SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuibua upya mjadala wa posho za wabunge zilizokuwa zimepandishwa kinyemela kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 kwa kila kikao, akisema nusu ya wabunge walitishia kuachia ngazi kutokana na hali ngumu inayowakabili, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amemjibu akisema wanaotishia wangepaswa kujiondoa mapema.
Akihutubia wapigakura wake jimboni Njombe Kusini, mkoani Iringa, mwishoni mwa wiki, Spika Makinda, alisema sasa hivi nusu ya wabunge wanataka kuondoka kwenye ubunge lakini akawaambia hawawezi kwani watasababisha hasara nyingine ya gharama za kurudia uchaguzi.
Makinda aliongeza kuwa miaka 10 kuanzia sasa, mtu yeyote mwenye shughuli yake, hatagombea ubunge kwa sababu ni eneo la umaskini wa kutupwa kabisa.
Kauli hiyo ya Spika ilipingwa vikali na Zitto, akisema kuwa kwanza hana uhakika kama ni kweli wabunge wametaka kujiuzulu kwa kuwa posho ni ndogo.
“Hao wanaotaka kujiuzulu kwa sababu ya posho hawakuwa wabunge, wangepaswa wajiondoe mapema,” alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na mmoja wa wabunge walioko mstari wa mbele kupinga nyongeza ya posho hizo, alipotakiwa na gazeti hili kutoa msimamo wake.
Zitto alifafanua kuwa ni bora kuwa na gharama za uchaguzi mdogo kuliko kuwa na wabunge wanaojadili posho badala ya kazi kwa wananchi.
“Sijamwona mama Makinda ila kama kasema hivyo kweli na kama ni kweli wabunge walitaka kuachia ngazi, basi namlaumu sana kung’ang’ania wabunge kuongezwa posho,” alisema.
Kuhusu madai ya Spika Makinda kuwa wabunge wenzao wa mabunge ya mataifa jirani ya Kenya, Uganda na kwingineko wanawashangaa wanaishije kwa mishahara midogo, Zitto alisema hiyo si hoja ya wabunge wa Tanzania kulipwa mishahara midogo kwani uchumi wetu si sawa na ule wa mataifa mengine.
Mjadala wa posho ulizusha kauli tofauti baina ya viongozi ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, awali alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete amemwachia mafaili ya mapendekezo ya posho mpya ili aziidhinishe na baadaye alikuja na kauli nyingine kwamba tayari Rais alishasaini posho mpya.
Wakati Waziri Mkuu Pinda akitoa kauli hiyo, Spika Makinda aliibuka na kusema kuwa posho hizo zimeongezwa na tayari zimeanza kutolewa kwa wabunge kutokana na baraka za Rais Kikwete.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ikisema kuwa Rais Kikwete hakuwahi kuidhinisha posho hizo bali aliwatangazia wabunge watumie busara katika hoja hiyo, lakini mwisho kabisa, Naibu Spika,
Job Ndugai alinukuriwa akisema posho hizo hazitapanda tena.
Tanzania daima
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.