Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 20, 2012

Kashfa ya utapeli yatikisa Kanisa


Elius Msuya

KANISA moja huko Mlandizi, wilayani Bagamoyo, Pwani, limeingia katika kashfa ya kuwatapeli mamilioni ya fedha waumini wake kwa kisingizio cha kuziombea fedha ili kuondoa mikosi kwa kuzifanyia ibada ya utakaso. Uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa ibada katika kanisa hilo, inafanyika ili  kuwaombea watu wenye matatizo ya fedha na magonjwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, fedha zinazoletwa kwa ajili ya kuombewa, zinawekwa kwenye sanduku maalumu linaojulikana kuwa ni sanduku la agano na baadaye kuombewa kwa muda kabla kuzirejesha  kwa muumini.
  Mmoja wa waumini waliodai kuibiwa fedha zao, kwa njia hiyo na  ambaye hakutaka jina ake litajwe gazetini, alidai kuwa analidai kanisa Sh20 milioni, alizozitoa kwa nyakati tofauti ili ziombewe.

“Nilimpa mtumishi fedha  ili aziombee na kuzifanyia utakaso kwa sababu alisema mara nyingi fedha tunazotumia zina mashetani,” alisema muumini huyo ambaye ni mwanamke.

 “Unajua kuna wakati mtu unafanya biashara lakini, haitoki, hupati faida, sasa watumishi wa Mungu wanasema kunakuwa na mikosi kama vile chuma ulete. Ndiyo maana nilimkabidhi aziombee,”  alisema.
 “Mara ya kwanza nilipojiunga nilitoa Sh 600,000 ambazo aliziombea na baada ya miezi minne alinirudishia. Mara ya pili nilikuwa nasafirisha mzigo wa thamani ya Sh 7.5 milioni kwenda Zimbabwe. Siku hiyo walikuja dukani kwangu Kariakoo na kuniambia kuwa itabidi nitoe fungu la kumi la mzigo huo yaani Sh750,000 ambazo hata hivyo, walisema watanirudishia,” alisema.

  “Kwa kuwa sikuwa na fedha hizo nililazimika kukopa nikijua kuwa watazirudisha kabla sijasafiri. Kesho yake nilipozifuatilia Mlandizi nikakuta wamesafiri kwenda Moshi, ila wameniachia Sh 75,000 wakisema hilo ndiyo fungu la 10 langu.”

Alisema  kiongozi huyo wa kanisa na wenzake walimpa masharti ya kutoa ‘chenji’ fedha atakazopata faida isipokuwa nauli, pesa ya kulipa hoteli na ya chakula tu.  Alidai kuwa alipotoka Zimbabwe, watumishi hao walimpigia simu wakimtaka akutane nao Makambako, mkoani Iringa kwa madai kuwa Roho Mtakatibu amewaagiza wakafanyie ibada katika mji huo.
  Alisema ingawa ya hakuwa na fedha za Kitanzania lakini kwa faida ya Dola 4,800 alizopata kwenye biashara zake, aliwatii na kushukia Makambako.

“Pale Makambako ndiyo nyumbani kwa wazazi wa huyo mtumishi, tulifanya ibada kuanzia saa saba usiku. Wakaniambia nitoe fedha zote nilizonazo ili waziombee. Nikamwambia itabidi azirudishe mapema kwa sababu nilikuwa na order ya kupeleka mzigo nchini Zambia. Akasema atazirudisha mapema,”  alidai muumini huyo.

Alidai kuwa walikaa Iringa kwa muda wa siku tatu na kwamba waliporudi Dar es Salaam, mtumishi alianza kumzungusha licha ya kukumbushwa kila mara. “Badala ya kurudisha fedha kama tulivyokubaliana, alinipigia simu akisema twende kwenye maombi Mlandizi saa saba usiku. Huko tena akasema zile fedha itabidi ziombewe kwa siku saba zaidi. Siku saba zilipokwisha bado alisema ameambiwa na Roho Mtakatibu kuwa fedha zikae kwenye Sanduku la Agano kwa siku 21 zaidi,” alidai.

 Alidai kuwa wakati wakiendelea kusubiri siku hizo, mtumishi alimshauri asiendelee tena kufanya biashara.
Kwa mujibu wa mtu huyo, pamoja na  kuzungushwa lakini bado aliendelea kumwamini mtumishi kiasi cha kumpa fedha nyingine alizotaka.

 Alisema kijana mmoja wa Kitanzania anayeishi naye  alitaka kufanyiwa maombi ili mambo yake ya mwendee vizuri na kwamba yeye alimshawishi aje kufanyiwa maombi kwenye kanisa hilo.
“Yule kijana akaja kutoka Zimbabwe kwa ajili ya maombi hayo Siku hiyo mtumishi alikuja nyumbani Kinondoni. nikamtambulisha mgeni wangu kwake. Baada ya kusalimiana, alimwita kisha akamuuliza, una fedha hapo mfukoni. kijana akasita kwanza halafu akaja nje kuniuliza, ‘huyo mama anauliza kama nina fedha mfukoni lakini nimeshindwa kumjibu’. Mimi nikamwambia ampe tu” alisema.

  Kwa mujibu wa muumini huyo, kijana huyo alikuwa na a Dola 5,900 na Randi 1,000 ambazo zote aliamriwa kumkabidhi mtumishi kwa maelezo kwamba zinakwenda kuombewa na baadaye kurejeshwa.
Taratibu za ibada Habari zimeeleza kuwa ibada katika kanisa hilo inategemea uongozi wa Roho Mtakatifu na hakuna ratiba maalumu.

Mmoja wa wawatumishi wa kanisa hilo (jina tunalo), alisema hakuna ratiba maalumu hadi pale roho wa bwana atakavyowaambia.

 “Hii ni huduma ya maombezi ambayo ukija hapa, tunakuuliza mahitaji yako, kisha tunakufanyia maombi. Unajua sisi hatuombi kama makanisa mengine. Tunafuatilia mzizi wa tatizo la mtu tangu kizazi cha kwanza. Kama wewe hukufanya matambiko na maagano, inawezekana wazazi wako au hata babu zako. Hayo yote tunayavunja kwa jina la Yesu. Muda wa maombi utategemea uzito wa tatizo,” alisema Kuhani huyo.

Baadhi ya watu walioko  karibu na kanisa hilo, walisema  misururu ya magari imekuwa ikufurika ikiwa na watu wanaofanya ibada katika kanisa hilo hasa nyakati za usiku.

  “Hapa kila siku wanakuja matajiri na magari yao ili kuombewa na mara nyingi ibada zinafanyika usiku,” alisema mwana kijiji ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.   Siku ya maombi  Akisimulia jinsi ibada ya kumwombea kijana huyo ilivyofanyika, mwanamke huyo alisema waliandaa mbuzi, maziwa, pombe ya mbege, mvinyo, vitambaa vya rangi mbalimbali, mtama na ulezi.

“Alisema vitu vyote hivyo ni kwa ajili ya kutengua laana alizowekewa na mababu zake. Ibada ilifanyika usiku wa manane huku yule kijana akiogeshwa kwa mvinyo, uliochanganywa na damu ya mbuzi na sarafu za amani huku akiombewa. Baadaye vile vitu vilichanganywa na biblia mpya na kufukiwa kwenye shimo. Yule kijana alioga na kwenda kupumzika. Hata hivyo, ibada iliendelea kwa siku tatu.”  Alisema  baadaye kijana aliambiwa asubiri kwa muda wa siku 21 ndipo akachukue fedha zake huku akitakiwa kujitakasa ndani ya siku hizo, lakini hadi sasa hajapata fedah hizo.

  Sanduku la agano Kwa mujibu wa mwanamke huyo, baada ya kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Oysterbay na Polisi Mlandizi, alipewa ushirikiano iliowezesha kumkamata huyo mtumishi huku wakifuatilia kilichomo ndani ya Sanduku la Agano. “Siku hiyo tulikwenda na polisi kwenye kanisa hilo usiku, wakalitafuta bila mafanikio. Ikabidi waondoke. Ila wakati tunaondoka nilitumiwa ujumbe mfupi na mmoja wa waumini kuwa limefukiwa karibu na madhabahu.

Alisema siku iliyofuata polisi walilifukua na kulipata na kwamba walipolifungua walikuta bahasha nyingi, msalaba, Biblia, kitabu cha Tenzi za rohoni na fimbo.

Muumini mwingine wa kiume, ambaye pia ni mfanyabiashara naye alidai kutapeliwa Sh1.2 milioni alizoambiwa kuwa ni kwa ajili ya ‘Baraka za Ibrahim’ yaani makabila 12 ya Israel.

Madai hayo pia yanaungwa mkono na mwanamke mwingine anayeishi Sinza jijini Dar es Salaam, akisema aliwahi kutoa kama kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kupata ‘Baraka za Ibrahim’ lakini, hajazipata hadi leo.
  Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, ‘Kuhani’ huyo hakupatikana na hata namba za simu zote anazotumia hazikupatikana.

RPC Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Evarist  Mangu, alikiri kufahamu tuhuma hizo, akini aisema maelezo kamili atayatoa baadaye.  Ofisa Upelelezi wa  Makosa ya Jinai wa mkoa huo, Evance Mwijage, amekiri kulifuatilia sakata hilo na kwamba  polisi wanalishikilia sanduku hilo la agano kama ushahidi katika  tuhuma hizo. .  Mwisho

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.