Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Friday, March 2, 2012

Dk. Shein azindua mradi wa matumizi ya teknolojia uliofadhiliwa na wamarekani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,(katikati) na Balozi wa Marekani Nchni Tanzania Alfonso Lenhardt,(katikati) wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Elimu wa Karne ya 21,unaohusiana na Elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Skuli za Msingi hapa Zanzibar,unaofadhiliwa na Shrika la Misaada la Marekani USAID,(kulia) ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akizungumza na Wananchi,Walimu na Wanafunzi,wakati uzinduzi wa Mradi wa Elimu wa Karne ya 21,unaohusiana na Elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Skuli za Msingi hapa Zanzibar,unaofadhiliwa na Shrika la Misaada la Marekani USAID,katika Skuli ya Mwanakwerekwe C,(katikati)Balozi wa Marekani Nchni Tanzania Alfonso Lenhardt, na (kulia) Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Maalim Seif Sharif.
Balozi wa Marekani Nchni Tanzania Alfonso Lenhardt,akitoa hutuba yake wakati wa ktika picha ya pamoja na Viongozi wengine na wanafunzi wakati uzinduzi wa Mradi wa Elimu wa Karne ya 21,unaohusiana na Elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Skuli za Msingi hapa Zanzibar,unaofadhiliwa na Shrika la Misaada la Marekani USAID,katika Skuli ya Mwanakwerekwe C.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,na Balozi wa Marekani Nchni Tanzania Alfonso Lenhardt,wakinyanyua kompyuta iliyotolewa zawdi na Balozi wa Marekani,wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Elimu wa Karne ya 21,unaohusiana na Elimu ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano kwa Skuli za Msingi hapa Zanzibar,unaofadhiliwa na Shrika la Misaada la Marekani USAID,uzinduzi huo ulifanyika janakatika Skuli ya Mwanakwerekwe C.
 

Mkurabita Wamuaga Mtumishi Wao

 Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA na Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda akihutubia jana jijini Dar es salaam wakati wa halfa fupi ya kumuaga aliyekuwa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za WanyongeTanzania(MKURABITA) Mhandisi Ladislaus Lema baada kustaafu rasmi Desemba 2011.
 Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za WanyongeTanzania(MKURABITA) Mstaafau Mhandisi Ladislaus Lema akitoa neno la shukurani jana jijini Dare s salaam wakati wa halfa fupi ya kumuaga baada kustaafu rasmi Desemba 2011 wakati wa sherehe fupi iliyoandaliwa na Ofisi ya MKURABITA.
 Mratibu wa MKURABITA akitoa neno la utangulizi jana jijini Dar es salaam wakati wa halfa fupi ya kumuaga aliyekuwa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za WanyongeTanzania(MKURABITA) Mhandisi Ladislaus Lema baada kustaafu rasmi Desemba 2011.
 Naibu Katibu Mkuu Ikulu Susan Mlawi akihutubia jana jijini Dar es salaam wakati wa halfa fupi ya kumuaga aliyekuwa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za WanyongeTanzania(MKURABITA) Mhandisi Ladislaus Lema baada kustaafu rasmi Desemba 2011
 Baadhi ya wafanyakazi Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za WanyongeTanzania(MKURABITA) wakitoa zawadi ya Komputya jana jijini Dar es salaam kwa aliyekuwa Mratibu wa MKURATIBA Mhandisi Ladislaus Lema baada kustaafu rasmi Desemba 2011.
Wakiwa katika picha ya pamoja
 Picha na Tiganya Vincent, Dar es salaam

Siyoi Ambwaga Tena Sarakikya



Waandishi Wetu, Arusha
KWA mara ya pili, wana CCM Jimbo la Arumeru Mashariki wamedhihirisha kuwa chaguo lao ni Siyoi Sumari baada ya kumchagua kwa kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, William Sarakikya aliyepata kura 361 katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.Matokeo hayo ni kama ushindi kwa mojawapo ya kambi ndani ya CCM inayohusishwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa dhidi ya wanachama waliopo katika makundi mengine, ambayo yalikuwa yakipinga kwa nguvu zote kupitishwa kwa jina la Siyoi.

Vyombo mbalimbali vya habari kwa wiki nzima sasa, vimekuwa vikiripoti kuhusu mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala kutokana kuwa na misimamo inayokinza kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo mdogo.

Siyoi alianza kuzua mtafaruku ndani ya CCM pale suala la uraia wake lilipozua utata ndani ya kikao cha Sekretarieti ya chama hicho, hivyo kusababisha kutolewa kwa mapendekezo kwamba aenguliwe katika kinyang’anyiro hicho.

Kundi linalomtetea limekuwa likilalamikia kile linachodai kwamba ni kuwapo kwa njama za kumtosa mshindi huyo kwa sababu kadhaa za kimakundi.

Hata hivyo, Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana chini ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kiliamuru kurudiwa kwa uchaguzi baina ya Siyoi na Sarakikya, kwa maelezo kwamba katika wagombea wote sita hakuna aliyekuwa amepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

Habari zaidi zilidai kuwa, hata baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo, mmoja wa vigogo wa CCM alituma mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu kwenda kumshawishi Siyoi ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho, jitihada ambazo hazikufanikiwa kwani alikataa.

Matokeo ya kura
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa Saa 11:30 jioni na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, Sumari aliibuka na ushindi huo wa silimia 67.8 kati ya kura halali 1,122 zilizopigwa, dhidi ya asilimia 32.2 za mpinzani wake anayedaiwa kupigiwa chapuo na viongozi wa chama na Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi taifa.

Jumla ya kura 1,124 zilipigwa ambapo mbili ziliharibika na kura halali kubakia 1,122.

Akitangaza matokeo hayo, Msekwa alilazimika kuanza kwa kumtangaza mshindi hali iliyofanya ukumbi kukosa usikivu kwa wapenzi, mashabiki na wafuasi wa Siyoi kuanza kushangilia.

Msekwa alisema ameridhishwa na upigaji kura na matokeo hayo yameonyesha imani kubwa waliyonayo wana Arumeru kwa mgombea huyo.

Baadhi ya wana CCM walidai kuwa kauli tata za Msekwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati katika ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa Wilaya ya Arumeru jana zilimponza, Sarakikya baada ya wajumbe kuamua kupiga kura za hasira wakipinga kile walichodai kushinikizwa kumchagua mtu aliyeelezwa anatakiwa na mfumo (system), wa Serikali na uongozi wa chama.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na idadi kubwa ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), maofisa usalama wa taifa na askari kanzu kutoka Jeshi la Polisi, Msekwa na Chiligati waliwataka wajumbe kutumia vyema kura yao kumchagua mtu atakayemudu na kuhimili vishindo vya upinzani kutoka vyama vingine vitakavyosimamisha wagombea.

“Ndugu wajumbe napenda kuwakumbusha jambo moja muhimu kabla ya kupiga kura, leo hatuchagui mbunge, mnachofanya ni kupiga kura za maoni. Mgombea atateuliwa na kikao cha Kamati Kuu Machi 3, mwaka huu,” alisema Chiligati.

Wakati Chiligati akisititiza hoja hiyo, Msekwa alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maneno aliyokuwa akiyasema Naibu Katibu Mkuu huyo huku baadhi ya wajumbe wakiguna.

Msekwa aliyetumia muda mwingi kuzungumzia historia yake ya uongozi ndani ya chama kuanzia TANU hadi CCM aliwataka wajumbe kutoangalia uswahiba wala ushawishi wa aina yoyote katika maamuzi yao bali wahakikishe wanayemchagua anastahili kupeperusha bendera ya chama hicho tawala na kukiletea ushindi.

Siyoi Sumari akiwa amebebwa na wafuasi wa CCM baada ya kuibuka mshindi wa kura za maoni za mgombea Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kupitia chama hicho, jana. Picha na Filbert Rweyemamu

Katika uchaguzi wa awali wa kura za maoni uliofanyika Februari 20, mwaka huu, Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari aliyefariki hivi karibuni aliongoza kwa kupata kura 361 akifuatiwa na Sarakikya alijinyakulia kura 259.

Wagombea wengine na kura walizopata katika uchaguzi wa awali kwenye mabano ni pamoja na Elirehema Kaaya (205), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Elishilia Kaaya (176), Antony Msami (22) na Elishiankira Urio aliyeambulia kura 11.

Msami tayari amehamia Chadema alikochukua fomu kuomba uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuambulia kura 8 katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho zilizopigwa juzi eneo la Maji ya Chai wilayani Arumeru.

Kamatakamata ya Takukuru
Katika hatua nyingine, kitendo cha kuwakamata baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho juzi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa lengo la kumsaidia mmoja wa wagombea jana kilibadilisha upepo miongoni mwa wapiga kura ambao wengi walidai kitendo hicho kililenga kumnufaisha mmoja wa wagombea na hivyo kuazimia kuonyesha hasira yao kwenye sanduku la kura.

Miongoni mwa viongozi na makada wa CCM aliyekamatwa kwa kudaiwa kujihusisha isivyo halali katika kampeni za Siyoi ni pamoja na Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kwa jina la ‘Askofu’ aliyesema baada ya kutiwa mbaroni kwa maagizo ya watu aliowaita wakubwa, alihojiwa kwanini anamfanyia kampeni mgombea huyo na aliyemtuma kufanya hivyo.

Ingawa kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto alikataa kuwataja viongozi wengine walioshikiliwa juzi kwa mahojiano, waandishi wetu waliofika ofisi za taasisi hiyo walimshuhudia mmoja wa waliogombea katika awamu ya kwanza ya kura za maoni pamoja katibu wa UVCCM katika moja za Wilaya za Mkoa wa Arusha wakihojiwa na maafisa wa idara hiyo ya dola.

Katika orodha hiyo pia walikuwapo madiwani wawili wa Kata za Arumeru na jana eneo lote la mkutano ulijaa maafisa wa Takukuru, na askari kanzu waliokuwa wakiranda kila kona na kujisogeza kwenye kila kundi la watu zaidi ya wawili walioonekana kuzungumza kwa lengo la kunasa mazungumzo yao.

Maofisa wa Takukuru jana waliendela na kamatakamata hadi muda mfupi kabla ya matokeo ambapo mmoja wa kada maarufu wa vijana wa CCM wilayani Arumeru, Ally Majeshi alitiwa mbaroni kwa mahojiano baada ya kudaiwa kutajwa na baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa juzi.

Shamrashamra
Baada ya matokeo, Siyoi alitoka ukumbini akiwa amebebwa juu juu na wafuasi wake kwa umbali wa zaidi ya kilomita mbili huku watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Sarakikya wakiwa wamebaki eneo la ukumbi wa mkutano katika makundi wakijadiliana.

Akizungumzia matokeo hayo, Sarakikya alikubali kushindwa na kumpongeza mgombea mwenzake akimtakia kila la kheri katika uchaguzi ujao wakati mshindi akiwashukuru wajumbe kwa imani waliyoonyesha kwake akiwataka kuanza kampeni za kutafuta ushindi wa CCM.

HALI YA VENGU BADO NI MBAYA DUA ZAIDI KWA WATANZANIA

Na Waandishi Wetu
TAARIFA zilizotua kwenye dawati la gazeti hili kutoka nchini India juu ya hali ya mchekeshaji maarufu wa Kundi la Orijino Komedi, Joseph Shamba ‘Vengu’ zinatoa machozi kufuatia maelezo kwamba hali yake bado ni tete.
Mtanzania mmoja aishiye nchini humo anapotibiwa Vengu katika Hospitali ya Apollo, aliyejitambulisha kwa jina la Japhet Kris alilitumia gazeti hili barua-pepe akieleza kuwa, msanii huyo bado hali yake si shwari licha ya kwamba jitihada zinafanywa na madaktari kuokoa uhai wake.
“Nilipata fursa ya kwenda kumuona Vengu kwenye Hospitali ya Apollo, kwa kweli hali yake bado siyo nzuri ingawa kuna mabadiliko kidogo ya afya yake.
“Nilipomuona kwa kweli niliumia sana, nilikuwa na marafiki zangu Watanzania…tuliumia sana, hali yake inatia huruma sana kwa kweli.
“Nilijaribu kuzungumza na mmoja wa madaktari pale hospitalini akasema wanafanya wanavyoweza kuhakikisha anapona lakini kikubwa nawaomba Watanzania wenzangu walio huko nyumbani wazidishe maombi kwa Mungu hakuna linaloshindikana, atapona tu,” ilieleza sehemu ya ujumbe huo.

Ndugu wanasemaje?
Akizungumza na mwandishi wetu, ndugu mmoja wa Vengu aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa familia alisema: “Kuna ndugu yetu ambaye yuko kule anafuatilia kwa karibu matibabu yake (Vengu), juzi alitupigia simu na kutuambia kuwa amefanyiwa operesheni, kikubwa tuzidi kumuombea.”

Mama yake Vengu ana siri nzito
Huku kukiwa na madai kuwa mama yake, Bi. Hellen ana siri nzito juu ya

afya ya mwanaye, mambo ya kishirikina yakihusishwa, mama huyo alipatikana mwanzoni mwa wiki hii na kuelezea juu ya ishu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu Bi. Hellen alisema, kinachomsumbua mwanaye ni maradhi ya kawaida na wala siyo kwamba amerogwa kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodhani.
“Wapo wanaosema mwanangu amerogwa, ninachoamini ni kwamba anachougua Vengu ni maradhi ya kawaida hivyo wenye dhana hiyo potofu waachane nayo,” alisema mama huyo.

Ugonjwa wa Vengu
Mwishoni mwa mwaka jana, Vengu alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akikabiliwa na ugonjwa uitwayo kitaalam Brain au Cerebral Atrophy ambapo seli za kichwani hukosa mawasiliano na sehemu nyingine na mgonjwa kupoteza fahamu.
Hali ilipozidi kuwa tete, mchekeshaji huyo alipelekwa Hospitali ya Apollo nchini India kwa matibabu zaidi.

RAIS JK AWATETEA WANAISHI KUIZUNGUKA MIGODI

RAIS Jakaya Kikwete amewaagiza wawekezaji katika sekta za madini, gesi na mafuta, kuhakikisha misaada kwa jamii inayowazunguka inakuwa moja ya sera zao za kibiashara ili kutoa fursa ya wananchi kufaidika na rasilimali zao.

Akizindua Tuzo ya Rais kwa kampuni zinazojihusisha na sekta ya uziduaji juzi usiku Dar es Salaam, pia aliwaagiza wawekezaji hao wa ndani na nje, kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za Serikali kwa wakati bila kusukumwa.

“Cha msingi hapa ni kulipa kodi na jamii ifaidike na rasilimali zake na ninyi pia mfaidike na uwekezaji wenu,” alisema Kikwete na kuongeza kwamba iwapo kampuni hizo zitatekeleza masuala hayo zitafanya biashara zao ziwe endelevu zaidi.

Rais alisema kuwapo vurugu katika baadhi ya maeneo ya uwekezaji, kunachangiwa na wananchi kutoona faida kutokana na rasilimali zao na akaongeza kuwa iwapo wawekezaji watawajibika kwa jamii walimowekeza, kutakuwa na maelewano mazuri ya kibiashara baina yao.  

“Hii italeta maelewano mazuri kati ya wawekezaji na jamii katika maeneo mlimowekeza, la sivyo uhusiano unaweza kuwa mbaya na kuibuka misiguano mibaya katika masuala ya kibiashara,” alionya Rais na kutoa mfano kwa wazalishaji wa sukari wanavyoshirikiana na wakulima wadogo wa miwa katika maeneo yanayowazunguka.

Katika hotuba yake, Rais aliagiza pia kampuni za uwekezaji kuwa na sera za kununua bidhaa za nchini. Alisema kuna bidhaa na huduma ambazo zinapatikana nchini na hivyo kutokuwapo haja ya kuagiza nje. Alisema hiyo ni njia mojawapo ya kuwawezesha wananchi na kuinua uchumi wa mahali kuliko na uwekezaji.

Alitoa mfano alivyokwenda hoteli ya kitalii nchini na kukuta maji ya kunywa yanatoka nje ya nchi, jambo ambalo halikumfurahisha na akagoma kuyanywa. “Kwa nini muagize maji nje ya nchi wakati tuna Uhai, Ndanda, Kilimanjaro na Masafi? Haya mambo hayafurahishi wananchi,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Kuna bidhaa na huduma nyingi ambazo mnaweza kununua nchini na hii ni moja ya kukuza uchumi wa wananchi wetu.” Rais alisema utaratibu huu wa kampuni kushirikiana kiuchumi na jamii zinazozunguka miradi yao ya uwekezaji, utasaidia kuongeza ajira na kipato kwa jamii husika.

“Hii itawafanya watu wajihisi na wao ni sehemu ya umiliki na wana wajibu wa kulinda wawekezaji … lakini kama hilo halifanyiki, watu hawatafurahishwa na shughuli zenu za uwekezaji na matokeo yake hawatajali uwekezaji huo; hivyo nakuombeni suala hili mlitilie maanani.
“Watu watajiuliza wanapata nini, dhahabu yetu inachukuliwa, kampuni hizi zina misamaha ya kodi, lakini hata hawatuungi mkono kiuchumi kwa kununua bidhaa zetu. Hawatakuwa na chochote katika biashara hii,” alisema.

Eneo lingine ambalo Rais aliagiza wawekezaji walifanye kama sera yao ya uwekezaji ni kujenga uhusiano kati ya kampuni kubwa, ndogo na wananchi ambao wamo kwenye sekta inayofanana. Alisema ni wajibu wa kampuni kubwa za kigeni kusaidia ndogo za wananchi ili nazo zifanikiwe.


“Kampuni kubwa zitumie uchumi wao na maendeleo yao ya kiteknolojia, kusaidia kampuni ndogo za wananchi ili kuboresha na kuongeza uzalishaji. Ninaamini hii itaisaidia kupunguza wivu, misuguano na kuongeza urafiki na uhusiano mzuri,” alisema Rais Kikwete.

Mapema akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema sekta ya uziduaji imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto za namna wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji wanavyoweza kufaidika na miradi ya uwekezaji katika sekta hiyo.

“Tuzo ya Rais ambayo lengo lake ni kuhamasisha wawekezaji wawe karibu na jamii zinazowazunguka itakuwa inatolewa kila mwaka kwa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo katika sekta hii ya uziduaji,” alisema Ngeleja.

Tuzo hiyo imeandaliwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Jukwaa la Wadau wa Sekta ya Madini (MISF). MISF ni asasi ya faida na inahusisha kampuni ambazo zimesaini hati ya makubaliano (MoU) na Wizara ili kuwa na jukwaa lenye jukumu la utetezi wa sera, utafiti, elimu na namna ya kutatua migogoro kati ya wawekezaji na wanajamii.
Tuzo hiyo inatarajiwa kuhamasisha sekta za madini, gesi na mafuta kushirikiana na jamii katika kuboresha uchumi wa maeneo ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii ya maeneo husika.


Wanaume kujichubua hakuongezi ubora wa filamu

Shabani Matutu

KARIBUNI katika safu hii ya ‘Vunja vunja’ ambayo hukuijia kila Ijumaa ikiwa maalumu kwa ajili ya kuchambua filamu za nyumbani lengo likiwa kuboresha na kuzifanya zifikie levo za kimataifa.
Leo tumekuwa na mada ambayop nahisi itakuwa ikizungumzia kuhusu waigizaji wetu wa kiume takriban wote kuingia katika mkumbo wa kujichubua ngozi huku wengi wakidhani huenda kunaongeza ubora wa filamu.
Sababu kubwa ya kuandika mada hiyo imetokana na wimbi kubwa lililoibuka kwa wasanii wengi waigizaji wa kiume wa hapa nyumbani kutumia mkorogo maarufu kama ‘Karolaiti’.
Suala hili si geni kwa watazamaji wa tasnia hii ya filamu ambao wamekuwa mashuhuda wakiwashuhudia baadhi ya waigizaji walioanza wakiwa weusi tena wa kuvutia kuwatazama lakini hivi sasa wamejikoroga na kushindwa kuwatambua aina ya rangi zao kama ni weupe, njano au wekundu.
Kutokana na katabia hako walikojijengea wanaume kwa kufanya mambo ambayo hufanywa na mabinti imenifanya nikose uvumilivu kama mdau.
Swali jingine linaloniumiza kichwa kuhusu tabia hii ni kwamba, wanafikiria kwamba wanapojichubua ndipo filamu zao zitaongeza ubora au kupiga bao nje ya nchi?
Swali jingine ninalojiuliza ni kwamba wanafanya hivyo ili wawe kama Wazungu ambao ndio wamefanikiwa katika fani hii ya uigizaji?
Napenda kuwashauri kuwa kujipodoa hakukatazwi lakini kitu cha muhimu ambacho wasanii hawa wanapaswa kuangalia ni kuepuka kujichubua ngozi zao.
Pia wao kama kioo cha jamii wakumbuke kuwa mbali ya kwenda kinyume na tamaduni za mtoto wa kiume matumizi ya mikorogo ni hatari kwa ngozi ya binadamu.
Wasanii wa hapa nyumbani wanatakiwa kuachana na dhana mgando za kutumia mikorogo kwa kutaka pengine kufanana na Ramsey.
Si vibaya kwa mtoto wa kiume kujipamba lakini si busara wala hekima kwa mwanamume kujichubua ngozi yako.
Waigizaji wa hapa nyumbani wanatakiwa wajifunze madhara ya kujichubua kupitia kwa mfalme wa Pop duniani, Michael Jackson kwa yaliyompata ya ngozi kutoka.
Wanachopaswa kujua wasanii wetu ni kwamba kuiga mambo yanayoelimisha ambapo pia hayaathiri mila na tamaduni zetu hakuna wasiwasi.
Kinachosikitisha ni kwa wasanii hawa kupenda kuiga bila kujua faida au athari ya kile anachoiga kutoka kwa mastaa mbalimbali duniani.
Wasanii hao wanachotakiwa ni kujali kufanya kazi kwa bidii kitendo ambacho kinaweza kuwaletea umaarufu katika fani hiyo.
Kuna nyota kama Danzel Washington, Bill Branks wamefanikiwa kupata umaarufu sana katika tasnia hiyo wakiwa na ngozi zao za asili sasa kama ubora ungekuwa unapatikana katika kubadili rangi wangefanya hivyo kwa kuwa kwao ni bei rahisi.

JK: Nilisaini Sheria ya Katiba kuepuka hasira za wabunge

Rais Jakaya Mrisho Kikwete



Raymond Kaminyoge
RAIS Jakaya Kikwete amesema alisaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kukwepa hasira za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete alitoboa siri hiyo katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari aliyoitoa juzi kupitia vyombo vya habari.Uamuzi huo wa Rais kutia saini muswada huo ambao tayari ulikuwa umepingwa kila kona ya nchi licha ya kupitishwa na Bunge, ulizidi kuibua hasira za makundi mbalimbali ya kijamii.

Rais wakati akisaini muswada huo, Novemba mwaka jana, alikuwa ameanza  mazungumzo na makundi  ya  kijamii ukiwamo ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).   

Lakini, mwenyewe akifafanua ni kwa nini alisaini muswada huo wakati ulikua ukipingwa na wananchi na huku akiwa katika mazungumzo na wadau, ndipo alisema, “Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa wabunge walio wengi.

... ambao waliujadili muswada huo na kuupitisha. Wangeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana hawana thamani.”

Rais Kikwete alisema vyama vya siasa na asasi za kiraia waliomba asitie saini na badala yake aliagize Bunge liujadili tena muswada huo.

“Sikutaka kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba  usiokuwa wa lazima unaoweza kuepukwa kwa kutumia njia nyingine za kisheria na kikatiba,” alisema Kikwete.

Alisema, alipofanya mazungumzo  na vikundi hivyo vya kiraia, aliwaeleza kuhusu ugumu huo wa kuacha kutia saini na kuurudisha bungeni kujadiliwa upya.

Kikwete alisema kama muswada huo ungerudishwa kujadiliwa bungeni, kuna hatari asingeweza kupata ushirikiano wao na kushindwa kupata kile kilichotarajiwa.“Wangeweza kujadili na kuamua kuyakataa mapendekezo yote mapya na kubakia na msimamo wao ule ule,” alisema.

Mauaji ya Songea
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alizungumzia mauaji ya Songea akisema, amesikitishwa na mauaji hayo, lakini akaahidi kufanyika kwa uchunguzi ili kuwashughulikia waliohusika kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema yapo mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina na yapo yaliyotokea kwenye maandamano.

“Napenda kutumia nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa vifo hivyo na kutoa pole na rambirambi zangu na za wananchi wa Tanzania, kwa ndugu wa marehemu wetu hao,” alisema Kikwete.

Aliongeza;“Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji hayo hadi wahusika wote wapatikane,” alisema.

Kikwete alisema hadi sasa yametokea mauaji ya watu  13 yanayohusishwa na imani za ushirikina na kwamba watuhumiwa 26 wamekwishakamatwa kutokana na mauaji yao.

Kuhusu mauaji yaliyotokana na maandamano, alisema askari wanne wamekamatwa na upelelezi unaendelea.

Taarifa kutoka katika Mkoa wa Ruvuma zilisema watu wanne waliuawa na Polisi wakiwa kwenye maandamano hayo.“Nashukuru kwamba amani na utulivu vimerejea katika Manispaa ya Songea, nawapongeza viongozi wa ngazi zote na wananchi kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwezesha amani kupatikana,” alisema Kikwete.