Blog yenu ya wananchi yenye habari motomoto za kijamii, Blog yenye kuelimisha, kuburudisha na kufurahisha. Wapenzi na wasomaji wetu tunaomba ushirikiano wenu ili kuendeleza Blog yetu, kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Monday, February 20, 2012

Maliasili Watoa Ufafanuzi Tuhuma Za Ubadhirifu


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU FEDHA ZA MFUKO WA TWPF

NA IDADI YA WATALII

Baadhi ya Magazeti ya tarehe 17 Februari 2012 yaliandika habari zisizo sahihi
kuhusiana na kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
cha tarehe 16 Februari 2012 kilichohusu hesabu za Wizara ya Maliasili na Utalii za
mwaka 2009/10.

Magazeti hayo yaliliripoti kuwa baadhi ya fedha zilizokusanywa katika kipindi
hicho hazikupelekwa Hazina, kila gazeti likinukuu kiasi chake cha fedha, na
mengine yakataja kuwa kulikuwa na ufisadi kuhusiana na suala hilo.

Habari hiyo ihusuyo ufisadi siyo ya kweli kwa kuwa fedha zote zinazotakiwa
kupelekwa Hazina kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii hupelekwa Hazina,
isipokuwa zile za mifuko maalum ambayo ilianzishwa kisheria, kama vile Mfuko
wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Protection Fund -
TWPF) ambao ndiyo uliohojiwa siku hiyo.

Ufafanuzi ulitolwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi
Maimuna Tarishi mbele ya Kikao hicho cha PAC na muafaka ukafikiwa kuwa
Wizara itakaa tena na Wakaguzi ili kufafanua zaidi kuhusu Mfuko wa TWPF na

1

sheria inayotawala taratibu zake za utendaji.

MFUKO WA TWPF NI KWA MUJIBU WA SHERIA

Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF) ni mfuko wa Serikali
ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1978. Aidha, Sheria ya
Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 iliendelea kutambua mfuko
huo katika Kifungu cha 91 (1) cha Sheria hiyo.

Vyanzo vya fedha zinazoingia kwenye Mfuko wa TWPF vimeainishwa katika
Kifungu cha 91 (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka
2009 kuwa ni:

(i) asilimia 25 ya maduhuli yatokanayo na Wanyamapori,
(ii) mauzo ya vitu vilivyotaifishwa chini ya Sheria ya Uhifadhi wa
Wanyamapori,
(iii) fedha zitokanazo na utalii wa picha nje ya Hifadhi za Taifa na
Ngorongoro.

Kazi zinazogharimiwa na mfuko wa TWPF zimeainishwa katika Kifungu cha 9 (2)
cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, baadhi yake
zikiwa kama ifuatavyo:

(i) kuzuia ujangili;
(ii) kulinda wananchi na mali zao kutokana na wanyama wakali na
waharibifu;
(iii) kugharimia miradi inayowanufaisha wananchi wanaoishi katika vijiji
vinavyopakana na mapori;
(iv)kufanya utafiti wa wanyamapori;
(v) kuelimisha kuhusu uhifadhi wa wanyamapori kwa kutumia Klabu za
Malihai;
(vi) kuwafunza askari wa wanyamapori.

Mfuko hugharimia shughuli hizo baada ya mipango yake kupitishwa na Bodi ya
Utendaji ya Mfuko wa TWPF.

Mfuko wa TWPF hukaguiwa na Wakaguzi wa Serikali kutoka Ofisi ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kwa mwaka 2009/10
Hoja ilihusu kwa nini fedha za mfuko huo zisipelekwe Hazina kwanza ndipo
zirudishwe kwenye mfuko.

2

Hoja hiyo ilitolewa maelezo tarehe 16 Februari 2012 na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi ambaye alitoa ufafanuzi mbele
ya Kamati ya PAC kuwa Mfuko huo ulianzishwa na Sheria, hivyo taratibu za
kukusanya mapato, pamoja na utendaji wake, hutawaliwa na Sheria husika.

Mwenyekiti wa PAC Mheshimiwa John Cheyo alihitimisha mjadala huo kwa
kuagiza kuwa wakaguzi wakae tena na Wizara ili kupata maelezo zaidi kuhusu
Mfuko wa TWPF na sheria inayotawala taratibu zake za utendaji.

IDADI YA WATALII INAJULIKANA

Suala jingine lililoripotiwa isivyo na baadhi ya magazeti ya tarehe 17 Februari2012
ni kuwa Wizara haina takwimu za watalii walioingia nchini mwaka 2009/2010.

Habari hiyo siyo kweli kwa kuwa idadi ya watalii wanaoingia nchini kila mwaka
inajulikana. Kwa mfano, kwa mwaka 2009 watalii waliotembelea Tanzania ni
714,367 ambao walilingizia taifa mapato ya Sh. Milioni 1,511,704.59 (takriban
Trilioni 1.5). Aidha, kwa mwaka 2010 idadi ya watalii ilikuwa 782,699 ambao
waliingiza Sh. Milioni 1,767,967.85 (takriban Trilioni 1.7).

Katika kikao cha PAC cha tarehe 16 Februari 2012 Hoja ilihusu ni kwa nini
takwimu zote za Wizara hazikutunzwa sehemu moja. Katibu Mkuu aliitolea hoja
hii ufafanuzi kuwa takwimu zipo ila kila Idara inatunza takwimu zake. Aliongeza
kuwa kwa sasa mifumo inaboreshwa ili takwimu zote ziweze kuwekwa pamoja
chini ya Mkurugenzi wa Sera na Mipango.

Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kufanya kazi pamoja na Wakaguzi kutoka
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kutekeleza
maagizo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.

George Matiko
MSEMAJI WA WIZARA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
20 Februari 2012
Simu 0784 468047

No comments:

Post a Comment

Msomaji wetu hakikisha unaheshimu mila na tamaduni za mwafrika,lugha zenye utata au kumkashifu mtu haitapendeza kuonekana kwenye post.Kumbuka vigezo na masharti ya comments kuzingatiwa.Asanteni sana kwa kuwa nasi kwenye blog yenu.