Huwa tunapewa kadi kadhaa kwa wiki au kwa mwezi zikiwa ni kadi za harusi. Tunatakiwa kuwachangia watoto, ndugu, jamaa na marafiki zetu ambao wanataka kuoa au kuolewa.
Tunatakiwa kuchangia kiasi fulani ambacho kama kisipotimia, sharti ni kwamba hatutapewa kadi kuhudhuria harusi hizo.
Umeshawahi kwenda kwenye kumbi za burudani na hasa muziki? Kama umeshaenda ni kwamba huruhusiwi kuingia kwenye kumbi hizo hadi uwe na tiketi, kwa maana kwamba uwe umelipa Kiingilio.
Kuna tofauti gani kati ya kulipa kiingilio cha ukumbi wa burudani ili kuona kinachoendelea humo na ile ya kutoa mchango ili upewe kadi ya kuhudhuria kwenye harusi?
Ukweli ni kwamba hakuna tofauti kati vitu hivyo. Vyote ni biashara inayohusu burudani.
Hebu fikiria umeingia ukumbini ukijua kwamba kikundi fulani cha muziki ndicho kitakachokuwa humo, badala yake unakwenda kukutana na kikundi kingine kabisa. Ni wazi labda tu uwe umekipenda hicho kikundi kingine ambacho hukukitarajia, vinginevyo unaweza kudai urudishiwe fedha zako, au utalalamika sana kwamba hukutendewa haki.
Je hujawahi kwenda kwenye harusi ambayo chakula kimekuwa kidogo au kisichopendeza?
Je hujawahi kwenda kwenye harusi ambayo vinywaji kama bia havikuwa vingi kwa mujibu wa matarajio ya washiriki?
Kama umewahi kwenda, naamini utakubaliana na mimi kwamba lawama na malalamiko, utakayoyasikia hayana tofauti na yale ya kwenye ukumbi ambao kimekuja kikundi tofauti na kile alichotarajia mhusika. Hizi zote ni biashara na walioingia humo wameingia kutokana na kile walichochangia.
Siku hizi michango ya harusi imeondoka kutoka kwenye utaratibu wake wa asili ambapo mtu huchangia kile alichonacho na sasa imeingia mahali ambapo ni kero dhalilisho na chanzo cha kuvunja uhusiano miongoni mwa watu.
Kuchangia harusi kwa sasa ndio shughuli inayoongoza katika kuwa na harambee nyingi na zenye kudhalisha zaidi katika jamii kwa upande wa mijini.
Uchunguzi usio rasmi nilioufanya hapa jijini Dar es salaam umeonesha kwamba kwa watu wenye kipato cha kati na cha juu kwa wastani kila mmoja hupokea kadi kati ya tatu hadi tisa za michango ya harusi kwa mwezi.
Nilikuja kugundua kwamba kiwango cha kuchangia kimepanda kutoka wastani wa shilingi 10,000 kwa kadi hadi shilngi 20,000.
Kati ya kadi hizo tisa imebainika kwamba, ni mbili tu ndizo ambazo ni za watu wa karibu wa mchangiaji, nne ni za ndugu wa mbali, mbili ni za ndugu asiowajua na moja ya mtu ambaye hana udugu wala ujamaa naye, bali ni ndugu au jamaa wa huyo aliyempa kadi hiyo.
Nimezidi kubaini kwamba kuna watu ambao hugawa kadi za michango za jamaa zao wa mbali kama kisasi au hasira kwa kuwa wamechangia harusi nyingi sana za wengine wakati wao hawana watoto, ndugu au jamaa wa karibu ambao wanahitaji au watahitaji kuchangiwa karibuni.
Ili angalau kupoza maumivu kidogo, huamua kuvalia njuga harusi za jamaa wa mbali ili kujaribu kujipa ahueni ya kule kuchangia kwake kusiko na faida.
Hii ni dalili ya wazi kwamba wengi wanaochangia sherehe za harusi hawafanyi hivyo kwa kupenda bali kutokana na shinikizo la kijamii.
Ukweli ni kwamba michango ya harusi imezidi kuwa kero na kisirani kwa jamii, kiasi kwamba hata wanaotoa kadi hizo kwa watu huhisi kushtakiwa na dhamira kwa sababu wanajua kwamba wanaowapa kadi hizo hawapendi kuzichangia.
Tukumbuke kuwa gharama za ndoa haziwezi kuzidi shilingi 50,000. Kinachotakiwa ni fedha za kumlipa mfungisha ndoa na nauli ya kuwatoa bwana na bibi harusi kutoka kwenye eneo la tukio na kuwapeleka nyumbani.
Kwa bahati mbaya sana, kumekuwa na tatizo la kuchanganya kati ya harusi na ndoa. Kwa wengi harusi ambazo ni sherehe, kinaonekana ndio kitu muhimu na kikubwa kuliko ndoa.
Na harusi sasa zimegeuka pia kuwa ni uwanja wa kuoneshana uwezo wa kipato.
Kwa mtu ambaye ana ufahamu, hawezi kuendeshwa na kupangiwa maisha na kadi za michango. Kama una uwezo wa kuchangia una haki ya kuchangia kwa maana ya kusaidia na unaweza kuchangia kiasi chochote.
Lakini kama huna uwezo, huna sababu ya kuumia kwa kujiuliza kuwa utaeleweka vipi usipochangia.
Anayegawa kadi na kutangaza kwamba kima cha chini ni shilingi 20,000 ndiye anayepaswa kuona aibu kwa sababu anajaribu kufanya ujambazi kwa njia ya kiungwana.
Habari ndio hiyo!!!!!!!!!!
Jisikie huru kabisa kuchangia lolote linalohusiana na jamii, uchumi, siasa, imani na elimu katika Blog yetu. Tunakaribisha habari, taarifa, picha za matukio, maoni na ushauri ili kuwekana sawa katika dunia yetu hii ndogo. Wote mnakaribishwa katika kuimarisha mshikamano wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini mwetu!!
Pages
Forums
- Critical Analysis (11)
- Education Issues (15)
- Geology and Mining (21)
- International News (37)
- National News (147)
- Political Issues (67)
- Religious Issues (28)
- Social Issues (79)
- Sports (19)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.