walikuwa wanalipa kodi ya sh 60,000 lakini kutokana na kuzorota kwa biashara, walipunguziwa hadi sh 10,000 ambazo kwa mwezi watalazimika kukusanya karibu sh milioni 480.
“Jengo al Machinga lazima lijitegemee, lakini kwa utaratibu huu, lazima tukubaliane iwe ni sehemu ya huduma na sisi au serikali itoe ruzuku ili kurejesha mkopo huo au tuweke wafanyabiashara wakubwa,” alisema Dk. Masaburi.
Alisema wameunda bodi itakayotafuta mtaalamu atakayeona nini kifanyike, “lakini maadui wa kisiasa wanaona kama mimi ndiye ninayezorotesha shughuli za jengo lile. Tunaiachia bodi ifanye kazi yake.”
Kuhusu UDA, Dk. Masaburi alisema shirika hilo ndilo lenye matatizo makubwa na linaloleta mvurugano katika utawala wa jiji.
Alisema shirika hilo linaendeshwa kwa ubia wa makundi matatu, ambayo ni Jiji, Hazina na Simon Group.
Alisema pamoja na kwamba madiwani wanasema hawamfahamu Simon Group kama mwekezaji, lakini ameingia mkataba kisheria ingawa mkataba huo una mapungufu.
Alisema mwekezaji huyo amewekeza fedha zake na anaendelea kutekeleza mkataba wake ingawa sasa amefikia hatua ya kushindwa hata kuwalipa wafanyakazi mishara.
“Mkataba wake upo kihalali ingawa una mapungufu kama ya kuuziwa hisa kwa bei ya chini, na anayempinga aende mahakamani,” alisema.
Alisema mwekezaji huyo amekwisha kununua mabasi ambayo kama serikali itavunja mkataba wake, upo uwezekano wa kudai fedha nyingi zaidi ya alizowekeza sh milioni 285.
Alisema baada ya kutokea matatizo hayo, alilazimika kuzuia akaunti zote sita za UDA lakini baada ya kuona mwekezaji anasuasua alitaka kuifungua akaunti moja, lakini serikali na madiwani walipinga.
Hata hivyo alisema uamuzi uliofikiwa na baraza la madiwani ni kuunda bodi inayohusisha jiji, Simon Group, serikali kwa maana ya Hazina, lakini mikutano ikiitishwa mjumbe wa Hazina hafiki kwenye vikao, akidai kikao halali ni cha bodi ya UDA ambayo amekwisha kuivunja na shirika hilo kubakia mikononi mwa menejimenti ya muda.
Alisema mikataba yote hiyo yenye mapungufu ilipata baraka zote kutoka kwa Idd Simba.
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Meneja Mkuu wa UDA, Said Fikirini, alisema tangu kuingia kwa Simon Group, walichukua sh 1,080,000,000 na zilizotumika kwa shughuli za mishahara na matengenezo na mafuta ya magari ni sh milioni 500 katika kipindi cha miezi minane ya kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa meneja huyo, wafanyakazi waliopo sasa wa shirika hilo ni 96 na hupokea mishahara ya kati ya sh milioni 32 na 35 na kwamba kwa mwezi shirika hilo hutumia jumla ya sh milioni 40 wakati uzalishaji si zaidi ya sh milioni 30.
Dk. Masaburi alisema kuhusu matatizo ya Shirika la Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) walipata barua ya maelekezo kutoka kwa Waziri wa Tamisemi hivyo kuwafunga wasifanye chochote kwenye shirika hilo.
Kuhusu madai ya kuvunja bodi ya shirika hilo, alisema kuna sheria iliyompa mamlaka ya kuvunja bodi lakini ipo sheria nyingine ya Bunge inayokinzana na sheria hiyo.
Tanzania daima
|
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.