Patricia Kimelemeta na Fidelis Butahe SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kudai Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe hajalishwa sumu, kiongozi huyo ameibuka na kusema amekerwa na jeshi hilo kutoa taarifa za uongo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuingilia utaratibu wa matibabu bila ya idhini yake. Mwakyembe alifafanua kuwa sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, bali inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa na kusisitiza kuwa, aliwahi kulieleza jeshi hilo kwamba kuna kundi limejipanga kumdhuru, lakini lilifanya mzaha. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, alisema tangu alipoanza kutumiwa ujumbe wa vitisho na wabaya wake aliowaita ni mafisadi mwanzoni mwa mwaka jana, alikuwa akitoa taarifa kwa jeshi hilo, lakini mpaka sasa limeshindwa kuwachukua hatua zozote. Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe inafuatia Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai(DCI), Robert Manumba kuwaeleza waandishi wa habari juzi kwamba wananchi wanatakiwa kupuuza madai yaliyotolewa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwa Waziri Mwakyembe amelishwa sumu. DCI Manumba alieleza kuwa waliwasiliana na Wizara ya Afya ili kubaini chanzo cha ugonjwa wa Naibu Waziri huyo, lakini taarifa iliyowasilishwa na wizara hiyo kwa Jeshi la Polisi imeonyesha kuwa, hajalishwa sumu. Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mwakyembe alisema anapata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yake, au walisoma taarifa nyingine na kama waliisoma, taarifa hiyo wenyewe ama walisomewa. Katika taarifa hiyo, alisema alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo ya nchini India anakotibiwa. “Ripoti inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow (ndani ya ute wa mifupa) kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua,” “Lakini vyombo vyetu vya dola vinapelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu kwamba ‘sikulishwa sumu’, sikulishwa sumu,” alisema Mwakyembe katika taarifa hiyo. Aliongeza kuwa,“Nimelazimika leo Jumamosi (jana) kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari uliofanyika jana (juzi) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa, “sikunyweshwa sumu”. Mwakyembe alisema taarifa hiyo ya DCI Manumba imeshindwa kufafanua ugonjwa wake wa ngozi umesababishwa na nini. Waziri huyo alisema msimamo huo wa Jeshi la Polisi umemkera katika hali aliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yake na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea Hospitali ya Apollo ambako bado anatibiwa. Alisema kuna ufinyu wa uelewa uliojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi uliosisitiza kuwa ’hakunyweshwa sumu’ wakati sumu si lazima unyweshwe ili imdhuru mtu, bali inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa. Waziri huyo alisema kuwa ni hatari kwa Jeshi hilo kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini. Alifafanua kwamba Februari 9, mwaka jana, alimwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Said Mwema, kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yake na ya viongozi wengine. Alisema kuwa kwa kutambua kuwa Polisi wa Tanzania husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo wafanye kazi, alihakikisha ameainisha katika barua hiyo kila ushahidi alioupata au kupewa. Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema anashangazwa na utaratibu unaotumiwa na Jeshi hilo wa kusubiri ushahidi mezani bila ya kuchunguza na kuwafananisha na mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani. Alisema utaratibu huo haupo popote duniani ila ni Tanzania peke yake, kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. “ Polisi duniani kote wanachohitaji ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika,” Mwakyembe alisema katika taarifa hiyo. Naibu waziri huyo alisema pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi aliokuwa nao, yapo mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo. Mambo manne Akifafanua mambo hayo katika taarifa hiyo, alisema siku chache baada ya kumkabidhi IGP Mwema barua hiyo, alitumiwa timu ya wapelelezi ofisini kwake ili kuchukua maelezo yake ya ziada. Alifafanua kuwa timu hiyo ilikuwa inaongozwa na Ofisa wa polisi ambaye wiki chache zilizopita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia dawa za kulevya mtoto wa mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini, suala alilodai kuwa mpaka sasa uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Alisema kwa msingi huo, aliona ameletewa mtuhumiwa wa rushwa na ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi jambo ambalo haliwezekani na kwamba suala lake limefanyiwa mzaha. Mwakyembe alisema wiki chache baada ya barua yake kuwasilishwa kwa IGP na timu ya polisi kuanza kazi, Jeshi hilo likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari aliowatuhumu kushirikiana na majambazi. “Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza,”ilibainisha taarifa hiyo. Alisema tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari, wale aliowatuhumu kwenye barua yake, walihamishiwa mikoa mingine. Mwakyembea alisema ili kumkatisha tamaa kabisa, barua yake ya ‘siri’ kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari iliyokebehi na kukanusha taarifa nzima aliyoitoa “Sijui kwa faida ya nani,” alihoji katika taarifa hiyo na kuongeza, “ Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa Jeshi la Polisi. Akitoa mfano wa Waziri Sitta, kuwa hivi karibuni, kiongozi huyo alihojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, lakini taarifa ya mahojiano ikaonekana kwenye moja ya magazeti, ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta na kubainisha kuwa uadilifu wa uongozi wa Jeshi la Polisi, umefikia pabaya. Mwakyembe alisema, katika barua yake kwa IGP alieleza kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kumuua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wao. Waziri huyo alieleza kushangazwa na msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama alipewa sumu au la na kuamua kutoa tamko hata kabla ya kumchunguza alivyo. Alisema polisi hawajawahi kumhoji yeye wala wasaidizi wake ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaomfanyia uchunguzi nchini India. Waziri huyo aliwashangaa polisi badala ya kumshukuru, Waziri Sitta kwa sababu amekuwa akiwapa tahadhari kuhusu afya yake ili suala hilo lichunguzwe kwa kina, badala yake sasa anaonekana adui wao. “Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa Sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua,” alilalamika katika taarifa yake hiyo. Alisema viongozi hao wanajua kuwa hawezi kukaa kimya au kumung’unya maneno pale anapoona haki inakanyagwa bila ya kujali matokeo ya uamuazi huo. Katika taarifa hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka Watanzania kuombeana afya na uhai ili waweze kutenda haki na waendelee kuitetea nchi yao ikiwemo kumalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA na Kagoda kwa maslahi mapana ya Taifa. Historia ya ugonjwa wa Mwakyembe Dk Mwakymbe alianza kuumwa Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa nchini India na kulazwa katika Hospitali ya Apollo kwa matatibu. Alirejea nchini Desemba 11, mwaka jana baada ya kulazwa hospitalini humo kwa takribani miezi miwili. Msemaji wa familia ya Dk Mwekyembe na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, alisema baada ya mbunge huyo kurejea nchini, afya yake ni njema ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitali. Kauli za Waziri Sitta Mara kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu. Akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, jijini Dar es Salaam Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema: “ Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka,” alisisitiza Waziri Sitta katika hafla hiyo. Sitta alihoji “ Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida.” Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote. Waziri Nahodha Akijibu moja ya kauli hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nohodha alimtaka Waziri Sitta awasilishe ushahidi wake ili ufanyiwe kazi badala ya kuzungumza nje ya vyombo vya sheria. Hata hivyo, Sitta alisema hatapeleka ushahidi wa madai aliyotoa kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wanao ushahidi. Alisema wanachotakiwa kufanya Polisi ni kufanya uchunguzi kuhusu madai hayo ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu kwa kuwa ushahidi wanao na wasianze kurushiana mpira. “Waziri Nahodha anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa zilishapelekwa polisi, anataka mimi nitoe ushahidi gani?” Alisema Waziri Sitta. www.mwananchi.co.tz |
Jisikie huru kabisa kuchangia lolote linalohusiana na jamii, uchumi, siasa, imani na elimu katika Blog yetu. Tunakaribisha habari, taarifa, picha za matukio, maoni na ushauri ili kuwekana sawa katika dunia yetu hii ndogo. Wote mnakaribishwa katika kuimarisha mshikamano wa kuleta mabadiliko ya kweli nchini mwetu!!
Pages
Forums
- Critical Analysis (11)
- Education Issues (15)
- Geology and Mining (21)
- International News (37)
- National News (147)
- Political Issues (67)
- Religious Issues (28)
- Social Issues (79)
- Sports (19)
Sunday, February 19, 2012
Mwakyembe awasha moto
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.