Jinamizi linaloendelea kukitesa Chama cha Wananchi (CUF) limeendelea kukigubika chama hicho, kufuatia Uongozi wake Manispaa ya Mtwara-Mikindani kujiuzulu.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya kundi la watu wnaodaiwa kuwa ni wanachama kuvamia ofisi za chama hicho na kushinikiza kujiuzulu kwa uongozi wote wa manispaa. Katika kutii amri hiyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Salum Mchimbuli, alitangaza kuvunjwa kwa kurugenzi zote kisha na yeye kujiuzulu.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa uongozi wa chama hicho ulikuwa katika kikao cha ndani ambapo pamoja na mambo mengine, kilikuwa kinajadili taarifa ya aliyekuwa mgombea ubunge wa chama hicho, Uledi Abdallah, kujivua uanachama.

“Walikuwa katika kikao cha ndani,ghafla kundi la watu waliojitambulisha kuwa ni wananchama walivamia ofisi na kutaka kufanya vurugu…Mwenyekiti aliwasihi wasifanye vurugu huku akiwauliza shida yao, kundi hlo la vijana likasema kuwa wanataka uongozi wote ujiuzulu,” alisema mmoja wa wajumbe.

“Abdallah alitangaza nia ya kujiondoa katika chama hicho kwa madai kuwa chama hicho kimekaribia kufa hivyo hana budi kuachana nacho,” alisema.

Aliyekuwa Katibu wa CUF, Said Kulaga, alithibitisha kurungezi zote kujiuzulu pamoja na mwenyekiti. “Ni kweli tukio hilo limetokea na Mwenyekiti alitumia busara ili kuepusha madhara, lakini ni kinyume na katiba ya chama,” alisema Kulaga.



CHANZO: NIPASHE