Release No. 027
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 20, 2012
SH. 2,000 KUONA MECHI YA STARS, DRC
Kiingilio kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika Februari 23 mwaka huu kitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya kijani na bluu.
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo viti hivyo vya kijani na bluu vinachukua watazamaji 36,693 ambayo ni karibu theluthi mbili ya viti vyote kwenye uwanja huo wa kisasa.
Viti vya rangi ya chungwa kiingilio ni sh. 5,000, VIP C itakuwa sh. 7,000 wakati VIP B tiketi zitauzwa kwa sh. 10,000. Kiingilio kwa viti vya VIP A kitakuwa sh. 15,000.
Kwa vile Februari 23 mwaka huu ni siku ya kazi ili kutoa fursa kwa washabiki wengi kushuhudia pambano hilo la kimataifa, mechi hiyo itaanza saa 11 kamili jioni.
Wakati Taifa Stars inayofundishwa na Jan Poulsen imeingia kambini leo na ikitarajiwa kuanza mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Karume, DRC ambayo iko chini ya kocha Claude Le Roy inatarajia kutua nchini kesho.
Taifa Stars na DRC zinatumia mechi hiyo kunoa wachezaji wao kabla ya mechi zao za mchujo za Kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Katika raundi hiyo ya awali ambayo mechi zake zitachezwa Februari 29 mwaka huu, Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Msumbiji wakati DRC inaanzia ugenini dhidi ya Seychelles.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.