Na Richard Bukos
AMA kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Usemi huu unakamilishwa na tukio la hivi karibuni ambapo msichana aliyefahamika kwa jina la Mwanahamisi Hamis, mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam na wenzake wawili, Salima Juma na Halima Amir, walipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar na kusomewa shitaka la kunaswa sehemu ya wazi wakidaiwa kujiuza.
Wakati kesi ikiendelea, ilibainika kuwa Mwanahamisi ni Bi. Harusi mtarajiwa na vikao vya harusi vilikuwa vikiendelea huku ndoa yake ikitarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu, takribani saa 120 kuanzia leo.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Richard Magodi, mnamo Februari 16, mwaka huu, majira ya saa saba usiku, washitakiwa hao walikamatwa maeneo ya Buguruni wakifanya vitendo haramu vya ukahaba.
Washitakiwa wote walikiri kutenda kosa hilo lakini walimuomba hakimu anayesikiliza kesi yao, Timothy Lyon awasamehe kwa vile ilikuwa mara yao ya kwanza kufikishwa mahakamani hapo kwa kosa hilo.
Pamoja na ombi hilo, mwendesha mashitaka Magodi alimuomba hakimu kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye vitendo kama vyao.
Baada ya msumari huo wa mwendesha mashitaka, hakimu aliahirisha kesi hiyo na kuwanyima dhamana washitakiwa mpaka Februari 20 (leo).
Hata hivyo, Mheshimiwa Lyon alimhukumu mshitakiwa Salima Juma kwenda jela miezi 6 kufuatia kuonesha utovu wa nidhamu mahakamani pale alipomtaka hakimu atengue maamuzi ya awali.
Kifungo hicho kilimfanya Salima kuangua kilio akiwa haamini masikio yake.
Wakati huo huo, watu waliodaiwa kuwa ni miongoni mwa wanakamati wa harusi ya Mwanahamisi walionekana wakihaha mahakamani hapo kumnasua Mwanahamis kwenye aibu baada ya hakimu kuwanyima dhamana.
“Hii sasa aibu jamani, yule Mwanahamisi ni Bi. Harusi mtarajiwa, badala ya kutulia nyumbani anazurura hovyo usiku wa manane mpaka anafedheheka kiasi hiki,” alisema mwanamke mmoja aliyedai ni mwanakamati wa harusi hiyo.
Hata hivyo, mwanamke huyo alifunga ‘bakuli’ lake kufuatia kugundua kwamba alikuwa akihojiwa na paparazi wa gazeti baada ya kujitambulisha kwa ajili ya kupata data zaidi za harusi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.