Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 20, 2012

Mgombea CCM Arumeru Ajitoa Alia Mchezo Mchafu


 
Monday, 20 February 2012 07:32
Waandishi Wetu
HEKAHEKA za kutafuta mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Jimbo la Arumeru Mashariki zinazoshika, kasi zimeingia doa baada ya mmoja wa wagombea aliyejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kuamua kujitoa akilalamikia rafu ukiwamo mchezo mchafu wa rushwa.

Aliyejitoa katika mbio hizo ni Rais  wa Mtandao wa Vijana nchini (YDN), Elipokea Urio akidai kuwa mchezo mchafu umekuwa ukichezwa kwa baadhi ya wagombea wenzake wa CCM kutoa rushwa.

“Nimeamua kujitoa kwa roho moja kabisa kutafuta ridhaa ya chama kiniteua kitokana na mchezo mchafu wa rushwa unaoendelea huko Arumeru Mashariki. Ninajua mchakato hautakuwa wa haki, sasa kwaini nichafue historia yangu?”alisema Urio akihoji.

Katika hatua nyingine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeonya kuwa kitamuengua kwenye kinyang’anyiro hicho mgombea yeyote atakayebainika kwenda kinyume cha maadili na maelekezo ya kampeni za kuwania uteuzi wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Arumeru, Totinani Nandonde alitoa onyo hilo juzi, wakati akimkabidhi Mhadhiri wa Sheria, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Anna Mghwira fomu ya kuomba uteuzi kuwania ubunge jimboni humo ambaye ni mwanachama wa tano kujitokeza ndani ya chama hicho kuwania nafasi hiyo.

“Ili kudhibiti hujuma na matumizi ya fedha katika kampeni, chama kimepanga siku ya mkutano mkuu maalumu wa wilaya utakaotumika kuwapigia kura za maoni wagombea wote kuwa ndiyo siku ya kampeni kwa wote wanaowania uteuzi. Hakuna mgombea anayeruhusiwa kupita huko kwenye kata na vijiji kufanya kampeni hivi sasa,” alisema Nandonde.

Wakati huohuo pamoja na Takukuru kuonya wagombea ubunge wanaowania kuteuliwa na CCM katika Jimbo la Arumeru Mashariki  juu ya matumizi ya rushwa katika kinyang’anyiro hicho, baadhi ya wagombea hao wanadaiwa kuendelea kutoa mlungula bila wasiwasi wowote.

Katika kuhakikisha inazuia matumizi ya rushwa katika uchaguzi huo, Takukuru imetoa onyo hilo kwa wagombea wote sita wa CCM baada ya kukutana nao juzi jioni.

Hata hivyo, hatua hiyo haijasaidia lolote huku uchunguzi ukionyesha kuwa baadhi ya wagombea wakimwaga fedha kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya Arumeru  utakaofanyika leo,  kwa kuwagharamia usafiri kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, malazi na chakula.
Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.